NA
HAJI NASSOR, PEMBA::
MRATIBU wa Chama Cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania TAMWA-Zanzibar ofisi ya Pemba
Fat-hya Mussa Said, amesema sheria zenye mapungufu katika mapambano dhidi ya
ukatili na udhalilishaji, ni changamoto nyingine inayohitaji kufanyiwa kazi.
Alisema kwa mfano, sheria Adhabu nambari 6 ya mwaka 2018,
kwenye vifungu vyake vya 108 na 109 vilipotaja kosa la ubakaji na dhabu, hakuna
adhabu sawa kwa washitakiwa wa kosa la aina moja.
Mratibu huyo aliyasema hayo Januari 24, mwaka 2023 ofisi
ya TAMWA Chake chake Pemba, wakati akiyafunga mafunzo ya siku mbili, kwa waandishi
wa habari, kwenye mradi wa Kuhamasisha hatua za kitaifa, dhidi ya kupinga vitendo
vya ukatili na udhalilishaji, unaoendeshwa na tasisi za TAMWA, KUKHAWA, TUJIPE,
ZAFELA na ZAMWASO.
Alisema, bado sheria zinaendelea kuwaweka njia panda
wananchi, kwa kule washtakiwa wa makosa ya ubakaji, kupewa adhabu tofauti, na
sio iliyotajwa kwenye sheria husika.
‘’Kwa mfano, wapo wanaotiwa hatiani kwa ubakaji, hufungwa
miaka 20, mwengine miaka 15 na mwengine miaka 30, hii ni kasoro inayohitaji,
kufanyiwa kazi,’’alieleza.
Katika eneo jingine, Mratibu huo wa TAMWA Pemba, alisema
bado kundi la watu wenye ulemavu na vijana, wamekuwa hawaamini na jamii hasa
katika eneo la uongozi.
Alieleza kuwa, jamii imekuwa na mtazmo mbaya kuwa watu
wenye ulemavu, hawezi kuongoza, jambo ambalo sio sahihi.
‘’Kwa kasoro ziliomo ndani ya baadhi ya sheria na imani potofu
kwa jamii, ndio maana tunafanyakazi na waandishi wa habari, ili kwenda kuibua
hayo, ili yafanyiwe kazi,’’alieleza.
Akiwasilisha mapungufu ya sheria mbali mbali, Mwanasheria
wa serikali Ali Amour Makame, alisema yapo makosa kwa mfano kwenye sheria
Adhabu kifungu cha 116, kunajisi mtu mwenye ulemavu awe mtoto, mtu mzima
mtuhumiwa, anaweza kupewa dhamana.
Aidha alisema kasoro iliyopo, kosa la ubakaji kwa mtu
mwenye akili timamu, mtuhumiwa hawezi kupewa dhamana, jambo ambalo linaukakasi.
Kasoro nyingine alisema, ni pamoja na upelelezi wa makosa
ya udhalilishaji kukosa muda maalum, pamoja na kukosekana kwa miundombinu
rafiki, kwenye mahakama ya watoto.
Hivyo Mwanasheria huyo, amesema hayo yanaweza kuwa vizuri
ikiwa waandishi wa habari, watafanyakazi kazi zao kwa ufanisi.
Hassan Msellem mwandishi wa habari wa Bahari FM, alisema
kuwa, kazi iliyoko mbele yao ni kuziibua changamoto hizo, ili kuona zinafanyiwa
kazi, na ufanisi katika mapambano dhidi ya ukatili na udhalilishaji.
Salim Ali Msellem wa kituo cha redio cha Ist-qama,
alisema kama kufanya mapenzi na mwari sio kosa, ni vyema sheria ikaliunganisha,
kama ilivyo kumpa ujauzito kuwa ni kosa.
‘’Ukimpa ujauzito mwari kwa mujibu wa sheria ni kosa,
usipompa sio kosa, sasa napendekeza yote haya yawe makosa, maana ni uvujifu wa
maadili, kwa jamii,’’alishauri.
Kwa upande wake, Amina Ahmed mwandishi wa Zenj fm
alisema, ni vyema sheria ya sasa ya mwari aliyepata ujauzito kutumikia jamii,
iondolewe kwani, itakuwa amempa adhabu mara mbili.
Afisa mawasiliano wa TAMWA Pemba Gaspery Charles, alisema
anawategemea sana waandishi hao, kwenda kuibua hayo, ili kuwa na sheria nzuri.
Awali mafunzo hayo yalifunguliwa na Mkurugenzi Mtendaji
wa TAMWA-Zanzibar Dk. Mzuri Issa Ali, ambae alisema, vyombo vya habari ni
jukwaa muhimu katika mageuzi ya sheria mbali mbali.
Mradi huo wa miaka miwili, unafadhiliwa na the foundation
for civil Society, na unaendeshwa na Jumuiya ya wanasheria wanawek Zanzibar
ZAFELA, KUKHAWA, TUJIPE, ZAMWASO na TAMWA Zanzibar.
Mwisho
Big up mafunzo ni mazuri sana ila msiangalie sheria moja tu bali sheria nyingi zinamapungufu
ReplyDelete