NA ZUHURA JABIR, ZANZIBAR @@@
Wanawake ni nguzo muhimu katika maendeleo ya familia, jamii
na taifa. Kwa miaka mingi, juhudi mbalimbali zimefanywa na Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na
taasisi za kiraia ili kuhakikisha wanawake wanapata haki sawa za kushiriki
katika uongozi na maamuzi ya maendeleo.
Pamoja na hatua hizo,
bado wanawake wengi hukutana na changamoto zinazowazuia kufikia nafasi za
uongozi kutokana na mila na desturi, mitazamo hasi ya kijamii, ukosefu wa fursa
za elimu na uwezeshaji wa kiuchumi.
Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, pamoja na marekebisho yake, na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 zinatambua usawa wa watu wote mbele ya sheria bila ubaguzi wa kijinsia. Aidha, Tanzania imeridhia mikataba mbalimbali ya kimataifa inayolinda haki za wanawake, ikiwemo Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Kutokomeza Aina Zote za Ubaguzi dhidi ya Wanawake (CEDAW),
Itifaki ya Maputo ya Umoja wa Afrika kuhusu Haki za Wanawake
Afrika na Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs), hususan Lengo la Tano
linalohimiza usawa wa kijinsia na kuwawezesha wanawake na wasichana wote.
Akizungumza kuhusu nafasi ya wanawake katika uongozi, Bikame
Sheha Ussi, Mkuu wa Divisheni ya Pensheni, Jamii na Maendeleo ya Wazee, anasema
hata historia za dini zinaonesha wazi kuwa wanawake hawajazuiwa kuwa viongozi.
Anaeleza kuwa dini zimekuwa zikisisitiza zaidi maadili, uwajibikaji na uadilifu
kuliko jinsia ya kiongozi.
“Kwa
upande wa Dini ya Kiislamu haijakataza mwanamke kuwa kiongozi, bali inasisitiza
kuzingatia mipaka na maadili,”
anasema.
Kauli hiyo inaondoa dhana inayotumiwa na baadhi ya watu
kwamba dini ndiyo kikwazo kikubwa cha wanawake kushika nafasi za uongozi.
Badala yake, inaonesha kuwa tafsiri potofu za dini pamoja na mila na desturi
ndizo zinazochangia kuwanyima wanawake nafasi za kushiriki kikamilifu katika
maamuzi ya kijamii na kisiasa.
Naye Mkurugenzi wa Ustawi wa Jamii na Wazee, Hassan Ibrahim
Suleiman, anasema wanawake wana uwezo mkubwa wa kuwa viongozi katika ngazi zote
kuanzia familia, jamii hadi taifa endapo watapatiwa fursa sawa za elimu,
mafunzo na uwezeshaji wa kiuchumi.
Hata hivyo, anaeleza kuwa bado kuna vikwazo vinavyowakabili
wanawake wengi. Miongoni mwa changamoto hizo ni masharti ya baadhi ya ndoa ambapo
waume huwazuia wake zao kushiriki katika shughuli za kijamii na kisiasa,
utegemezi wa kiuchumi unaotokana na ukosefu wa kipato cha kutosha, pamoja na
vitendo vya rushwa ya ngono vinavyowakatisha tamaa wanawake wanaotafuta nafasi
mbalimbali za uongozi.
Kwa mujibu wake, pamoja na juhudi za serikali na mashirika
yasiyo ya kiserikali, bado baadhi ya familia huendelea kuwekeza zaidi katika
elimu ya wavulana kuliko wasichana kwa kuamini kuwa wanaume ndio tegemeo kuu la
familia. Mtazamo huo huwanyima wasichana fursa za kujijengea msingi wa elimu na
uongozi tangu wakiwa wadogo.
Anasema pia uongozi ni mchakato unaohitaji muda, kujituma,
uvumilivu na dhamira thabiti. Hata hivyo, wanawake wengi hukabiliwa na mzigo
mkubwa wa majukumu ya kifamilia, mfumo dume na mitazamo hasi inayowafanya
washindwe kushiriki kikamilifu katika shughuli za kisiasa na kijamii.
Kwa upande wake, Makamu Mstaafu wa Rais wa Chuo Kikuu cha
Zanzibar (ZU), Nunu Issa Juma, anasema elimu imekuwa silaha muhimu iliyomjengea
mwanamke uwezo wa kujiamini, kujieleza na kushiriki katika maamuzi yanayogusa
maendeleo ya jamii.
“Kupitia
elimu, nimepata ujasiri mkubwa wa kujieleza na kusimamia hoja zenye msingi,” anasema.
Anafafanua kuwa elimu humwezesha mwanamke kutambua haki zake
za msingi, kuelewa sheria mbalimbali na kushiriki kwa ufasaha katika mijadala
ya kijamii, kisiasa na kitaifa. Elimu pia humsaidia mwanamke kujenga uwezo wa
kufanya maamuzi sahihi na kujilinda dhidi ya vitendo vya ubaguzi na
unyanyasaji.
Kwa mujibu wake, mafanikio ya mwanamke katika uongozi hayaji
kwa bahati mbaya bali yanahitaji juhudi binafsi, nidhamu, kujifunza kila wakati
na mazingira yanayotoa fursa sawa kwa wanawake na wanaume.
“Wanawake
wanaweza kuwa viongozi bora endapo jamii itabadilisha mtazamo kwamba mwanamke
ana uwezo wa kuongoza,”
anasisitiza.
Anabainisha kuwa Chuo Kikuu cha Zanzibar kupitia Dawati la
Jinsia kinaendesha programu mbalimbali zinazowajengea wanafunzi wa kike uwezo
wa uongozi, kujiamini na kutambua haki zao. Programu hizo huwapa wanawake
vijana nafasi ya kuandaliwa kuwa viongozi wa baadaye katika sekta mbalimbali za
maendeleo.
Kwa upande wa vyombo vya habari, Khairat Ali, Afisa wa
Programu na Mawasiliano kutoka Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania
(TAMWA Zanzibar), anasema taasisi hiyo imeendelea kuwajengea uwezo waandishi wa
habari kuhusu uandishi unaozingatia usawa wa kijinsia, haki za wanawake na
uongozi.
“Tunaendelea
kuwafundisha waandishi wapya kila baada ya muda kwa sababu tunataka waandishi
wote Zanzibar wawe na uelewa kuhusu masuala ya wanawake, uongozi na haki za
kidemokrasia,”
anasema.
Anasema vyombo vya habari vina nafasi kubwa katika kubadili
fikra za jamii kwa kuandika habari zenye kuhamasisha ushiriki wa wanawake
katika uongozi na kupinga dhana zinazowadhalilisha wanawake. Waandishi wa
habari wanapaswa kuandika habari zinazotoa nafasi sawa kwa wanawake na wanaume,
huku wakiepuka lugha zinazoweza kuendeleza ubaguzi wa kijinsia.
Wataalamu wa maendeleo ya kijamii wanaeleza kuwa ushiriki wa
wanawake katika uongozi huongeza uwajibikaji, uwazi na utofauti wa mawazo
katika kufanya maamuzi. Tafiti mbalimbali pia zimeonesha kuwa taasisi zenye
uwakilishi mzuri wa wanawake katika nafasi za maamuzi huwa na uwezo mkubwa wa
kusimamia maendeleo jumuishi yanayozingatia mahitaji ya makundi yote ya jamii.
Ili kuongeza idadi ya wanawake katika nafasi za uongozi,
kuna haja ya kuendelea kuwekeza katika elimu ya mtoto wa kike, kuwajengea
wanawake uwezo wa kiuchumi, kuimarisha utekelezaji wa sheria zinazolinda haki
za wanawake na kuhamasisha jamii kubadili mitazamo inayowabagua wanawake.
Aidha, wanaume wanapaswa kushirikishwa kama wadau muhimu katika kuhamasisha
usawa wa kijinsia badala ya kuona mafanikio ya wanawake kama tishio.
Kwa ujumla, wanawake wana uwezo mkubwa wa kuwa viongozi wenye
maono, uadilifu na mchango chanya katika maendeleo ya taifa. Hata hivyo,
mafanikio hayo yatapatikana pale ambapo jamii itaondoa vikwazo vya kijinsia,
itawekeza katika elimu na uwezeshaji wa wanawake na kuhakikisha sheria pamoja
na mikataba ya kitaifa na kimataifa inayolinda haki za wanawake inatekelezwa
kwa vitendo. Safari ya kufikia usawa wa kijinsia si jukumu la wanawake pekee,
bali ni wajibu wa jamii nzima kuhakikisha kila mwanamke anapata nafasi ya
kutimiza ndoto zake za uongozi bila ubaguzi wala vikwazo visivyo vya lazima.




Comments
Post a Comment