Katibu Mkuu Wizara ya
Ardhi na Maendeleo ya Makaazi Zanzibar Dkt Mngereza Mzee Miraji amesema wizara
yake imeshakamilisha ramani ya mji wa Serikali
kiutendaji kwa awamu ya kwanza ambapo maeneo sita yameshaainishwa kwaajili ya
kujenga mji huo.
Akizungumza mara baada ya kumaliza kikao baina ya wizara
yake na Taasisi ya Rais ufuatiliaji na Usimamizi wa utendaji Serikalini (PDB),
kilichofanyika mwisho wa wiki katika hoteli ya Golden Tulip Kiembesamaki,
Unguja, alisema ramani ya Mji wa Serikali imekamilika na muda sio mrefu Serikali itaamua wapi
ujengwe mji huo.
Dkt Mngereza aliyataja
baadhi ya maeneo ambayo wizara yake imependekeza kujenga mji wa Serikali
ikiwemo, Fumba, Kisakasaka, Dunga na Tunguu ambapo maeneo hayo kwa unguja yameonekana
yanafaa kujengwa Mji wa Serikali kutokana vigezo vinavyohitajika katika Mji wa
Serikali.
“Ni kweli mwezi mmoja uliyopita tuliwaita watendaji wa wizara zote
za Serikali tuliwaita wizarani watupe maoni yao ya mwisho ili tukafanye
marekebisho katika dizaini (design) ya Mji wa Serikali iliyokuwepo, lakini leo maeneo
yaliyoanishwa nitayataja matatu, Fumba, Kisakasaka, na Dunga. Naongeza na moja
Tunguu“ Alisema Dkt Mngereza.
Alisema chanzo cha fedha za ujenzi wa Mji wa
Serikali bado hakijafahamika lakini Serikali ikishaamua kujenga sehemu Fulani
bila shaka kutakuwa na chanzo cha fedha na bajeti yake ambapo Ofisi ya Rais
Fedha na Mipango itaeleza chanzo hicho na bajeti yake.
Pia alisema kupitia
kikao hicho kunamajukumu wamekubaliana baina Wizara ya Ardhi na Taasisi ya PDB
na majukumu hayo yametakiwa kukamilika kwa kipindi cha muda wa wiki moja.
Aidha Dkt Mngereza
waliishukuru Taasisi ya Rais Ufuatiliaji wa Usimamizi Utendaji Serikalini (PDB)
kwa kuanda kikao cha pamoja na Wizara yake kwa lengo la kuleta ufanisi katika utekelezaji
wa majukumu ya Wizara ya Ardhi Zanzibar.
Naye Mkurungenzi Mkuu
Shirika la Nyumba (ZHC) Mwanaisha Ali Said alisema kikao hicho ni muhimu sana
kwasababu ZHC bado inachangamoto ya kiutendaji ikiwemo fedha, jinsi ya kupata
fedha na jinsi ya kuandika maandiko ya kupata fedha na vipaumbele mbali mbali.
“PDB imekua taasisi
muhimu kwa ZHC kwa kutumia utaalamu wao katika sekta ya nyumba na sekta ya uendeshaji miradi wametusaidia
kutuongoza kwani vipaumbele vya Mhe Rais wa Zanzibar Dkt Hussein Ali Mwinyi ni
vingi hata vipaumbele vya Shirika la Nyumba Zanzibar pia ni vingi” Alisema
Mwanaisha.
Kwa upande wake Mkuu
wa kitengo cha Mawasilino na Habari Kutoka Taasisi ya Rais Ufuatiliaji na
Usimamizi wa Utendaji Serikalini (PDB) Dr. Mohamed Mansour Nassor alisema
Taasisi yake imeweza kujua Shirika la Nyumba Zanzibar namna gani linavyofanya kazi,
mikakati yake , mafanikio pamoja na changamoto.
Alisema kikao hicho
ni muendelezo wa vikao vya PDB na Wizara
mbali mbali za Serikali katika kufuatilia utekelezaji wa miradi ili waweze
kujua ni changamoto zipi zinazoikabli miradi hiyo na kuipatia ufumbuzi ili
kufikia malengo ambayo Mhe. Rais wa Zanzibar Dkt Hussein Ali Mwinyi anataka katika
uongozi wake.
MWISHO
Comments
Post a Comment