NA
HAJI NASSOR, PEMBA::
MKURUGENZI
Mtendaji wa Chama Cha waandishi wa habari wanawake Tanzania TAMWA-Zanzibar Dk.
Mzuri Issa Ali, amesema, bado vyombo vya habari vitaendelea kuwa tegemeo kwa
jamii, katika kuwabadilisha kutoka mtazamo finyu na kwenda wenye tija.
Dk. Mzuru aliyasema hayo leo Januari 23, 2023 wakati
akifungua mafunzo pacha, kati ya waandishi wa habari wa Unguja na Pemba, kwa
njia ya kielektronik, kwenye mafunzoi ya siku mbili, chini ya mradi wa
Kuhamasisha hatua za kitaifa dhidi ya kupinga vitendo vya ukatili na
udhalilishaji, unaoendeshwa na tasisi zaTAMWA, KUKHAWA, TUJIPE, ZAFELA na
ZAMWASO.
Alisema, vyombo vya habari ni jukwaa muhimu na limeshafanya
magauzi kadhaa, ikiwa ni pamoja na kusababisha kupatikana kwa sheria mbali
mbali zikiwemo za kupinga udhalilishaji na adhabu zake.
Alieleza kuwa, ndio maana TAMWA katika kutekeleza kazi
zote, lazima kuwashirikisha waandishi wa habari, ili kuhakikisha wanachotaka
kukifanya, iwe rahisi kupata matokeo.
‘’Bado vyombo vya habari, vimekuwa eneo muhimu kwetu sisi
wadau, kwa kule kufanya kazi zao kwa ufanisi, na kusababisha uwepo wa mabadiliko
makubwa,’’alieleza.
Katika hatua nyingine, Mkurugenzi huyo Mtendaji wa
TAMWA-Zanzibar Dk. Mzuri Issa Ali, aliwakumbusha waandishi hao, kuendelea
kuibua changamoto za uongozi kwa wanawake, watu wenye ulemavu na fursa za
kiuchumi kwa vijana.
Akizungumza kabla ya mafunzo hayo, Mratibu wa TAMWA-Pemba
Fat-hya Mussa Said, alisema mradi huo, unalenga kuibua changamoto, hasa zinazowakwaza
wanawake na watu wenye ulemavu, zinazopelekea wasifikie malengo yao.
‘’Kundi la vijana, wanawake na watu wenye ulemavu nayo
yanahaki sawa kama yalivyo mengine, sasa iweje yakose kuaminiwa na jamii, ni
wajibu wa vyombo vya habari kwenda kuona nini tatizo,’’alihoji.
Akiwasilisha mada ya ushiriki na ushirikishwa wa wanawake,
vijana na watu wenye ulemavu katika siasa, uongozi, uchumi na fursa nyingine,
mwanaharakati Sabah Mussa, alisema kama vyombo vya habari, vitatumia mbinu
mbadala, makundi hayo yataishi kwa salama.
Alieleza kuwa, vyombo vya habari vimeshasababisha mabadiliko
ya sheria na mitazamo mbali mbali, hivyo kama vitendelea kujengewa uwezo,
makundi hayo yatapata haki za fursa zao.
Mwandishi wa Mawio online tv Suleiman Rashid, alisema bado
elimu ya kujitambua kwa vijana inahitajika, ili waaminiwe ndani ya jamii yao,
pale wanapotaka kugombea nafasi mbali mbali.
Mwandishi wa habari wa ZBC Pemba, Khadija Kombo Khamis,
alisema uwezeshwaji na ufuatiliaji kwa vyombo vya habari, ni jambo moja,
linalohitajika kufanyika.
Mwandishi wa blog ya pemba ya leo Fatma Hamad, alisema
moja ya changamoto ambayo inaendelea kujitokeza na makundi hayo kukosa haki
zao, ni elimu ya kuondoa dhana potofu kwa jamii.
Mradi huo wa miaka miwili, unafadhiliwa na the foundation
for civil Society, na unaendeshwa na Jumuiya ya wanasheria wanawek Zanzibar
ZAFELA, KUKHAWA, TUJIPE, ZAMWASO na TAMWA Zanzibar.
Mwisho
Comments
Post a Comment