NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@
WANANCHI 710, wakiwemo
wanafunzi wa kike 663, sambamba na wasikilizaji 4,800 wa redio mbalimbali,
wamefikiwa na elimu ya kisheria, haki za binaadamu, kupitia mradi uliokuwa ukiendeshwa
na Jumuiya ya wasaidizi wa sheria Wete ‘WEPO’ hivi karibuni.
Hayo yalibainishwa
na Mratibu wa Uwezeshaji wa upatikanaji wa haki, kutoka ‘WEPO’ Rashid Hassan
Mshamata leo Mei 10, 2026 skuli ya sekondari ya Utaani Wete, wakati wa
mjadala wa wazi.
Alisema, wapo waalimu
na wazazi, wakimwemo wanawake 27 na wanaume 19, walifikia wakati wa utekelezaji
wa mradi huo.
Alieleza kuwa, kwa
sasa matumaini yao, ni kuona jamii, imebadilika na waliokalia haki za wingine,
sasa wanapata haki zao, kama sheria zilivyo.
Alifafanua kuwa,
kwa mfano waligundua ipo familia, ambayo, haijarithi kwa miaka 30 sasa, ambapo
wanaume, wamekalia mirathi, jambo ambalo linaendelea kuwanyima haki wingine.
‘’Mradi huu,
tulifanya shughuli kadhaa, lakini mafanikio yapo, maana hata wakati wa urushaji
wa vipindi vya moja kwa moja, wapo wanachi 146, walituma ujumbe mfupi,’’alifafanua.
Aliongeza kuwa,
watu hao wapo waliouliza maswali, wapo walielezea kutofahamu masuala ya ardhi,
mirathi na wingine, wakitoa ushauri kwa vyombo vya sheria.
Katika hatua nyingine,
Mratibu huyo wa mradi wa Uwezeshaji wa kisheria katika kufikia haki, Rashid
Hassan Mshamata, alisema wasikilizaji wastani wa 4,800 nao walifikiwa na elimu
hiyo.
Kuhusu kuwafikia
wananchi walioko visiwa vya Fundo, Uvinje, Kojani na Njau, alisema walikwenda
kufanya mikutano ya ana kwa ana.
‘’Tulihisi kuwa,
kwa kutumia vyombo vya habari pekee, tungaliwanyima elimu hiyo, na hili
lilithibitika wakati tulipokwenda, walilalamikia kutosikia vyombo vya habari,’’alifafanua.
Mapema Mlezi wa
jumuiya za kiraia mkoa wa kaskazini Pemba, Mohamed Hassan Ali, alisema bado elimu
ya kisheria, inahitajika, kwa jamii.
Alisema, bado zipo
changamoto za uwelewa mdogo wa matumizi ya ardhi, uuzaji, mirathi na haki za
binaadamu, kutotambuliwa vyema.
‘’Niwapongeze sana ‘WEPO’,
juu ya kuendelea na utendaji wao kazi, na wajue kuwa bado jamii inahitaji
ushauri, elimu na msaada wa kisheria.
Mapema Mwandishi wa
habari wa kituo cha tv cha Chanel ten, Masanja Mabula alishauri mikutano na
ufikishaji wa elimu, kuwatumia wasanii.
Nae aliyekuwa Mratibu
wa TAMWA Zanzibar ofisi ya Pemba,
Fat-hya Mussa Said aliishauri ‘WEPO’ kutumia mitandao ya kijamii, kufikisha
elimu kwa jamii.
‘’Endeleeni kutumia
redio na magazeti ya kawaida, lakini ujumbe mfupi mfupi, itengenezeni na mtumie
face book, Tick Tok, ili kuona vijana wanafikiwa na elimu,’’alishauri.
Nae Msaidizi wa
sheria kutoka ‘WEPO’ Said Rashid Hassan, alisema bado katika maeneo ya visiwa, kunahitajika
nguvu ya pamoja na taasisi nyingine.
‘’Kwa mfano wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, inatakiwa kuongeza elimu, ya nini maana ya elimu, hasa maeneo ya visiwa,’’alisisitiza.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa ‘WEPO’ Hemed Ali Hemed, aliahidi kuvitumia vyombo vya habari mtandaoni, ili kuyafikia makundi yote.
Mradi huo wa Uwezeshaji
wa kisheria katika kufikia haki, ulikuwa unatekelezwa na WEPO na wadau wao
Idara ya Katiba na Msaada wa Kisheria, kwa kushirikiana na UNDP wakifadhiliwa
na Ubalozi Iceland.


Comments
Post a Comment