NA FATMA HAMAD, PEMBA@@@@
WANANCHI wamehimizwa kujitokeza hospitali kupima
afya zao, wakati wanapojihisi na dalili za ugonwa wa kifua kikuu, ili kujigundua
mapema na kupatiwa, na sio kukimbilia kwa waganga wa jadi.
Kauli hiyo imetolewa na Afisa
Habari TEHAMA na Mawasiliano kutoka Kitengo shirikishi Ukimwi, Homa ya Ini,
Kifua kikuu, na Ukoma Khalifan Khamis Khalifan, wakati akizungumza na mwandishi
wa habari hizi, Ofisini kwake Chak chake.
Alisema kwa mujibu wa utafiti wa
Shirika la Afya Duniani (WHO) unaonesha
kwamba, ugonjwa wa kifua kikuu upo, ingawa bado wagonjwa kugundulika ni shida.
Alisema takribani asilimia 80 ya
wagonjwa kuwagundua inapotea, na hubakia katika jamii na kutumia dawa za waganga wa jadi.
‘’Licha ya jitihada zinazofanyika
kuondosha ugonjwa huo, bado watu hawaji hospitali, wanakwenda kwa waganga wa
jadi, kwani wanaimani kwamba wamerogwa,’’alisema.
Alieleza kuwa, wananchi
waliowengi wanaamini kwamba kifua kikuu, ni maradhi yatokanayo na ushirikina,
hivyo hukimbilia kwa waganga, jambo linalopelekea kuenea kwa maambukizi ya
ugonjwa huo kwa kasi.
‘’Mtu anapoona dalili za kifua
kikuu, haendi hospitali na hata anaekuja na tukamgudua hatumii dawa zetu, bali
anatumia mitishamba na wingi hupoteza maisha,’’alieleza.
Alisema ugonjwa wa kifua kikuu
unatibika, hivyo ni vyema wanajamii kufika vituo vya afya kupima afya zao
kuweza kugundulika na kupatiwa tiba mapema, ili kuepusha kuenea kwake.
Alifahamisha kuwa ugonjwa wa kifua
kikuu unaambukizwa kwa njia ya hewa, hivyo
mgonjwa anaeugua maradhi hayo na kama hajanza kutumia dawa, inakua ni rahisi
zaidi kuambukiza.
Akitaja dalili za ugonjwa huo alisema
ni pamoka na kukohoa kwa muda wa wiki mbili mfululizo au zaidi, kupungua uzito,
kukonda bila sababu yoyote, kupata homa za mara kwa mara hasa inapofika wakati wa jioni.
Dalili nyingine ni kutokwa na
jasho jingi wakati wa usiku hata kama ni kipindi cha baridi, makohozi yaliochanganyika
na damu.
Alisema matibabu ya maradhi hayo
ni miezi sita mfululizo, ambapo dawa hutolewa bure na zinapatikana saa 24, bila
ya gharama yoyote.
Alisema maranyingi wagonjwa
wanaowapata na kuwaanzishia matibabu, ni wale ambao walishashindikana kwa
waganga, na kuamua kuenda hospitali.
Fatma Khamis Ali, mkaazi wa
kisiwa cha Pemba alisema baada ya kuumwa na kifua, alikwenda kwa mganga na
kutumia dawa, ingawa hakupata nafuu hadi alipokwenda hospitali na kuanza matibabu.
‘’Nilishahangaika kwa muda wa miaka
miwili sijafanikiwa, ila nilipokwenda hospitali, nikagundulika nina TB, nilianzishiwa
dawa na sasa nimeshapona,’’alisema.
Mkurugenzi mkuu kutoka Shirika la
afya Duniani WHO Dokta Tedros Adhanom Ghebreyesus, alisema juhudi za kimataifa
za kutokomeza kifua kikuu, zimeshaepusha vifo milioni 750 tangu mwaka 2000, hata
hivyo ugonjwa huo husababisha vifo vya watu milioni 1.3 kila mwaka.
MWISHO.
Comments
Post a Comment