SAIDA
ALI, PEMBA
MAMA
mzazi ambae mwanawe mwenye ulemavu wa uziwi wa miaka 38, alifanyiwa vitendo vya
ukatili na udhalilishaji, ameviomba vyombo vya ulinzi na usalama, kuwa haki
itendeke kufuatia unyama aliodai kufanyiwa, kijana wake.
Aliyasema hayo, alipokuwa
akizungumza na waandishi wa habari, shehia ya Shumba vyamboni wilaya ya
Micheweni, kufuatia sitofahamu ya majibu ya hospitali na athari aliyonayo
kijana wao.
Alisema kuwa kitendo alichodai kufanyiwa kijana wao
huyo, ambacho alimshuhudia akiwa amefungwa mikono nyuma akiwa na tambara
mdomoni, ni cha kikatili na udhalilishaji.
Alieleza kuwa, muda wa saa 8:00 usiku baada ya
kusikia kelele za kukorota kwa kijana wake, alikimbilia chumbani kwake, na
kufika alijonea maajabu.
‘’Kwanza alikuwa amevungwa mwiili mzima nguo nyeusi
mithili ya beibui, nilishuhudia vichupa vidogo viwili, kimoja kikiwa na
majimaji, (dawa) nusu na chingine kikiwa kitupu,’’alifafanua.
Aidha mzazi huyo alisema, jingine ambalo limemshitua
kwa kijana wake huyo ambae ni kiziwi, ni kumuona na kitambaa cheusi shingoni
mwake, kukatwa nywele za kichwani na nguo yake ya ndani kuchanwa.
Aliongeza, jingine ambalo alilishuhudia usiku huo,
ni kuchinjwa mtoto wake mmoja mdogo mguuni, kunyofolewa nywele zao, na kupewa
maelekezo na watu hao kutosema chochote.
Mzazi huyo, alisema baada ya tukio hilo, alimpigia
simu sheha wa Shumba vyamboni, ingawa baada ya kujibu kuwa anaogopa usiku huo,
alipelekewa usafiri wa pikipiki (bodaboda) na kufika.
‘’Sheha alipomshuhudia kijana wangu hali ilivyo, alitushauri
tumpeleke spitali na harakati, zilianza usiku huo, na kulazwa,’’alisema.
Aliongeza kuwa, baada ya kulazwa hospitali hiyo ya
wilaya ya Micheweni, siku ya pili yake, majira ya saa 7:00 waliotolewa na
kuelezwa kwamba, mgonjwa hana shida yoyote.
Mama huyo alisema, baada ya kufika nyumbani kwao, wakati
kijana huyo, alipodai kwenda haja kubwa, aliwamuonesha mama yake, vitu
alivyotoka.
‘’Ni kweli mwanangu, baada ya kumaliza haja,
aliniita na kunionesha mapande ya damu na kifuko mithili ya glavu, ambacho
ndani yake, mlikuwa na vichupa vidogo viwili,’’alifafanua.
Kijana huyo akizungumza kwa njia ya lugha ya alama
chini ya familia yake, alisema ni kweli siku ya tukio, aliwaona vijana watatu
wakiwa wamefunika nyuso zao na kumfanyia ukatili na udhalilishaji.
‘’Chaajabu mlango na dirisha halikuvunjwa, na mimi
nilikuwa chini ya ulinzi wao, badaa ya muda sikujifahamu nilijikuta nipo
hospitali,’’alifafanu.
Aidha kijana huyo, alikiri kutokwa na vitu hivyo, na
kisha baada ya kuongezeka kwa maumivu walirejea tena hospitali, ingawa baadae
walihamishiwa spitali ya Mkoani, kwa uchunguuzi zaidi.
Sheha Shumba vyamboni Time Said Amour, ambae alikuwa
wa mwanzo kufika nyumbani kwao kijana huyo, alikiri kuona maajabu hayo siku ya
tukio.
Alisema, ni kweli alitoa rai ya kupelekwa spitali,
ingawa kwa hatua za awali, walijibiwa kuwa mgonjwa hana tatizo.
‘’Baada ya kurejea spitali kwa mara ya pili,
walihamishiwa spitali ya Mkoani, na huko walifanyiwa uchunguuzi, ambapo majibu
yake tuliarifiwa tuende baada ya siku tatu,’’alifafanua.
Baadhi ya majirani wakieleza mkasa huo, waliviomba
vyombo vya ulinzi na usalama, kufanya uchunguuzi wa kina.
Walisema, changamoto ya kijana huyo kushindwa
kujieleza, isiwe chanzo cha kukosa haki yake, kwani kwa maumivu aliyonayo, kuna
kitendo kimefanyika.
Mapame Naibu waziri Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto,
Zawadi Amour Nassor, alifika kwa familia huyo na kuahidi kushirikiana nao.
Alisema, serikali inakerwa mno ya wimbi la
kuwadhilishaji na kuwafanyia ukatili wanawake na watoto, kwani kufanya hivyo ni
kuwazimia ndoto zao.
‘’Serikali haikufurahishwa na tukio hili, na
tunaungana na familia na wanaharakati wingine, kwanza kulaani na kuwataka wawe
wastahamilivu,’’alifafanua.
Hata hivyo Naibu huyo Waziri, aliitaka familia hiyo
kuwa watulivu wakati huu vyombo vya serikali, vikiendelea na taratibu nyingine.
‘’Msikubali kughilibiwa na watu kwa kuwachochea
chochea, na endeleeni kuviamini vyombo vya ulinzi na usalama na spitali
zetu,’’alifafanua.
Kaimu Mratibu wa TAMWA-Pemba Amina Ahmed Mohamed,
alisema wamepokea kwa masikitiko tukio hilo, na kuviomba vyombo vinavyofuatilia
kutenda haki.
Alisema, wamekuwa wakiielimisha jamii siku hadi
siku, ili kujikinga na matukio hayo au vinapotokea kuviripoti maeneo husika,
kama alivyofanya mama huyo.
‘’Kwanza niipe pole familia kwa tukio hili la
kusikitisha, lakini nimpongeza mama mzazi kwa ushujaa wake wa kuripoti
changamoto hiyo,’’alifafanua.
Hata hivyo aliviomba vyombo vya habari, kufuatilia
hatua kwa hatua, tukio hilo hadi mwisho, ili kuona haki imetendeka.
Mkuu wa wilaya ya Micheweni Khatib Juma Mjaja,
aliipa pole hiyo, na kuahidi kushirikiana nayo hatua kwa hatua.
Kamanda wa Polosi Mkoa wa Kaskazini Pemba Kamishna
Msaidizi Mwandamizi wa Polisi ‘SACP’ William Mwampangale, amekiri kutokea kwa
tukio hilo na alisema hawakumbaini muhusika aliyefanya tukio hilo.
‘’Tumekagua tukio hilo na kufanya upelelezi wa kina
ingawa hadi sasa hakuna mtu tunaemshikilia hadi leo,’’alifafanua.
Daktari dhamana wa spitali ya Micheweni Khamis
Rashid Salim alisema kuwa, mgonjwa huyo alipokelewa na kufanyiwa uchunguzi wa
kina, ingawa hawakubaini madhara yoyote.
Alisema kuwa hakukuonesha tofauti yoyote ya
dalili ya kuingiliwa kwa nguvu au
kaingiziwa kitu chochote, katika sehemu zake za siri, kama familia inavyodai.
Tukio hilo lililonasibishwa na imani za
kishirikiana, lilitokea Mei 15 mwaka
huu, majira ya saa 8:00 usiku, kwa watu watatu wasiofahamika wakiwa
wameziba nyuso zao, kuingia hadi chumbani cha kijana huyo ambae ni kiziwi na
kumfanyia ukatili na udhalilishaji.
Hayo yakijiri, takwimu za Mtakwimu Mkuu wa seikali
Zanzibar, imeonesha kuwepo matukio 143 ya udhalilishaji wilaya ya Micheweni,
kuanzia mwaka 2023 hadi 2025. wastani wa matukio 48 kwa mwaka.
Maana kwa Zanzibar yote, matukio kwa kipindi hicho,
yalikusanywa 4,991, huku mwaka 2023 yakiwa 1,954, mwaka 2024 1,809 na mwaka
jana yalikuwa 1,228.
MWISHO.



Comments
Post a Comment