NA
HAJI NASSOR, PEMBA::
WANANCHI
kisiwani Pemba, wametakiwa kuufanya mwaka mpya wa 2023, uwe wa mageuzi kwa
kupunguza matukio ya ukatili na udhalilishaji, kwa kuwatumia wasaidizi wa
sheria, ili kupata elimu, ushauri na msaada wa kisheria.
Kauli hiyo imetolewa na
Afisa sheria, kutoka Idara ya Katiba na Msaada wa kisheria Zanzibar, ofisi ya
Pemba Bakari Omar Ali, wakati akizungumza na mwandishi hizi, katika kuukaribisha
mwaka mpya.
Alisema, matukio ya ukatili
na udhalilishaji kwa wanawake na watoto bado yalikuwa yameshika kasi kwa mwaka
2022, hivyo amewataka wananchi, kwa huu 2023 uwe mwaka wa mageuzi kwa kupunguza
matukio hayo.
Alieleza kuwa, Idara
inaowasaidizi wa sheria katika kila jimbo, la uchaguzi, hivyo ni vyema
wakawatumia ili kupata uwelewa wa kisheria, sambamba na elimu ya kupambana na
matukio hayo.
Afisa sheria huyo alifafanua
kuwa, wasadizi hao wa sheria, wako tayari na saa yoyote kutoa elimu na msaada
wa kisheria bila ya malipo, hivyo ni wajibu wa wananchi, kuwa nao karibu.
‘’Zanzibar bila ya kuwa na
matendo ya ukatili na udhalilishaji kwa wanawake na watoto inawezekana sana,
ikiwa jamii itafanyakazi kazi, kwa karibu na wasaidizi wa sheria,’’alieleza.
Katika hatua nyingine Afisa
sheria huyo, amewataka wananchi kushirikiana na vyombo vya sheria, kama jeshi
la Polisi, Mahakama katika kutokomeza matendo hayo.
Alisema moja ya changamoto
iliyojitokeza kwa mwaka uliomalizika, ni kwa wananchi kutofika mahakamani kutoa
ushahidi na kusababisha kesi nyingine kuondolewa.
‘’Wapo watuhumiwa kadhaa wa
makosa ya ukatili na udhalilishaji kwa mwaka jana, wameachiwa huru, baada ya
mashuhuda wa matukio hayo, kukataa kufika mahakamani kutoa ushahidi,’’alisema.
Wakati huo huo Afisa huyo
amezitaka jumuia za wasaidizi wa sheria Pemba, kuendelea kuwa karibu na Idara hiyo,
ili kufanikisha majukumu yake mbali mbali.
Alisema kwa mwaka uliopita,
walishirikiana vyema na Idara hiyo, hali iliyopelekea kufanikisha shughuli
mbali mbali, kama mikutano ya wazi ya utoaji elimu ya kisheria.
Kwa upande wake, Mkurugenzi
wa Jumuia ya wasaidizi wa sheria wilaya ya Chake chake Pemba ‘CHAPO’ Nassor
Bilali Ali, aliipongeza Idara hiyo, kwa kuendelea kuwaamini katika utendaji wao
wa kazi.
‘’Idara ya Katiba na Msaada
wa Kisheria Zanzibar, imekua ikituamini katika utendaji wetu wa kazi, na tunashirikiana
kwa karibu, katika kufanikisha azma ya kuwafikia wananchi,’’alieleza.
Hivyo Mkurugenzi huyo, ameuhakikisha
uongozi wa Idara hiyo kuwa, kwa mwaka huu wa 2023, watazidisha kasi na
kufanyakazi kwa karibu, ili wananchi wazitambur haki zao.
Nae Mkurugenzi wa Jumuia ya
wasaidizi wa sheria Mkoani Nassor Hakim Haji, aliipongeza Idara hiyo kuwa
kufanikisha jukwaa la pili la msaada wa kisheria, lililofanyika mwishoni mwa
mwaka jana kisiwani Unguja.
Hata hivyo amewakumbusha
watendaji wenzake, kuzidisha kasi, ari na hamu ya kuwahudumia wananchi, katika
kupambana na matendo ya dawa za kulevya na udhalilishaji.
Akizungumza hivi karibuni
kwenye jukaa la pili la msaada wa kisheria, Mkurugenzi wa Idara hiyo, Hanifa
Ramadhan Said, alisema mwaka huu 2023, utakuwa mzuri kama ushirikiano
utaongezeka.
‘’Mimi najua kwenye jumuia
za wasaidizi wa sheria, zipo changamoto mfano gharama za kukodi za ofisi,
ukosefu wa usafiri, lakini tuongeze juhudi za kuwafikia wananchi popote
walipo,’’alishauri.
Baadhi ya wananchi kisiwani
Pemba, walisema kazi inayofanywa na Idara ya Katiba na Msaada wa Kisheria, kwa
kushirikiana na wasaidizi wa sheria ni kubwa, ingawa kwa mwaka huu, lazima
ushirikiano wao uongezeke.
Mnufaika wa msaada wa
kisheria kutoka shehia ya Madungu wilaya ya Chake chake, Asha Hussein Seif,
anasema upo umuhimu mkubwa wa wasaidizi wa sheria, kuendelea kujengewa uwezo.
Mwisho
Comments
Post a Comment