NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@
MGOMBEA
urais wa Zanzibar kwa tiketi ya ACT- Wazalendo Othman Massoud Othman, amesema kama
akipata ridhaa ya kuingoza Zanzibar, atasimamisha utawala wa sheria na haki,
ikiwa ni njia moja wapo ya kukuza uchumi.
Alisema, haiwezekani
wananchi kupata maendeleo endelevu, kama hakuna utawala wa sheria, ambao utawahakikishia
wananchi kubaki na mali zao ikiwemo ardhi.
Mgombea huyo
wa urais wa aliyasema hayo jana Septemba 18, 2025, uwanja wa mpira wa Mpika tango Mkoani, wakati
akizungumza kwenye mkutano wa hadhara wa chama hicho, wa kampeni.
Alisema, utawala
huo wa sheria, utakuwa na mambo kadhaa, ikiwemo kila mmoja kupata heshima ya
kufanya shughuli zake, kwa mujibu wa sheria.
Alieleza kuwa,
kufanya hivyo ni kuifungua Zanzibar kiuchumi, kutokana na watu kuheshimiana na
kutunza amani na utulivu miongoni mwao.
‘’Kama
nikiingia mdarakani, nitahakikisha, kwanza tunakuwa na utawala wa kuheshimiana,
ambao ndani yake utamuhakikishia kila mmoja mali yake ikiwemo ardhi kutoporwa,’’alieleza.
Aidha Mgombea
huyo wa urais, alisema katika kufikia uchumi wa kweli, suala la ujenzi wa
bandari za kisasa katika miji ya Mkoani na Wete ni lazima.
Alisema, ili
kisiwa cha Pemba, kifunguke kiuchumi, ujenzi wa bandari ya kisasa itakuwa ndio
kipaumbele chake, ili mzungumko wa watu uwe mkubwa.
‘’Nafahamu
kuwa, ili maendeleo yapatikane, mzunguruko wa watu ni jambo lazima, na watakuja
kama miundombinu ya milango ya kiuchumi iko vizuri,’’alifafanua.
Katika hatua
nyingine, alisema njia nyingine ya kuifungua Pemba, ni kuanzisha mpango maalum ‘Cluster
program’ ambao utasaidia kuwa na maeneo ya ujenzi, wa nyumba za kisasa kwa
gharama nafuu.
‘’Ili
kukifungua kisiwa cha Pemba, suala la uwepo wa nyumba za kisasa tena za gharama
nafuu kila eneo, haliepukiki, na hili ni kwa ajili ya watakaokuja kibiashara,’’alifafanua.
Mgombea huyo
wa urasi wa Zanzibar kwa tiketi ya ACT-Wazalendo Othman Massoud Othman, alisema
njia nyingine ya kuifungua Zanzibar, ni kurahisisha mawasiliano ya kimtandao.
Alisema,
lazima katika kufikia hilo, kuwepo kwa eneo la kupata huduma ya intanet bure litazingatiwa,
ili mawasiliano yasiwe changamoto kuelekea kukua uchumi wa kati.
Alisema, kwa
sasa wananchi wanapoingiza bando la shilingi 1000, linachukuliwa kwa haraka,
jambo ambalo ni changamoto kwa wananchi.
Aidha, alisema katika kufikia hayo, ni vyema wananchama wa chama hicho, kuwapa kura wagombea wote wa ACT-Wazalendo, kuanzia madiwani, wawakilishi, wabunge na rais wa Zanzibar.
Kwa upande
wake Makamu Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo Zanzibar Ismail Jussa Ladu, amesema
kwenye amani na utulivu wao wanaweza kuwa wa mwanzo.
Alisema,
suala la kutunza amani, mamlaka zisiwe na wasi wasi, kwa wanachama wa chama hicho
wataunga mkono, na hawatokubali kuchokozeka.
‘’Wanachama
wa ACT-Wazalendo, suala ka kutunza amani ni jambo la kawaida kwetu, na na kuomba
haki itatendeka katika mchakato wa uchaguzi mkuu,’’alifafanua.
Nae Naibu
Katibu Mkuu wa chama hicho Omar Ali Shehe, alisema ili chama hicho kishinde,
suala la kujitokeza kupiga kura, ni lazima kwa kila mmoja.
Alieleza
kuwa, ACT-Wazalendo haina wasiwasi na ushindi, kutokana na mtaji wake mkubwa wa
kuwa na wanachama wingi, ambao wataingia kwenye uchaguzi mkuu mwaka huu.
‘’ACT-Wazalendo,
kulekea uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu, suala la ushindi kwetu halina shaka,
ninachowaomba mwende mkapige kura,’’alifafanua.
Wakati huo
huo Mwenyekiti wa chama mkoa wa Mkoani Mohamed Ali, amesema suala la kuendesha
uchaguzi kwa njia ya kistaarubu, iwe ni lazima kwa kila mmoja kutunza amani.
Mwisho
Comments
Post a Comment