Skip to main content

JE WAVIJUA VIFUNGU VYA KANUNI YA UTUMISHI WA UMMA AMBAVYO SIO MAARUFU KWA WATUMISHI?

 


NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@

SIKUKUU ya wafanyakazi duniani, ni kumbukumbu ya mauaji ya halaiki ya mwaka 1886,yaliyotokea katika viwanja vya Haymarket, Chicago nchini Marekani.

 

Taarifa za mitandao zinaeleza kuwa, Polisi walikuwa wakitawanya mkusanyiko wa wafanyakazi, wakati wa mgomo wa kupinga saa nane za kazi.

 

Papa Pio XII kunako Mei Mosi, ya mwaka1955 akamteua Mtakatifu Yosefu, kuwa tegemeo, mfano na mwombezi wa wafanyakazi wote duniani.

Aliaminika kuwa, ndie atakayewasaidia kusimama kidete, kulinda na kutetea haki zao, ili kujenga na kudumisha utu, heshima, haki msingi.

Mitandao inaendelea kuripoti kuwa, jumuiya ya kimataifa, inaadhimisha sikukuu ya wafanyakazi, lengo ni kuhamasisha utoaji wa haki msingi kwa wafanyakazi wote.

Mei mosi, ni siku maalum ya kuonesha umoja na mshikamano kati ya wafanyakazi, sanjari na kuhimiza usawa na haki, katika maeneo ya kazi, sehemu mbalimbali duniani.

Kwa Tanzania, nayo mwaka 2025 kwa mara nyingine tena, iliungana na watumishi wingine duniani, kuadhimisha siku hiyo.

 

Ambapo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, aliwahutubia wafanyakazi, akiwa ndie mgeni rasmi.

 

Kwenye hutuba yake, alitoa rai kwa vyama vya wafanyakazi, kuendelea kutoa huduma na kusimamia kikamilifu, maslahi ya wafanyakazi, ili waendelee kudumu kwenye vyama hivyo.

 

Dk. Samia, akalitaka Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania ‘TUCTA’, waweke miongozo ya kutatua migogoro, baina ya wafanyakazi wa ndani ya vyama vyao, ili viwe na afya kwao na serikali.

 

Hata kwa Zanzibar, mwaka jana nayo iliungana na mataifa mingine, kuadhimisha sikukuu hiyo, ambapo awali Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji, Shariff Ali Shariff, alitoa taarifa.

 

Kwa mwaka jana, kilele cha maadhimisho hayo, kilifanyika pia kisiwani Pemba, na kusema siku hiyo ni muhimu, katika kuenzi mchango wa wafanyakazi, kwa maendeleo ya taifa.

 


Ambapo kwa mwaka jana, kauli mbiu ilikuwa ni “wafanyakazi tufanye kazi kwa bidii na nidhamu, tudai haki zetu kwa mujibu wa sheria na tushirikiane, katika uchaguzi mkuu kwa amani.”

 

Tena ikafahamika kuwa, kaulimbiu hiyo inalenga kuhimiza uwajibikaji kazini, kwa watumishi hao.

 

Watumishi wa umma wa Zanzibar, wanaongozwa na sheria na kanuni kadhaa, lengo likiwa ni kuongeza uwajibikaji miongoni mwao.

 

Moja ya Kanuni hizo ni ile ya Utumushi wa Umma ya mwaka 2014, iliyoundwa na vifungu wastani wa 134.

 

Kanuni hii, ni zao la sheria ya Utumishi wa Umma ya Zanzibar, ambayo nayo ilitungwa kwa lengo la kubainisha na kuweka wazi haki, wajibu wa watumushi wa umma.

 

Ujio wa kanuni hii, ni kama vile kuja kufafanua na kuweka taarifa kwa upana zaidi, kwa watumishi wa umma, ili kuongeza kasi, ari, hamasa na juhudi za kuwahudumia wananchi.

 

Kanuni hii ya utumushi wa umma ambayo ilisainiwa Mei, 29 mwaka 2014, kazi iliyofanywa na aliyekuwa Waziri wa Nchi ofisi ya Rrais, Kazi, na Utumishi wa Umma Zanzibar Haroun Ali Suleiman, kwa wakati huo.

 

UTEKELEZAJI WA KANUNI HIYO

Watumishi waliowengi wa umma wa Zanzibar, kwao kanuni hii, imekuwa maarufu na kuitekeleza kwenye vifungu vichache, ambavyo pingine vinamsaidia mwajiri na sio mwajiriwa.

 

Kwa mfano, wengi wa watumushi wa umma, wanaelewa kuwa, kanuni hiyo inavifungu vya kufika kazini saa1:30 na kuondoka saa 9:30 kama sio vyenginevyo, kwa wale watumishi wanaonyonyesha.

 

Ingawa vifungu vyingine maarufu kwa watumishi wa umma ni kile cha 58, kinachogusa likizo la mwaka, kifungu cha 61 cha likizo la uzazi, iwe pacha au mtoto mmoja.

 


Kifungu chingine maarufu ni cha 59 cha haki ya likizo la dharura, pamoja na ya muda na kile cha 60 cha likizo ya maradhi.

 

Kwenye kanuni hiyo, kifungu chengine ambacho ni maarufu kwa watumishi wa umma, ni bwana mkubwa, yaani kupewa mshahara, ruhusa ya kufiliwa baba, mama, mke, au mtoto.

 

Vifungu hivyo na vyingine, vimekuwa maarufu, maana watumishi wanapoajiriwa, wamekuwa wakielezwa na muajiri, ingawa vyingine huelezwa polepole, kadiri matukio yanapotokea.

 

VIFUNGU VIZURI VISIVYOTANGAAZWA HADHARANI NA BAADHI YA WAAJIRI

 

Kwa uwingi wa vifungu vya aina hiyo, vilivyomo ndani ya Kanuni ya Utumushi wa Umma ya Zanzibar ya mwaka 2014, leo tosheka na vifungu vifuatavyo, ili kuvijua uzuri wake.

 

Kifungu cha 15, kinachoelezea upandishwaji daraja kwa watumushi wa umma, ambapo kifungu kidogo (1), kinaeleza ‘kwa kuzingatia masharti ya kifungu cha 64 cha sheria, Katibu Mkuu au Mkuu wa Taasisi, atapendekeza kwa Tume ya Utumishi, husika kumpandisha daraja mtumishi yeyote wa umma’.

 

Kifungu kikazidi kufafanuwa kuwa, mtumushi huyo ni ‘mwenye sifa na ujuzi wa nafasi zinazotarajiwa kujazwa, kwa masharti, ikiwa ni pamoja na nafasi hiyo, iwe inafahamika katika miundo ya kada za utumishi.

 


‘Na mtumishi wa kujaza nafasi hiyo achaguliwe kwa mujibu wa masharti ya sheria, ambapo kupandishwa cheo, kutafanyika kwa mtumishi atakayethibitika kuwa, anao uwezo wa kushika madaraka, katika nafasi zilizowazi na  inayohitaji kujazwa’.

 

Kifungu chingine ambacho kama hakitangaazwi sana na muajiri, ni kile cha 17, ambacho kinampa haki mtumishi wa umma, aidha kukataa au kukubali cheo alichopandishwa.

 

Ingawa inamtaka mtumishi huyo, ikiwa anataka kukataa cheo hicho, afanye hivyo kwa muajiri wake kwa muda usiozidi mwezi mmoja, baada ya kuarifiwa kwake, juu ya cheo hicho.

 

Kifungu chengine ni cha 26, ambacho kimempa haki mtumishi mjamzito kikieleza kuwa, ni marufuku kwa Katibu Mkuu au Mkuu wa taasisi, baada ya kupata uthibitisho kutoka kwa daktari, kwa usalama na kwa afya ya mtumishi mjamzito, kumpangia kazi za usiku au za ziada.

 

Kifungu hicho kikafafanua kuwa, ‘ni marufuku kuajiri au kumpangia mtumishi wa kike, kufanya kazi katika eneo lolote, lenye kutumika dawa ya kemikali za sumu, benzino au mionzi, ambayo yatapelekea kuathiri uzazi au ujauzito.

 

Utamu mwingine uliomo kwenye kanuni ya utumishi wa umma, ni kwa wale wenzetu wenye ulemavu, maana kifungu cha 30, kinaeleza wazi kuwa, ‘itakapotokezea watu wa makundi maalum wana sifa sawa na watu wingine katika masharti ya ajira, kipaumbele cha ajira kitatolewa kwa watu wa makundi maalum.

 


Kipo kifungu cha 62 nacho sio maarufu sana, kinachompa haki muume, ambae ni mtumishi wa umma, cha mapunziko ikiwa mke wake, hata sio mtumishi, amejifungua kupata mapumziko.

 

Kifungu hicho kinachoundwa na vifungu viwili vidogo kinafafanua kuwa, ‘mtumishi wa umma ambae mkewake amejifungua, ataruhusika kupewa likizo ya malipo kwa muda wa siku tano za kazi.

 

Vifungu hivyo pacha vikaeleza kuwa, ’likizo hilo litachukuliwa ndani ya siku saba baada ya mtoto kuzaliwa na halitoathiri likizo yake ya mwaka na litatolewa kila baada ya miaka mitatu.

 

Zuri zaidi kanunia haikuwasahau wale watumishi wenye mke zaidi ya mmoja, iksema ‘mtumishi mwenye mke zaidi ya mmoja, atastahiki likizo la kila mke atakapojifungua, hata hivyo, endapo atakaekuwa anajifungua kila mwaka, ni mke huyo huyo, atastahiki likizo hilo kila baada ya miaka mitatu.

HALI IKOJE?

Mtumishi wa umma wa wizara ya Afya Pemba Ali Bakar, anasema amesharuhusiwa mara mbili, likizo la uzazi wa mke wake, kama Kanuni ilivyo.

 


Omar Machano Mcha wa wizara ya Elimu, anasema hata yeye amaeshawahi mara tatu, kwa miaka tofauti, kukifaidi kifungu hicho.

 

Ingawa Juma Juma Kombo wa wizara hiyo ya Elimu Pemba, anasema hajawahi kuomba wala kuruhusiwa, licha mke wake kujifungua mara nne.

 

Hidaya Haji Mussa, anasema mume wake hajawahi kumuona nyumbani, eti kwa sababu ya yeye kujifungua.

 

Afisa Mdhamini wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Pemba, Mohamed Nassor Salum, anasema hajawahi kunyima mtumishi haki yake, iwe ya fedha ama mapunziko.

 

Mfanyakazi wa wizara ya Habari Pemba Ali Suleiman, anasema sasa ana watoto watano, ingawa ni mtoto mmoja pekee, ndie alipata haki ya kupata mapunziko ya siku tano.

 

‘’Ni kweli muajiri, zipo haki nyingine huzikalia kwa watumishi wao, na wanachojua wao ni kutimiza wajibu kwa mtumishi, ikiwemo kufika kazini na kuondoka kwa wakati,’’anasema.

 

Halima Iddi Omar anayefanyakazi wizara ya Maji kwa miaka 28 sasa, anasema hakumbuki kupandishwa daraja, kama kanuni inavyoelekeza.

 

Hivi karibuni akizungumza na watendaji wake, Ofisa Mdhamini wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Pemba, Mfamau Lali Mfamau, aliwataka watumishi kuheshimu sheria.

 

‘’Niwakumbushe kufika kazini kwa wakati na kuondoka kama ilivyo kwenye Kanuni, labda kwa wale wenye dharura za kunyonyesha,’’anasema.

 

Hata Ofis Utumishi wa ofisi hiyo Khamis Massoud, alitwangaazia watumishi hao kuwa, wanaotaka kwenda masomoni, wajiorodheshe mapema, ili kuingizwa kwenye bajeti kuu.

 

                 Mwisho 

 

Comments