Skip to main content

WANAWAKE VIJANA WENYE ULEMAVU, NGUVU ISIYOTAMBULIKA KIKAMILIFU KATIKA UONGOZI, MAENDELEO

 



 NA HABIBA ZARALI PEMBA@@@@

 KILA siku wanawake vijana wenye ulemavu, huamka wakiwa na ndoto kama vijana wengine kupata elimu, kujiajiri, kushika nafasi za uongozi na kushiriki katika maamuzi, yanayogusa maisha yao. 

 

Mara nyingi ndoto hizo, hukwama si kwa sababu ya ukosefu wa uwezo, bali ni vikwazo, vinavyotokana na mitazamo hasi ya jamii, unyanyapaa na kukosekana kwa mifumo jumuishi.

 

Katika kipindi ambacho dunia inaendelea kusisitiza usawa wa kijinsia, haki za binadamu na maendeleo jumuishi, wanawake vijana wenye ulemavu, bado ni miongoni mwa makundi yanayokabiliwa na changamoto kubwa za kutoshirikishwa. 

 

Licha ya kuwa na uwezo, elimu na vipaji, wengi wao hukosa nafasi, kutokana na mazingira yasiyowawezesha kushiriki kwa usawa.

 


Awena Khamis Rashid, mwenye ulemavu wa ngozi (albino), kutoka mkoa wa kaskazini Pemba, anasema wao mara nyingi, hushirikishwa kwa jina tu, lakini si kwa vitendo.

 

Maana hupewa mwaliko kwenye mikutano, warsha na majukwaa mbalimbali, lakini maoni yao hayapewi uzito unaostahili, wingine.

 

“Wakati mwingine, tunaitwa kwenye mikutano ili kuonekana tumeshirikishwa tu, lakini mawazo yetu hayaingii katika maamuzi ya mwisho,’’anasema.

 

Katija Mbarouk Ali kutoka wilaya ya Wete, mwenye ulemavu wa viungo, anasema changamoto kubwa wanayokutana nayo, si uwezo wao, bali mtazamo funyu wa jamii, unaowafanya waonekane hawafai kuwa viongozi.


“Pamoja na kujitolea kwetu, bado jamii inatuchukulia kuwa watu wasio na uwezo, na wasiostahili kupewa nafasi yoyote,’’anafafanua. 

 

Hali hiyo wakati mwingine, hutufanya wakose ushirikiano unapojitokeza katika nafasi za uongozi au vikao ngazi ya shehia.

 

Amekuwa akishiriki katika nafasi mbalimbali za uongozi, ikiwemo kuwa mjumbe wa Jumuiya ya Watu Wenye Ulemavu wilaya ya Wete, mjumbe wa Baraza la Vijana Taifa, Katibu wa Kikundi cha Elimu Mkombozi Wete, msaidizi wa sheria na mjumbe katika ngazi mbalimbali za kijamii.

 


Aliwahi kugombea nafasi ya uwakilishi wa viti maalum mwaka 2015, na mwaka 2025 aligombea nafasi ya uwakilishi wa Jimbo la Kojani, ingawa hakufanikiwa kushika hatamu.

 

Mkasi Simai Makame, mwenye ulemavu wa kuona kutoka wilaya ya Mkoani, anasema wakati mwingine watu wenye ulemavu, hualikwa kwenye mikutano kama sehemu ya kutimiza idadi ya washiriki, na sio vyenginevyo.

 


Anasema changamoto hizo zilianza tangu akiwa mdogo, ambapo aliwahi kufungiwa ndani, kwa miaka kadhaa kutokana na imani kuwa, ulemavu wake ulimfanya ashindwe kufanya jambo lolote.

 

“Nilionekana siwezi lolote, lakini baada ya kutolewa ndani na kupelekwa skuli, nilianza kuamini uwezo wangu, leo najishughulisha na kazi zangu na najitegemea,” anasema.

 


Mratibu wa Baraza la Taifa la Watu Wenye Ulemavu Zanzibar upande wa Pemba, Mashavu Juma Mabrouk, anasema wanawake wenye ulemavu, wana uwezo mkubwa wa kuwa viongozi, iwapo watawezeshwa na kuaminiwa.


“Wanawake wenye ulemavu wana uwezo wa kuongoza kama watu wengine, kinachohitajika ni kuondoa vikwazo vinavyowazuia kushiriki kikamilifu, katika maendeleo na maamuzi,” anasema.

 

Kwa mujibu wa Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa serikali (OCGS), kwenye taarifa yake mwaka 2024, inaonesha kuwa mwaka 2023, Zanzibar ilikuwa na watu 8,100 wenye ulemavu waliosajiliwa, wakiwemo wanawake 3,838 na wanaume 4,262.

 


Afisa Programu wa ‘WYDE’ kutoka TAMWA, Sophia Ngalapi, anasema ushiriki wa wanawake wenye ulemavu katika uongozi una umuhimu mkubwa, kwa sababu huwapa nafasi ya kuwakilisha mahitaji ya makundi ambayo mara nyingi husahaulika.



Hata hivyo, bado wanawake wengi wenye ulemavu hukosa fursa za elimu bora, mafunzo ya uongozi, ajira, mikopo na nafasi za kushiriki, katika vyombo vya maamuzi

 

Shirika la Afya Duniani (WHO), linaarifu kuwa, zaidi ya watu bilioni 1.3 duniani wanaishi na aina fulani ya ulemavu, sawa na takribani asilimia 16 ya idadi ya watu duniani.

 

Hali hiyo inaonyesha umuhimu wa kujenga jamii inayojumuisha watu wote, katika nyanja mbalimbali za maisha.

 

Shirika la Umoja wa Mataifa la Wanawake (UN Women) linaeleza kuwa, wanawake wenye ulemavu hukabiliwa na changamoto za ubaguzi unaotokana na jinsia pamoja na ule unaotokana na ulemavu wao. 

 

Hali hiyo imechangia kundi hilo, kuwa na uwakilishi mdogo katika nafasi za uongozi, ajira na maamuzi.

 

Nalo Shirika la Kazi Duniani (ILO), linabainisha kuwa, wanawake wenye ulemavu wako katika hatari kubwa zaidi ya kukosa ajira na fursa za kujitegemea, kiuchumi kuliko wanawake wasio na ulemavu.

 


Aidha, UNICEF inaeleza kuwa elimu jumuishi ni msingi muhimu wa kuwawezesha watoto na vijana wenye ulemavu, kushiriki kikamilifu katika maisha ya baadaye.

 

Sheria ya Watu Wenye Ulemavu Na. 8 ya mwaka 2022 inatambua haki ya watu wenye ulemavu kupata fursa sawa katika elimu, ajira, huduma za jamii na ushiriki katika maendeleo bila ubaguzi.

 

Sera ya Taifa ya Watu Wenye Ulemavu ya mwaka 2004, kwenye ibara zake kadhaa, inalenga kuondoa vikwazo vinavyowazuia kushiriki kikamilifu katika maendeleo.

 

Katika ngazi ya kimataifa, Tanzania imeridhia Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Watu Wenye Ulemavu (CRPD), wa mwaka 2006 ambao unatambua haki za wanawake wenye ulemavu kushiriki katika maisha ya kisiasa na maamuzi ya umma.


HATUA ZINAZOCHUKULIWA

Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto Pemba, Mwanaisha Ali Massoud, anasema serikali imeendelea kuweka programu za kuwawezesha wanawake wenye ulemavu, kwa kuwapatia mafunzo ya uongozi, mikopo na fursa katika vikundi vya kiuchumi.

 

“Hakuna mtu anayepaswa kuachwa nyuma katika masuala ya kiuchumi, kisiasa, uongozi na kijamii,” anasema.

 


TAMWA Zanzibar inasisitiza kuwa hatua inayohitajika sasa si kutunga sheria mpya pekee, bali kuhakikisha sheria zilizopo zinatekelezwa kikamilifu.

 


Shirika hilo linashauri kuongeza uwakilishi wa wanawake wenye ulemavu katika taasisi za umma, vyama vya siasa, sekta binafsi na kamati za maendeleo. 

 

Pia linashauri kuimarishwa kwa elimu jumuishi, teknolojia saidizi, lugha ya alama, miundombinu rafiki na kampeni za kuondoa unyanyapaa.

 


Awena Khamis Rashid anasema watu wenye ulemavu wangepewa nafasi maalumu za uwakilishi ili waweze kusimamia changamoto zao katika ngazi za maamuzi.

 


Naye Mwanaisha Ali Massoud anasisitiza umuhimu wa kuwaandaa watoto wenye ulemavu tangu wakiwa wadogo kupitia familia, shule na mabaraza ya watoto ili wajenge kujiamini na uwezo wa kushiriki katika uongozi baadaye.


HITIMISHO

Wanawake vijana wenye ulemavu si kundi la kuhurumiwa, bali ni nguvu muhimu katika ujenzi wa jamii na taifa.

 

Changamoto inayowakabili si ukosefu wa uwezo, bali ni vikwazo vya kijamii, kimazingira na kimfumo vinavyowazuia kutumia uwezo wao kikamilifu.

 

Kuwapa nafasi wanawake wenye ulemavu katika uongozi na maamuzi si hisani, bali ni haki yao ya msingi.

 

Zanzibar na Tanzania kwa ujumla zitafikia maendeleo jumuishi pale kila mwananchi atakapopewa nafasi sawa ya kushiriki na kuchangia katika maendeleo ya taifa.

 

MWISHO

 



Comments

BLOG'S VISITORS

DAKTARI MWENGINE CHAKE CHAKE KULA SIKUKUU POLISI, NI KWA TUHUMA ZA KUMBAKA MGONJWA WAKE

NA WAANDISHI WETU, PEMBA::: DAKTARI anaetoa huduma kwa wagonjwa kituo cha afya cha serikali cha  Gombani wilaya ya Chake Chake Pemba, Is-haka Rashid Hadid, anaendelea kushikiliwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa kaskazini Pemba, akituhumiwa kumtorosha na kisha kumbaka mtoto wa mwenye umri wa miaka 16, mkaazi wa Gombani. Daktari huyo miaka 35 ni mkaazi wa Kangagani Wilaya ya Wete mkoani humo, ambapo anadaiwa alimchukua mtoto huyo kutoka kwa rafiki yake, na kumpeleka kwenye nyumba anayoishi eneo la Kangagani. Mtoto aliefanyiwa kitendo hicho alisema kuwa, April 21 mwaka huu alikwenda kituo cha afya Gombani, kwa ajili ya matibabu na baada ya kupatiwa huduma na daktari huyo, alimuomba nambari yake ya simu. Alisema ilipofika usiku, walikuwa wanawasiliana kupitia ujumbe mfupi (sms) kwa lengo la kwenda kuchukua dawa nyingine ambazo kwa mchana huo alizikosa hospitalini hapo. "Nilikwenda hospitali kutibiwa, baada ya kufanya mapele katika sehemu zangu za siri, lakini akaniambia mpaka aje da...

HII KALI MBUNGE ASIYA AMKOGESHA MWANANCHI HADHARANI KISA HICHI HAPA......

  NA HAJI NASSOR, PEMBA MBUNGE wa viti maalum nafasi za wanawake mkoa wa kaskazini Pemba Asiya Sharif Omar, amewataka wananchi wa kijiji cha taifu, shehia ya Kinyasini jimbo la Gando wilaya ya Wete Pemba, kuyalinda miundombinu ya maji safi na salama, ili yawe endelevu kwao. Kauli hiyo ameitoa wakati alipokuwa akizungumza na mwandishi wa habari hizi, mara baada ya kuwasili kijijini humo, na kumkogesha mwananchi mmoja kama ishara ya uzinduzi wa mradi wa maji safi na salama, ulioasisiwa na mbunge wa Jimbo la Gando. Alisema, hawana mbadala kwa sasa bali ni kuilinda miundombinu ya huduma hiyo, hasa baada ya mbunge wa wao Salim Mussa Omar, kuwarejeshea huduma hiyo. Alieleza kuwa, inafahamika kuwa kwa miaka 14 waliikosa huduma hiyo hasa kwa vile viongozi waliokuwepo hawakujali kuwatatulia tatizo hilo, hadi juzi ilipofanywa na mbunge wao. “Baada ya huduma hii sasa kurejeshwa na mbunge wa jimbo la Gando, kazi iliyobakia kwenu wananchi ni kila mmoja kuwa mlinzi wa miundombinu hii,’...

'MKAPA' NA WENZAKE PEMBA WALAZWA RUMANDE

  NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@ MAHKAMA kuu Zanzibar kisiwani Pemba, chini ya Jaji Ibrahim Mzee Ibrahim, imewapeleka rumande watumuhimwa wanne wanaokabiliwa na tuhuma za kuua kwa makusudi, akiwemo Ali Mussa Omar ‘ Mkapa’ mkaazi wa Wawi wilaya ya Chake chake Pemba. Watuhumiwa wengine walioanza maisha mapya ya rumande ni mtuhumiwa Yassir Mohamed Juma miaka 23, Anuwari Mussa Omar miaka 30 pamoja na mtuhumiwa Yassir Mussa Omar ‘ Makababu ’ miaka 29, wote wakaazi wa shehia ya Wawi, wilaya ya Chake chake Pemba. Awali watuhumiwa hao waliwasili mahakamani hapo, kwa mara ya kwanza, kwa ajili ya kusomewa tuhma zinazowakabili za kumuua kwa maksudi Said Seif Kombo. Ilidaiwa mahakamani hapo na Mwendesha Mashtaka kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashataka Seif Mohamed Khamis akiambatana na mwenzake Mussa Khamis Ali kuwa, watuhumiwa hao kwa pamoja wanadaia kufanya mauwaji hayo kwa maksudi. Ilidai kuwa, watuhumiwa wote kwa pamoja, walitenda kosa hilo Oktoba 16, mwaka huu, baina ya saa 7:00 m...

TUHMA ZA DAKTARI PEMBA KUCHIWA HURU: POLISI KASKAZINI KUTOA TAARIFA RASMI LEO

  NA HAJI NASSOR, PEMBA KAMANDA wa Polisi mkoa wa kaskazini Pemba, Juma Saad Khamis, amesema leo Mei 9, mwaka huu atatoa taarifa rasmi, juu ya kuendelea kumshikilia au kumpa dhamana ya Polisi, daktari wa Kituo cha Afya Gombani Is-haka Rashid Hadid, anayetuhumiwa kwa ubakaji. Alisema, kwa vile alikuwa katika mapumziko mafupi, haelewi jambo lolote linaloendelea kwa mtuhumiwa huyo, juu ya kuendelea kushikiliwa kwake kituoni hapo. Alieleza kuwa, leo Mei 6 (jana), hajapata taarifa za ndani za mtuhumiwa, huyo na kuwataka wananchi na wanaharakati, wasubirie hadi Jumatatu ijayo. Akizungumza na waandishi wa habari kwa nyakati tofauti Kamanda huyo, alisema hana taarifa zozote za kupewa dhamana mtuhumiwa ndani ya kituo chake cha Polisi au kuendelea kuwepo. ‘’Ilikuwa mimi sipo kazini kwa muda, kuanzia anakamatwa hadi anafikishwa Polisi, kwa sasa siwezi kueleza jambo lolote kwa mtuhumiwa huyo, hadi Jumatatu,’’alieleza. Aidha Kamanda huyo alieleza kuwa, kwa sasa hawezi kutoa uf...

MADAKTARI KUTOKA CHINA WAOKOA MAISHA YA MTOTO PEMBA

  HABIBA ZARALI, PEMBA TIMU ya 32 ya madaktari wa kichina katika hospitali ya Abdalla Mzee Mkoani wamefanikiwa kufanya upasuaji mkubwa wa mtoto mwenye umri wa miaka 15 mkaazi wa Chole Kengeja, baada ya kuchomwa na jiti sehemu ya njia zake za mfumo wa uzazi. Mtoto huyo ambae alianguka hivi karibuni katika mti na baadae kuchomwa na jiti hilo na kumsababishia kutokwa na damu nyingi katika sehemu ya nyonga, alifanyiwa upasuaji uliodumu kwa muda wa saa tatu na   kuokolewa maisha yake. Akizungumza mara baada ya operesheni huo kiongozi wa timu hiyo Dr Jiang Jinhua, alisema mara baada ya mtoto huyo kufikishwa hospitalini hapo na kufanyiwa vipimo na kuonekana   ilibidi apatiwe rufaa ya kwenda katika hospitali nzuri yenye kutibu tatizo lake huko nchini Kuwado ambapo haikuwezekana kutokana na hali ya umaskini wa f amilia ya mtoto huyo . Alisema timu ya madaktari hao itaendelea kutowa huduma za matibabu   kwa wananchi kisiwani humo,   ili kuwaondolea gharama ya kuta...