NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@
WANAWAKE wa kijiji cha Mleteni shehia
ya Kisiwani wilaya ya Wete, wameikumbusha serikali kuwajengea kituo chao cha
Afya, kama ahadi ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.
Hussein Ali Mwinyi, alivyoitoa wakati alipowatembelea.
Walisema,
tayari wameshakuwa na eneo ambalo walitakiwa kulitoa kwa ajili ya ujenzi wa
kituo hicho cha afya, ingawa hadi sasa ni miezi zaidi ya mitano tokea Rais
atowe ahadi, ingawa hakujaanza ujenzi.
Wakizungumza
na mwandishi wa habari hizi kijijini hapo, walisema wanahamu kubwa na kujengewa
kituo hicho, ili sasa kwao iwe rahisi, kupata huduma mbali mbali zikiwemo za
uzazi na mtoto.
Walieleza
kuwa, wamekuwa wakiifuata huduma hiyo eneo la Kisiwani ambapo pana umbali wa
zaidi ya meli mbili, jambalo linalowapa ugumu, hasa kutokana na uchakavu wa
barabara yao.
Mmoja
kati ya wanawake hao Aisha Nassir Sheha, alisema kutokana na umbali wa kituo
cha afya hasa huduma za mama na mtoto, wengi wao wamekuwa hawamalizi mtiririko
wa kuhudhuria kliniki.
‘’Zipo
baadhi ya siku hutakiwa kufika kliniki kwa ajili ya uchunguuzi, lakini kutokana
na umbali na uchakavu wa barabara yetu, hukatisha,’’alisema.
Alieleza
kuwa, inakuwa vigumu kwa mjamzito kuanzia miezi sita kutembea umbali mrefu,
kufuata huduma Kisiwani, na hasa kutokana na uchakavu wa barabara yao.
Kwa
upande wake Husuna Mohamed Kombo,
alisema hakuna hata mjamzito mmoja anaemaliza siku kamili za kuhudhuria kliniki
eneo la Kisiwani, kutokana na umbali uliopo hadi hospitalini.
‘’Ni
vyema kwa serikali kutimiza ahadi yake ya ujenzi wa kituo cha afya kijiji cha
Mleteni, ili wananchi sasa tuwe na uhakika wa huduma,’’alieleza.
Katika
hatua nyingine, mwananchi huyo alisema, kama huduma nyingine ikiwemo umeme, maji
na skuli imeshajengwa, ni wakati sasa na kituo cha afya kujengwa.
Kwa
upande wake Mkubwa Abdalla Yussuf, alisema kutokana na uchakavu wa barabara
yao, hata gari inakuwa ni usumbufu kuwafuata wagonjwa au wajawazito.
Hivyo
ameikumbusha serikali, kutekeleza ahadi yake ya ujenzi wa kituo cha afya, hasa
kwa vile tayari wameshapata eneo karibu na skuli yao ya maandalizi.
Kaimu
Sheha wa shehia ya Kisiwani wilaya ya Wete Bahati Juma Mtwana, alisema ni kweli
eneo kwa sasa wameshalipata na wananchi waliwashi kuliondolea vichaka hivi
karibuni.
Mkuu
wa wilaya ya Wete Dk. Hamad Omar Bakar, alisema ujenzi wa kituo cha afya bado
uko pale pale, ingawa umechelewa kutokana na kukamilisha miradi walioiomba
mwanzo wananchi hao.
Alieleza
kuwa, baada ya kufika Rais wa Zanzibar Dk. Hussein Ali Mwinyi kijijini hapo,
wananchi hao kwanza waliomba skuli ya maandalizi ambayo tayari imeshajengwa.
‘’Kisha
waliomba huduma ya maji safi na salama na huduma ya umeme, na tayari huduma
hizo zimeshafikishwa kijijini hapo kwa muda mfupi,’’alieleza.
Hata
hivyo Afisa Mdhamini wizara ya Afya Pemba Khamis Bilali Ali, amewataka wananchi
na hasa akina mama kuendelea kukitumia kituo cha afya cha Kisiwani.
‘’Wajawazito
wanatakiwa kuhakikisha wanahudhuria kliniki, kwa ajili ya kupata maendeleo ya
mama na mtoto, kwani kinyume chake kunaweza kukajitokeza matatizo,’’alieleza.
Wakati
rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi
alipowatembelea wananchi hao, aliwaahidi kuwafikisha huduma kadhaa za kijamii
ikiwemo umeme, afya, elimu, maji na barabara.
Comments
Post a Comment