Skip to main content

HAKI YA AFYA YA UZAZI JUKUMU LA WOTE: TAMWA-ZANZIBAR

 



NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@

JAMII imekumbushwa kuwa, suala la afya ya uzazi, sio jukumu la mwanamke pekee, kama wengine wanavyofikiria, bali linahusu jamii yote, ili kuwa na afya bora iwe ya kimwili au kiakili.  

Kauli hiyo imetolewa leo Julai 29, 2023 na Afisa Mradi wa haki ya afya ya uzazi kutoka Chama cha waandishi wa habari wanawake Tanzania TAMWA- Zanzibar Zaina Abdalla Mzee, wakati akiutambulisha mradi huo, kwenye mafunzo ya siku tatu kwa waandishi wa habari, kisiwani Pemba.

Alisema, imegundulika na tafiti zinaonesha kuwa, linapozungumza suala la haki ya afya ya uzazi, huangaliwa zaidi mwanamke, bila ya kumuhusisha mwanamme.

Alieleza kuwa, hakuna suala la uzazi linalomgusa mwanamke pekee, na hasa likihusisha afya, kwani mwanamme asipowajibika, anaweza kusababisha madhara kwa mjamzito na mtoto wake.




‘’Hii ndio maana, TAMWA-Zanzibar imeibua mradi huu ambao sasa utawawezesha waandishi wa habari, kuieleza jamii, madhara ya kutozingatia haki ya afya ya uzazi na faida zake,’’alieleza.

Katika hatua nyingine, Afisa huyo mradi wa haki ya afya ya uzazi, alisema anaviamini mno vyombo vya habari, katika kuieleza jamii, maana ya afya ya uzazi kwa ufasaha.

Akifungua mafunzo hayo, Afisa ufuatiliaji na tathmini kutoka TAMWA- Zanzibar Mohamed Khatib Mohamed, alisema utafiti unaonesha kuwa, vyombo vya habari viko chini katika kielimisha jamii kwa ufasaha, juu ya haki ya afya ya uzazi.

Alifahamisha kuwa, kupitia mradi huo, anatarajia kuona mafanikio kadhaa, moja wapo ni kupunguzika kwa vifo vya mama na mtoto na ushiriki wa wanaume, katika afya ya uzazi.



Hata hiyo Afisa huyo, alieleza kuwa, bado katika jamii zipo dhana potofu kadhaa, ikiwemo uleaji mimba, mtoto na majukumu ya ndani, kuendelea kuachiwa mwanamke pekee.

‘’Waliowengi hawaoni athari ya mwanamke kukosa kwenda kilini kwa wakati, kukosa lishe bora wakati wa ujauzito na hata kutosindikizwa anapokwenda kliniki, haya yanaweza kumpoteza mtoto yasipozingatiwa,’’anasema.

Akiwasilisha mada ya mtazamo wa dini ya kiislamu, juu ya afya uzazi, Sheikh Abdalla Nassor Abdalla ‘Mauli’ kutoka Jumuiya ya Maimamu Zanzibar ‘JUMAZA’ alisema hilo linazia tokea uchaguaji wa mwenza, katika ndoa.

‘’Uislam umeelekeza hata namna ya kumuendea mwenza wako, namna ya kuilea mimba, ushiriki wa mwanamme kabla na baada hata ya kuzaliwa mtoto,’’alieleza.




Hata hivyo sheikh huyo, alisema uislamu ndio muanzilishi wa uzazi wa mpango, pamoja na uimarishaji wa afya ya mjamzito pamoja na uleaji na makuzi ya mtoto.

Kwa upande wake, Mratibu Tume ya Ukimwi Zanzibar ofisi ya Pemba Ali Mbarouk Omar, alisema waandishi wa habari wazuri, ni wale wanaozijua istilahi za haki ya afya uzazi, ili iwe rahisi, wakati wa kuwaelimisha wananchi.

‘’Kwa mfano ujue nini maana ya umri baleghe, utoaji mimba ulioruhusiwa, mimba zisizotarajiwa, umuhimu wa haki ya afya ya uzazi pamoja na athari za kuzaa kila mwaka,’’alifafanua.

Wakichangia kwenye mafunzo hayo, waandishi hao wa habari walisema, elimu hiyo kwao ilikuwa mpya na hawakua na uwelewa wa kutosha.



Mwandishi wa blog ya Pemba ya leo, Fatma Hamad Faki, alisema hakuwa akijua kuwa, anaweza kupata maeneo mengi ya kuwaelimisha wananchi, juu ya afya uzazi.

Meneja wa redio Jamii Micheweni Ali Massoud Kombo, alisema wamekuwa wakifanya vipindi vya aina hiyo kwa muda mtefu, ingawa hakuwa na uwelewa kwa baadhi ya mambo.

Mwandishi wa kujitegemea Hassan Msellem, alisema sasa amejua kuwa, dini haikatazi kufanya vipimo na mtarajiwa, ili kuelewa uwezo baina yao.

Maradi huo wa majaribio wa mwaka mmoja, unaendeshwa katika wilaya za Magharibi B, Kati kwa Unguja na wilaya ya Chake chake kwa Pemba.

Ambapo mradi huo unatekelezwa kwa ushirikiano kati ya TAMWA-Zanzibar na wenzao wa Tanzania bara, unafadhiliwa na Shirika la Wellspring Philonthropic fund la Marekani.




Ambapo shabaha kuu ya mradi huo ni kuwajengea uwezo waandishi wa habari, ili kuripoti kwa ufanisi, juu ya haki ya afya ya uzazi kwa wanawake na wasichana walioko mjini na vijijini.

                  Mwisho

Comments