NA ZUHURA JUMA, PEMBA @@@@
MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar Hemed Suleiman Abdulla amesema, kufunguliwa kwa Tawi la Taasisis ya Sayansi na Teknolojia ya Karume Pemba kutasogeza kwa karibu huduma za masomo ya sayansi na teknolojia kwa wananchi na kutoa fursa kwa vijana kujiendeleza kielimu wakiwa kisiwani Pemba badala ya kufuata masomo nje ya kisiwa hicho.
Ameyasema hayo leo Septemba 16, 2025 wakati akifungua Tawi la chuo cha Sayansi na Teknolojia ya Karume Pemba katika viwanja vya Mnazimmoja Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba.
Amesema, Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Karume inatoa
mchango mkubwa katika kukuza taaluma ya Sayansi na Teknolojia ndani na nje ya
nchi sambamba na kupata mafanikio mengi ikiwemo kuongezeka kwa wataalamu wa
fani ya Sayansi na Teknolojia nchini na Barani Afrika kwa ujumla.
Alieleza kuwa, uwepo wa Tawi hilo kutafungua milango ya
kuitangaza Pemba kielimu katika nyanja za sayansi na Teknolojia na kuwavutia watu
wengi sambamba na kutoa fursa za kiuchumi kwa wananchi kutokana na wanafunzi
watakaosoma chuo hicho watahitaji mambo mbali mbali ambayo yatachangia kuleta
maendeleo ya kibiashara yatakayowaongezea kuongezeka kipato.
Makamu huyo alifahamisha kuwa, katika kuipa kipaombele sekta
ya elimu Serikali kupitia Wizara ya elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, imekuwa
ikiboresha sekta ya elimu ikiwemo kuimarisha miundombinu, ubora wa elimu na
maslahi ya walimu ambayo yamechangia kupata mafanikio mazuri ya ufaulu kwa
wanafunzi wazanzibar.
Aidha, alisema Serikali imeongeza bajeti ya Bodi ya Mikopo
ya wanafunzi wa elimu ya juu Zanzibar hadi kufikia shilingi bilioni 37.5 kwa
mwaka wa fedha 2025/2026 ambayo itawanufaisha zaidi ya wanafunzi elf 14 wakiwo
wanafunzi wapya na wanaendelea kupatiwa mikopo na wanafunzi wa ngazi ya diploma
pia watanufaika na mikopo hio.
"Sambamba na hayo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
itaendeleo kuimarisha sekta ya elimu kwa kuiongeza bajeti ya Wizara ya elimu
hadi kufikia shilingi bilioni 864 kwa mwkaa wa fedha 2025/2026 kwa lengo la
kuendeleza mapinduzi ya kielimu nchini, ili kuendana na mabadiliko ya kielimu
na soko la ajira duniani," alieleza.
Waziri wa elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Lela Mohamed Mussa
amewatoa hofu wakufunzi pamoja na wanafunzi wa Taasisi ya Sayansi na
Teknolojia Pemba kuwa Tawi kubwa na la kisasa litajengwa kisiwani humo, ili
kutoa fursa kwa wananfunzi kujisomea vizuri na kwa ufanisi wa hali ya juu.
Waziri Lela alisema, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali
Zanzibar itahakikisha chuo cha KIST kinaendela kutoa taaluma yenye ubora na
viwango vinavyokubalika vitakavyowawezesha wahitumu wa chuo hicho kuweza
kufanya kazi mahala popote duniani.
Aidha Waziri Lela amewataka wazazi na wananchi kwa ujumla
kuitumia fursa ya uwepo wa tawi la KIST kisiwani Pemba kwa kuwasajili vijana
wao kujiunga na chuo hicho na kuamini kuwa elimu inayotolewa hapo ni sawa sawa
na elimu inayotolewa katika vyuo vinavyotoa taaluma kama hio nje ya kisiwa cha Pemba.
Kwa upande wake Mkuu wa Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya
Karume (KIST) Dk. Mahmoud Abdulwahab Alawi alisema KIST imejikita katika kutoa
mafunzo mbali mbali yanayohusu sayansi na teknolojia yakiwemo pia mafunzo ta
muda mfupi, ili vijana waweze kujifunza na kufanya kazi zao kwa kujiamini
kitaaluma.
Dk. Mahmoud alieleza kuwa, katika kuunga mkono juhudi za
Serikali za kuifungua Pemba kiuchumi na kielimu KIST imeamua kufungua Tawi lake
kisiwani hapa, ili kuhakikisha wanatoa fani mbali mbali za sayansi na
Teknolojia ambapo kwa sasa wanafunzi 90 wameshajiunga na chuo hicho.
Alisema, Tawi la KIST Pemba limenza kutoa mafunzo ya cheti
ambapo uongozi wa Taasisi hiyo upo katika mchakato wa kuanzisha mafunzo ya
ngazi ya Diploma, ili kuwawezesha wanafunzi wanaoishi kisiwani Pemba kujiunga,
ili kuwapunguzia gharama za masomo.
Nae Mwenyekiti wa bodi ya Taasisi ya Sayansi na Teknolojia
ya Karume (KIST) Dk. Afwa Khalfan Mohamed alifafanua kuwa, kuanzishwa kwa Tawi
la KIST Pemba kumeondoa kilio cha muda mrefu cha wananchi wa Pemba ambao
walihitaji kufunguliwa kwa Tawi la chuo hicho, ili kuwapunguzia gharama
za ada ya masomo pamoja fedha za kujikimu wanapokuwa vyuoni.
Alisema, kwa sasa Taasisi hiyo inafanya kazi zake katika
jengo la kukodi ambalo halitoshelezi kutoa mafunzo ya ngazi ya cheti hadi
diploma kama ilivyo malengo ya chuo hicho, hivyo ameiomba Serikali kusaidiwa
upatikanaji kwa jengo la kudumu ambapo tayari eneo la kutosha kwa ajili ya
ujenzi limeshapatikana.
MWISHO.





Comments
Post a Comment