NA ZUHURA JUMA, PEMBA@@@@
MGOMBEA Urais wa Zanzibar kupitia Chama cha ACT- Wazalendo, Othman Masoud Othman amesema, atahakikisha wananchi wa Pemba, wananufaika moja kwa moja na rasilimali ya zao la karafuu ambalo ni uti wa mgongo wa uchumi wa Zanzibar.
Akiwahutubia wananchi kwenye viwanja vya Mchangamdogo Kambini Jimbo la Kojani, Mkoa wa Kaskazini Pemba Othman alisema, pamoja na karafuu kuwa ni zao la kimkakati, na lenye thamani kubwa duniani, bado linahitaji kufufuliwa ili kuleta tija zaidi kwa wananchi wa Zanzibar.
Alisema kuwa, Zanzibar ina uwezo wa kuzalisha zaidi zao la karafuu, ili liendelee kuwa ni mwega wa uchumi wa nchi, hivyo atakapopewa ridhaa ya kuiongoza nchi, atalifufua zao hilo pamoja na mazao mIngine ya viungo kwa ajili ya kuiinua Zanzibar kiuchumi.
"Nitatafuta wawekezaji watakaokuja kununua karafuu hapa, hivyo zao hilo litaongezeka thamani na wananchi wataongeza vipato vyao," alisema mgombea huyo.
Aidha alieleza kuwa, wamejipanga kuwawezesha wavuvi ili waondokane na umasikini kwa kuwatafutia Teknologia za kisasa na vyombo vyao kutosha vya kuvulia, sambamba na kuwawezesha kuongeza thamani ya kile anachokivua.
Akizungumzia suala la uzalishaji wa chumvi, mgombea huyo alifafanua kuwa, Pemba imezungukwa na bahari ambayo inaweza kuzalisha chumvi inayohitajika duniani kote, hivyo atahakikisha kila mzalishaji ananufaika na fursa hiyo ili kujipatia kipato kitakachowasaidia kimaisha.
"Naahidi kuwekeza kwenye miundombinu ya kisasa ya uzalishaji wa chumvi, ili wananchi wa Pemba wapate kipato cha uhakika kupitia bidhaa hiyo," alisema.
Wakati huo huo aliwaomba wananchi kwenda kupiga kura ifikapo Oktoba 29 kwa ajili ya kumpatia ushindi huku akiwahimiza kutunza amani kwani ndio jambo la msingi wa maendeleo.
Awali, Meneja wa Kampeni wa ACT Wazalendo, Ismail Jussa Ladhu alisema, wanahitaji soko la karafuu huria litakalomfanya mwananchi na mkulima kuuza zao hilo anapotaka, kwani itasaidia kuwa na ushindani wa masoko, jambo ambalo litakuza kipato kwa wananchi.
"Zao la karafuu linalotoka kisiwani Pemba ni lenye thamani kubwa kuliko nchi nyengine yeyote, hivyo tutawaleta wawekezaji kuja hapa kununua bidhaa hiyo," alieleza.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Zanzibar kupitia Chama hicho, Omar Ali Shehe aliwataka wananchi waende kupiga kura kwa ajili ya kuchagua kiongozi wao, kwani uchaguzi ni fursa na ni haki ya kila raia kupiga kura.
Nae Mwenyekiti wa Mkoa wa Wete kichama Juma Khamis Ali aliwahamasisha akinamama kuwashawishi waume zao waliokwenda dago, kurudi kisiwani Pemba ili itakapofika Oktoba 29 wakapige kura.
MWISHO.



Comments
Post a Comment