NA HAJI NASSOR, PEMBA::
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi, ameigaiza wizara ya Elimu na
Mafunzo ya Amali Zanzibar, kushirikiana kwa karibu na Idara ya Utumishi, ili
kuajiri waalimu nchini.
Alisema, changamoto
ya uhaba wa waalimu anajua kuwa, ipo, lakinini ni vyema kwa wizara husika,
kuongeza kasi ya kuajiri waalimu na kipaumbele, iwe ni wale ambao
walishajitolea siku za awali.
Alieleza
kuwa, wakati serikali ikijenga skuli mpya zikiwemo za ghorofa na kuzifanyia
ukarabati zile za zamani, lazima na suala la kuajiri waalimu nalo liangaliwe
kwa haraka.
Dk. Mwinyi
ameyasema hayo Mwambe wilaya ya Mkoani Pemba, mara baada ya kuifungua skuli
mpya ya ghorofa mbili ya msingi Mwambe, wakati akizungumza na wanafunzi na
wananchi wengine, ikiwa ni shamra shamra za miaka 59, ya Mapinduzi ya Zanzibar
ya mwaka 1964.
Alieleza
kuwa, anasisitiza kuwa, wakati wizara hiyo ikiajiri waalmu wakiwemo wa masomo
ya sayansi, iwape kipaumbele waalimu wenye sifa, na ambao walishawahi
kujitolea, ili kuzingatia moyo wao wa kizalendo waliouonesha.
‘’Kama
walionesha moyo wa kujitolea kwa taifa lao, kwa kuwatumikia wananchi wenzao,
sasa wakati ukifika wa uajiri, nao wapewe kipaumbele kwa wenye sifa,’’alisisitiza.
Katika hatua
nyingine Rais huyo wa Zanzibar Dk. Hussein Ali Mwinyi, ameahidi kujenga skuli
nyingine ya ghorofa eneo hilo la Mwambe, ili kukabiliana na uwingi wa wanafunzi
uliopo.
Alieleza
kuwa, ameshtushwa na idadi ya wanafunzi wanaoendelea kuandikishwa wa darasa la
kwanza kwa mwaka huu, ambao kwa sasa wameshafikia 970.
‘’Kwa hili,
lazima niwaahidi wananchi wa Mwambe na vijiji jirani kuwa, serikali itajengwa
tena skuli nyingine ya ghorofa, ili mwakani tukisherehekea miaka 60 ya
Mapinduzi, nayo iwepo,’’alieleza.
Hata hivyo
rais huyo ameelezeam kuridhishwa na usimamizi mzuri wa fedha wa shilingi
bilioni 68, walizopewa wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, kwa ajili ya ujenzi
wa skuli mbali mbali nchini.
Hata hivyo alisema,
bado serikali ya awamu ya nane, itaendelea kuona kuwa, elimu ndio kipaumbele
cha kwanza, na azma ya kujenga skuli za kisasa na vifaa vya kufundishia ipo.
‘’Ndio maana
zipo skuli 24 za zamani kwa Unguja na Pemba, zinaendelea kufanyiwa matengenezo
makubwa, ambapo kwa wilaya ya Mkoani, ni skuli za Mauwani Kiwani, Chambani na Maendeleao
Ngwachani.
Hata hivyo alisema,
ndani kipindi cha mwaka mmoja, serikali imeshajenga madarasa 143, kati ya hao
95 yalianzishwa kwa nguvu za wananchi na 48 ndio mapya, samba mba na ujenzi wa
vyoo 318 kwa skuli za maandalizi, msingi na sekondari mkoani humo.
Kuhusu
mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964, alisema kuwa, moja ya shabaha ni kuhakikisha
watoto wa taifa hili, wanapata nafasi ya kujifunza, wakiwa kwenye skuli kisasa.
Alisema,
ndio maana serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya awamu ya nane, imeweka kipaumbe
cha miradi mbali mbali ya wananchi, ikiwemo ya elimu, ili kupunguza athari za
ukosefu wa makaazi ya kisasa ya kujifunzia.
‘’Leo tukiwa
tunaadhimisha miaka 59 ya Mapinduzi ya Zanzibar, tunayo mengi ya kujivunia,
ikiwa ni pamoja sekta ya elimu, afya, miundombinu ya barabara na huduma
nyingine za kijamii, kuimarika,’’alieleza.
Kwa upande
wake Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Leila Mohamed Mussa, alisema
kasi ya Dk. Mwinyi ndani ya wizara hiyo, imesaidiai kutatua changamoto mbali
mbali, zikiwemo za maakazi.
Alisema, sio
Mwambe pekee lakini kila wilaya ya Unguja na Pemba, Rais huyo, ameshaacha alama
kwa kuhakikisha kunajengwa skuli za kisasa na za ghorofa, kuingiza na fanicha
zake kamili.
‘’Malengo ya
Mapinduzi ya Zanzibar baada ya kuasisiwa na viongozi waliotangulia, sasa
yanaendelezwa kwa kasi na serikali ya awamu ya nane, chini ya Rais wa Zanzibar Dk.
Hussein Ali Mwinyi, kwa hili hongera sana,’’alisema.
Aidha
alimpongeza Dk. Hussein kwa kuwapatia fedha shilingi bilioni 68, kwa ujenzi wa
skuli na kutia samani, na ununuzi wa vitabu, sambamba na kukamilisha ujenzi
skuli 25 za maandalizi Unguja na Pemba.
Nae Katibu
Mkuu wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Khamis Abdalla Said, alisema
ujenzi huo ambao sasa umejumuisha madarasa 46, yakiwemo 5 ya zamani
Alisema
kuwa, fedha za sherehe ya mapinduzi shilingi milioni 450, zitawasaidia kwa
ununuzi wa samani na vitambu katika skuli mbali mbali za Unguja na Pemba.
Alifahamisha
kuwa, ujenzi wa skuli hiyo na nyingine ni utekelezaji wa ahadi zake kwa
vitendo, alizozitoa kipindi cha kampeni.
‘’Skuli hii
yenye ghorofa mbili na moja ya chini (ground) ni ya kwanza kwa Zanzibar, ambayo
itapunguza changamoto ya makaazi wa wanafunzi wa Mwambe,’’alieleza.
Hata hivyo
aliafafanua kuwa, wizara tayari imeshaingiza viti, meza mpya na za kisasa ndani
ya skuli hiyo na iko tayari kwa ajili ya kuhamiwa.
Mapema Mkuu
wa Mkoa wa kusini Pemba Mattar Zahor Massoud, amewakumbusha wananchi wa Mwambe,
kuilinda miundo mbinu ya skuli hiyo.
Aidha
alieleza kuwa, sasa vipo vyumba vya madarasa 1,116 ndani ya mkoa wa kusini
Pemba, ikijumuisha hivyo 42 vya skuli ya ghorofa ya Mwambe.
Afisa
Mdhamini wizara ya elimu na mafunzo ya Amali Pemba Mohamed Nassor Salim,
alisema matayarisho ya kuongoeza idadi ya waalimu skuli hapo, yameshakaa vyema.
Mwakilishi
wa Jimbo hilo Mussa Foum Mussa, aliiomba serikali kuhakikisha kunaongezwa idadi
ya waalimu, ili kwenda sambamba na idadi ya wanafunzi.
Mwalimu mkuu wa skuli hiyo, Ali Mohamed Omar,
alisema ujenzi wa skuli hiyo, umetoa mwanga mpya wa kupata elimu kwa wanafunzi
wao.
Alisema sasa
kilichobakia ni jukumu la wazazi na walezi, kuwahimiza wanafunzi wao ili, uwepo
wa jengo hilo la ghorofa mbili, thamani yake iaendane na kasi ya kupata elimu.
Mwananchi
Hassan Kombo na Aisha Omar Ali waliipongeza serikali kwa kutimiza ahadi yake ya
ujenzi wa skuli hiyo, ambao umefanikiwa kuondoa msongamano wa wanafunzi
madarasani.
Skuli hiyo
ya ghorofa mbili ya msingi ya Mwambe wilaya ya Mkoani Pemba, ujenzi wake
umechukua mwaka mmoja, umejengwa na kampuni na Mwamba kwa shilingi bilioni
3.571 fedha za UVIKO 19, kupitia Shirika la Fedha Duniani ‘IFM’.
Mwisho
Comments
Post a Comment