NA
HAJI NASSOR, PEMBA:::
WANAKIKUNDI
cha watu wenye ulemavu, kiitwacho ‘USHAURI’ kilichopo shehia ya Pandani wilaya
ya Wete Pemba, wanaojishughulisha na kilimo cha njugu, wameshauriwa kujitenga
mbali na migogoro, kwani ndio sumu inayoweza kuwagawa na kurudi tena, kwenye
umaskini.
Ushauri huo umetolewa leo Januari 26, 2023 na Mratibu wa Baraza la Taifa la
watu wenye ulemavu Zanzibar ofisi ya Pemba, Mashavu Juma Mabrouk, wakati
akizungumza na mwandishi wa habari hizi, mara baada ya kumaliza ziara maalum,
ya kukitembelea kikundi hicho.
Alisema, vikundi vingi huanzishwa kwa furaha na malengo,
mikakati mikubwa, lakini mwisho wa siku wanachama hufarakana kwa kuingia kwenye
migogoro.
Alieleza kuwa, suala la migogoro ni jambo lisiloepukika,
lakini suala la kuitatua ni jambo la lazima, ili kutimiza ndoto na azma ya
kuanzisha umoja wao.
‘’Niwatake wenzetu hawa wenye ulemavu kuwa, kikundi chao
hichi kisijekikaparaganyika, kwa kule kuikaribisha migogoro, kwani, mnaweza
kurudi tena kwenye umaskini,’’alieleza.
Aidha Mratibu huyo alisema, ziara hiyo aliyoifanya ni
kuangalia mafanikio, changamoto na mwelekeo wa kikundi hicho, ili kuona wapi wanahitaji
kusaidiwa.
Katika hatua nyingine, alisema tayari wamewakabidhi mbegu
za njugu mawe kilo tano na mbegu za matikti, kwa ajili ya kuendeleza mbele eneo
lao lililobakia hapo awali.
‘’Kwa sasa kilichomo chao cha njugu mawe na nyasa
zimeshakuwa vizuri, lakini wamekuwa na hamu ya kuendeleza mbele kilimo hicho na
ndio maana, tumeshawakabidhi mbegu,’’alisema.
Hata hivyo Mratibu huyo, aliwakumbusha kuwa, mvuno wa
mwanzo watakapovuna, wajihadhari na kuwagawana faida, hadi kupelekea kurudi
tena kwenye kuomba mbegu.
Mapema Mwenyekiti wa kikundi hicho cha ‘ushauri’ Seif
Omar Ali, alisema kwa sasa wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa maji ya
uhakika.
Alisema, kilimo chao kinategemea mno huduma ya maji kwa
kiwango kikubwa, hivyo kwa sasa wamekuwa wakitumia maji kwenye mashimo waliyoyachimba
kienyeji.
‘’Tumeshaanza na tunandelea kupanda mbegu za njugu mawe
na nyasa, na tumeshaanza na kilimo cha matikti, lakini maji ndio changamoto
hapa,’’alieleza.
Kwa upande wake Katibu wa kikundi hicho, Rashid Hamad Khamis,
alisema wanamatumaini makubwa, kufikia ndoto zao ikiwa watapatiwa mikopo ya
masharti nafuu, kuendeleza kazi zao.
Alisema, tayari ardhi wanayo na hamu ya kufanyakazi ipo,
lakini suala la ukosefu wa mtaji ya uhakika, ndio jambo ambalo wanaendelea
kuumiza kichwa.
‘’Ukiangalia kikundi hichi kimenzishwa mwezi Oktoba mwaka
2022, lakini kwa sasa tumeshapiga hatua, kwa kua na kilimo cha njugu na matikti
tena kwa gharama zetu,’’alieleza.
Wanachama wa kikundi hicho Salim Ali Salim na mwenzake
Salim Rubea, wamesema wanamatumaini kuwa, kuungana kwao katika kikundi hicho,
matunda yatapatikana.
Kikundi cha ‘Ushauri’ cha watu wenye ulemavu mchanganyiko
ambacho kinawanachama 15, wakiwa wanawake saba na wanaume wanane, kimeanzishwa
Oktoba, 2022 na tayari kwa sasa wameshapanda njugu mawe, nyasa na matikti.
Mwisho
Comments
Post a Comment