NA MOZA SHAABAN, PEMBA@@@@
WAKULIMA wa zao la karafuu kisiwani Pemba
wamesema, kilimo cha zao hilo kwa sasa kimekabiliwa na changamoto kadhaa,
ikiwemo mabadiliko ya tabianchi, jambo linalosababisha kupungua kwa uzalishaji.
Waliyasema hayo wakati wakizungumza na mwandishi wa habari
hizi, kuhusu changamoto mbali mbali za uzalishaji wa zao hilo.
Walisema kwa sasa, wanakabiliwa na changamoto ya uzalishaji
mdogo wa zao hilo, unaotokana na
kutostawi vizuri kwa mikarafuu wanayoendelea kuotesha, hali
inayosababishwa na kuongezeka kwa jua na
joto kali.
Mmoja kati ya wakulima hao Said Mattar Mohamed alisema, kwa
mwaka wa saba sasa, uzalishaji wa zao hilo umepungua, kwani mikarafuu iliokwishastawi
vizuri na kutegemewa kuanza uzalishaji yamekua yakinyauka na kukauka.
" Sasa hivi sisi wakulima wa kilimo cha zao la karafuu,
tunaathiriwa sana na mabadiliko ya tabia ya nchi, kwani mikarafuu
iliokwishastawi vizuri na kutegemewa, kuanza uzalishaji yamekua yakinyauka na
kukauka, kutokana na jua kali,"alisema.
Akieleza namna uzalishaji wa zao hilo, unavyopungua alisema,
kuna baadhi ya mikarafuu mikubwa
waliokua wakivuna kiasi cha pishi 40 hadi 60 za karafuu mbichi, kabla ya
miaka saba iliopita, ambapo kwa sasa hawanavuni
zaidi ya pishi 20.
Kwa upande wake mkulima Shaaban Haji alisema, mbali na
uzalishaji mdogo wa zao hilo, kumekua na changamoto ya ustawi wake pamoja na
kuingiliana kwa misimu miwili, hali inayosababishwa na mvua nyingi zinazonyesha
bila ya mpangilio.
" Uzalishaji wa karafuu ni mdogo, kwa miaka hii ya
karibuni, lakini pia ustawi wake sio mzuri, kama ilivyokua zamani, kutokana na
kuathiriwa na mvua nyingi, mfano mzao huu tulionao karafuu nyingi zilianguka,’’
alisema.
Hivyo ameiomba serikali, kupitia wizara ya kilimo kuongeza
jitihada kwa kuwapatia wakulima wa zao hilo mafunzo ya kitaalamu, ili kuwapa
njia sahihi za kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi.
Kwa upande wake mkulima Habib Khatib Faki wa Kangani alisema
mbali na kututumia nguvu kubwa, kuekeza katika kilimo hicho ambacho ndio
tegemeo, bado uzalishaji wake umepungua kwa kiasi kikubwa.
Alieleza kua lengo la kuwekeza kwao, ni kuongeza uzalishaji
ili waweze kunufaika ipasavyo, kama lilivyo lengo la serikali la kuhakikisha
wakulima wananufaika na kilimo hicho.
Afisa Maendeleo ya Kilimo wilaya ya Mkoani, Said Ali Hassan
alikiri kuwa, mabadiliko ya tabia ya nchi, ni miongoni mwa changamoto
inayowakabili wakulima wa zao hilo.
Alifafanuwa kuwa, baada ya kujitokeza kwa changamoto hiyo,
wamekuwa wakichukua jitihada mbali mbali, ikiwemo kuwashauri wakulima kutoipalilia
mikarafuu yao mara kwa maram ili kuzuia athari za joto.
Waziri wa Biashara na Viwanda Omar Said Shaaban, alisema Shirika
la Biashara la Biashara la Taifa ‘ZSTC’ kwa mwaka 2023/2024 lilipanga kununua
tani 4,940 za karafuu kavu, ingawa hadi mwezi Machi mwaka 2023, lilinunua tani
3,917.28.
Waziri alisema, sababu kubwa ya kushuka kwa ununuzi wa zao
hilo kulitokana na mambo kadhaa, ikiwemo mabadiliko tabianchi, ambayo
yamepelekea karafuu nyingi kununuliwa katika robo ya kwanza.
Aidha ZSTC kwa mwaka huo, lilipanga kununua makonyo tani 988,
ingawa hivyo, hadi kufikia Machi 2023, halikufikia lengo na kununua tani 771.3,
kulikosababisha na kushuka kwa uzalishaji wa zao la karafuu. MWISHO
Comments
Post a Comment