Dk. Mwinyi aliyasema hayo jana Septemba 15, 2025 katika
mkutano wa uzinduzi wa kampeni za CCM katika kiwanja cha Gombani ya Kale,
wilaya ya Chake chake kisiwani Pemba.
Alisema hatua hiyo
itawezesha wamiliki hao kuzalisha kwa wingi na hata pale watakapofariki
basi, warithi wao wanaweza kuyarithi, kisheria kwa ajili ya kuyaendeleza.
Mgombea huyo
alisema CCM ikiendelea kushika dola basi hayo yote yatatimia kwa asilimia 100,
kama ilivyofanya kwa awamu iliyopita.
Alifahamisha kuwa,
wamiliki wa mashamba hayo ya eka, wamekuwa wakipata changamoto kwa kule
kuyatunza, kisha kukosa hata kukodishwa wao.
‘’Naomba mnipe
ridhaa ya kuiongoza tena Zanzibar, na pamoja na mambo mingi, lakini nitahakikisha
wanaoyashughulikia mashamba ya mikarafuu ya eka, wanapewa hati ya umiliki,’’alifafanua.
Aidha Mgombe huyo ambae
pia ni Rais wa Zanzibar, alisema serikali, mwishoni mwa mwezi huu, inatarajia
kumkabidhi mkandarasi kazi ya ujenzi wa uwanja wa ndege Pemba, pamoja na ujenzi
wa barabara Chake chake- Mkoani.
Alisema hatua hiyo
ni dhamira za serikali kuifungua Pemba kiuchumi, na kukiwezesha kiwanja hicho
kupokea ndege kubwa za kimataifa pale kitakapokamilika.
Alisema mpango huo,
utakwenda sambamba na kuendeleza ujenzi wa barabara ya Chake Chake Mkoani,
hatua ambayo itaunganisha mikoa mbalimbali kisiwani humo, na kurahisisha
shughuli za usafiri.
‘’Niwahakikishe
wananchi wa Pemba, kuwa mwishoni mwa mwezi huu, natarajia kumkabidhi mkandarasi
kazi ya ujenzi wa barabara ya Chakechake- Mkoani, pamoja na ule ujenzi wa
uwanja wa ndege wa kimataifa Pemba,’’alisisitiza.
Aidha Mgombea huyo,
alisisitiza dhamira yake ya kuendeleza amani, umoja na mshikamano na kuondoa
aina zote za ubaguzi, ukabila au uasili kwa wananchi.
Alisema wakati
anaingia madarakani, aliahidi jambo hilo kuondoa ukabila baina ya Unguja na
Pemba, ukaskazini na ukusini na uasili, jambo ambalo amefanikiwa kwa asilimia
kubwa.
Alisema nchi ili
ipate maendeleo, ni lazima kuwa na amani na umoja mshikamano, na hakuna mbadala
katika jambo hilo.
"Sisi
tutaendeleza umoja wa wananchi wote, hili ndio jambo muhimu kwetu, ili nchi
yetu iendelee kupiga hatua za kimaendeleo,"alisema.
Mgombea huyo
alisema wananchi wa Zanzibar hawataki chuki, fitna na ubaguzi, bali wanataka
amani na maelewano, na sio jambo jingine lolote na wanaoweza kufanya
hivyo ni CCM pekee.
Katika hatua
nyingine, amewahidi wananchi hao, kama Oktoba 29, watampa kura za kumuwezesha
kuwa Rais wa Zanzibar, ataendeleza ujenzi wa barabara, bandari, kuendeleza
makundi yote ikiwemo, wakulima wa mwani, ili kuwawezesha kwa zana za kisasa na
mikopo.
Aliahidi kuwa CCM
itaendeleza kazi ya ujenzi wa skuli, ili kufikia lengo lake la wanafunzi wote
kuingia mkondo mmoja pekee, na sio miwili, kama ilivyo hadi sasa kwa baadhi
skuli za Zanzibar.
"Tutaendeleza
kujenga skuli za sekondari na msingi, ili dhamira yetu ya watoto kuingia mikondo
miwili sasa iwe basi,"alisisitiza.
Kuhusu huduma za
afya, alisema serikali itaendelea kuweka vifaa tiba, katika hospitali ya
Abdalla Mzee Mkoani, hasa kuiwezesha kutoa huduma ya upasuaji wa uti wa
mgongo.
Kwa upande wa maakazi
bora ya gharama nafuu, alisema ana lengo la kujenga nyumba 10,000 Unguja na
Pemba, ili kuhakikisha watu wanapata makaazi mazuri, na tayari kumeshatengwa
fungu maalum la bajeti.
Alitumia nafasi
kujiombea kura na kuwaombea kura viongozi wengine wa CCM akiwemo mgombea uris
wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan, wabunge,
wawakilishi na madiwani ili kwa pamoja, waweze kushirikiana katika kuleta
maendeleo.
Nae Katibu Mkuu wa
CCM taifa Balozi, Asha Rose Migiro, aliwaomba wazanzibari, kuchukua maoni ya
viongozi wao, ili kuhakikisha Oktoba wanawapigia kura wagombea wote wa CCM,
ili iendelee kuwatumikia.
Kwa upande wake
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM taifa, Mohamed Aboud Mohamed,
amempongeza mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi upitia Chama Cha Mapinduzi
(CCM), Dk. Hussein Ali Mwinyi, kwa kuendeleza maendeleo.
Alisema Dk. Mwinyi
ameonesha ubingwa wa kutekeleza Ilani ya CCM ya uchaguzi yam waka 2020/2025 kwa
unyenyekevu, subira na kwa kuzingatia mahitaji ya wananchi wake.
Aboud amebainisha
kuwa, kiongozi huyo amejikita katika kujenga mshikamano na umoja wa
wazanzibari, jambo lililogusa nyoyo za wananchi wengi.
Aidha, amewaomba wananchi kuwa Oktoba 29, 2025 wananchi watajitokeza kwa wingi kumpa kura Dk. Mwinyi pamoja na wagombea wengine wa CCM kutokana na kazi kubwa aliyoifanya.
Alisema sasa ni
wajibu wa wananchi kulipa ihsani kwa kutumia fursa ya kura, kuendeleza neema
hiyo, kwani Dk. Mwinyi ameweka mikakati thabiti ya kuimarisha maisha ya
wananchi, na kubaki nguzo muhimu ya kulinda misingi ya taifa.
‘’Niwaombe wananchi
kukataa watu wanaochochea chuki na mifarakano na shari unaoashiria umwagaji damu,
maana hayo sio maendeleo yanayotafutwa,’’alifafanua.
Kwa upande wake
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Mohamed Said Mohamed ‘Dimwa’ alisema mgombea urais
wa Zanzibar kupitia CCM, Dk. Hussein Ali Mwinyi, ndie kinara wa siasa za
maendeleo ya Zanzibar, kutokana na dira na maono yake.
Alisema ilani ya uchaguzi
ya CCM, imetoa mwelekeo mahsusi wa kuijenga Zanzibar mpya, yenye ushindani wa
kiuchumi na ustawi wa kijamii, jambo linaloendana moja kwa moja na falsafa ya
uongozi ya Dk. Mwinyi.
Alisisitiza kuwa, Ilani
hiyo imejikita katika maeneo muhimu ikiwemo mapinduzi ya uchumi, kuongeza fursa
za ajira, kuimarisha sekta ya habari na mawasiliano.
‘’Ustawi wa watu na
jamii kwa ujumla pamoja na kuimarisha miundombinu ya usafiri ni nguzo kuu,
zitakazohakikisha Zanzibar, inafikia hatua kubwa ya maendeleo chini ya uongozi
wa Dk. Mwinyi na hasa akipata tena ridhaa,’’alifafanua.
Aidha alibainisha
kuwa, ilani imeweka sehemu kuu ya kuchochea mapinduzi ya kiuchumi na
kisiasa, kuongeza ajira na kupunguza umasikini, ambayo ni kipaumbele kikubwa.
Akizungumzia kuhusu
amani, alisema kwa sasa ipo na maridhiano, mshikamano na demokrasia ya kweli na
kuahidi CCM, itaendelea kufanya kampeni za kistaarabu kwa kuthamini umoja na
utu.
Akizungumzia
maendeleo yaliyofanyika kisiwani Pemba kwa miaka mitano iliyopita, alisema
serikali ya awamu ya nane, imejenga skuli za ghorofa13 na kuajiri walimu 2,406
sawa na asilimia 40 ya walimu wote waliopo Pemba.
Makamu wa Pili wa
Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdullah, alisema wazanzibari wamedhihirisha
mapenzi waliyoyanyo kwa Dk. Hussein Ali Mwinyi, kutokana na maendeleo yaliofikiwa.
Alisema changamoto
kubwa, ilikuwa ikiwakabili wananchi wa kisiwa hicho, wagonjwa wenye matatizo ya
figo, ingawa kwa sasa, huduma za ugonjwa huo zinapatikana katika hospitali ya
Abdallah Mzee, bila ya gharama.
Hivyo, aliwaomba wananchi kisiwani humo, kuwachagua
viongozi wote wa CCM na kutokubali kudanganywa na watu, ambao hawana muelekeo
mzuri kwa wazanzibari, wakihubiri chuki na dharau kwa waanchi.
Mapema Mwenyekiti
wa Umoja wa Vijana, Mohamed Kawaida, alisema visiwa vya Zanzibar, kabla ya kufanyika
kwa mapinduzi mwaka 1964, vilitawaliwa na mkoloni, ingawa baada ya chama cha
ASP na kisha CCM kushika hatamu, maendeleo yalipatikana.
Alisema Rais Mwinyi
ameimarisha sekta mbali mbali ikiwemo elimu, kwa kiwango kikubwa kwa
ujenzi wa skuli za ghorofa, ambayo hayo ni mageuzi makubwa.
Wakati huo huo, mgombea
huyo wa urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM, aliwapokea wanachama 453 kutoka chama
cha ACT-Wazalendo, baada ya kukihama chama hicho.
Aidha kabla ya
hutuba yake, kulitanguliwa na shamra shamra kadhaa, ikiwemo tumbuizo za
wasanii, nyimbo za hamasa na matembezi maalum ya vyombo vya moto.
mwisho









Comments
Post a Comment