NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@
MGOMBEA Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi ‘CCM’ Dk. Samia Suluhu Hassan, amesema kama
atapata ridhaa ya kutetea nafasi hiyo, ataijenga bandari ya Wete ili, iwe ya kisasa.
Mgombea huyo wa Urais, aliyasema hayo jana, uwanja wa
Gomabani ya kale, wilaya ya Chake chake Pemba, kwenye mkutano wa hadhara wa kampeni,
kuelekea uchaguzi mkuu mwezi Oktoba, mwaka huu.
Alisema, ili kuifungua Pemba hakuna budi suala la
miundombinu ya bandari, ni lazim kupanuliwa, ili kurahisisha usafirishaji wa wananchi
na mizigo yao.
Alisema, tayari fedha zake zipo, ambazo ni mkopo kutoka Korea,
na anachosubiri ni kupata tena ridhaa ya wananchi ifikapo Oktoba 29, mwaka huu,
aanze kazi.
‘’Niwahakikishie kuwa, mini na Dk. Mwinyi kama mtatupa
ridhaa, basi moja ya eneo ambalo kwa Pemba, tutaliangalia, ni ujenzi wa bandari
ya kisasa ya Wete,’’alisema.
Ahadi nyingine, ambayo Mgombea huyo wa Urais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan, amesema atakeleza ni ujenzi wa
barabara ya Chake chake – Mkoani, pamoja na kuzimaliza zile nyingie saba,
ambazo ujenzi wake unaendelea kisiwani humo.
‘’Hatuwezi kuzungumzia maendeleo ya Pemba, bila ya
kuangalia miundombinu ya usafiri wa nchi kavu, na ndio manaa tunakusudia kuziharakisha,
kumalizia barabara hizo,’’alifafanua.
Katika hatua nyingine, Dk. Samia, alisema kama akipata
ridhaa, anakusudia kuondoa matumizi ya mkaa, kuni, matumizi ya mafuta ya
petroli, diseli na mafuta ya taa katika harakati za maisha ya kila siku.
Alifafanua kuwa, anakusudia hadi ikifika mwaka 2034,
asilimia 80 ya watanzania, wawe wanatumia nishati safi, iwe kwa kupikia, kuonea
na kwenye shughuli nyingine za kimaendeleo.
‘’Tunakusudia nisahti hizo, ziwe chanzo chake ni jua,
upepo mabwawa ya maji kama la Mwalimu Nyerere, ambalo, litaunganishwa na gridi
ya taifa, ili kuzalisha nishati safi,’’aliahidi.
Katika hatua hatua nyingine, Mgombea huyo wa urais,
aliwahakikisha wananchi kuwa, vikosi vya ulinzi na usalama vitalinda amani na
utulivu, kuelekea uchaguzi mkuu mkuu mwaka huu.
‘’Kila mmoja awe mlinzi wa mwenzake, juu ya kulinda amani, na baada ya kupiga kura rudini nyumbani, msubiri taratibu nyingine zifanyike,’’alifafanua.
Aidha Dk. Samia alisema, CCM imekuwa ikitekeleza miradi
zaidi kwa wananchi na sio, maneno kama baadhi ya vyama vinavyodai.
‘’CCM sio chama cha blaablaa, ni vitendo kwani
inawatumikia wananchi wote bila ya ubaguzi wa aina yoyote,’’alifafanua.
Alisema, kwa sasa Pemba, inazo skuli za ghorofa pamoja na
nyumba za waalimu, ikiwemo eneo la kisiwa cha Kojani wilaya ya Wete.
‘’Leo hadi kisiwa cha Kojani na maendeo mingine kama
Konde, Kiwani, Michakaini zipo skuli ambazo ni za kisasa, na ni haya ni ushirkiano
kati yangu na Dk. Mwinyi haoa Zanzibar,’’alisema.
Kuhusu yaliotekelezwa kwa miaka mkitano iliyopita na serikali
zote mbili, alisema zimefanikiwa, kuweka mazingira ya uwekezaji, na kuwepo kwa
viwanda kama vya maji, majani ya mkarafuu na kunuwafaisha wananchi.
Alieleza kuwa, kwa baada ya mazungumzo ya kideplomasia,
sasa makontena ya bidhaa yanashushwa moja kwa moja katika bandari ya Mkoani
Pemba, na kusababisha ahuweni ya bei ya bidhaa.
‘’Sasa meli kubwa hazishushi tena Unguja kwa bidhaa
ambazo zinakuja Pemba, bali ni moja kwa moja, na hii ni mwanzo, lakini kwa
miaka mitano ijayo, tutaimarisha zaidi,’’alifafanua.
Awali Katibu Mkuu wa chama hicho Dk. Asha Rose Migiro,
alisema CCM ikiendelea kukaa madarakani, mafanikio makubwa yataendelea kupatikana.
Alisema, hayo yanaweza kufikiwa, ikiwa watanzania watampa
kura Dk. Samia Saluhu Hassan na kwa upande wa Zanzibar Dk. Hussein Ali Mwinyi.
‘’Sio hayo tu, tunao wabunge, wawakilishi na madiwani
wote kutoka CCM, ni vyema nao wakapewa kura ili kuwa safu imara ya kuliendelea
taifa mbele,’’alifafanua.
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM taifa,
Hemed Suleiman Abdulla, alisema Ilani ya CCM ya mwaka 2020/2025, imetekelezwa
zaidi ya ilivyopangwa, kwa Tanzania nzima.
Alisema, ipo miradi kama ya barabara, maji safi na salama,
afya, elimu, uwezeshaji kiuchumi, jambo ambalo limenawirisha maisha ya wananchi.
Kuhusu Mgombea wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan, alisema amefanikiwa kusimamia umoja, mshikamano
na kurahisisha maendeleo kwa wote.
Alieleza kuwa, Dk. Samia asiwe na cha kupoteza kwa
wananchi wa Pemba, kama sehemu ya kumtunza, ili aiongoze tena Tanzania kwa
miaka mitano ijayo.
‘’Miradi kadhaa iliyopo Pemba, Dk. Samia amehusika kwa
njia moja ama nyingine, hivyo hakuna haja ya kumpa kura mgombea mwingine,’’alisema.
Alifafanua kua, ujio wa miradi hiyo ni kuimarisha ustawi
wa wananchi kwa makundi, ama mmoja moja, ili kuhakikisha kila mmoja anaishi kwa
furaha.
Hata hivyo, Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya halmashauri kuu
ya CCM taifa, aliwataka wananchi kutokochokozeka na kuendelea, kuilinda amani
iliyopo.
‘’Niwasihi wananchi wenzangu, jambo moja na la muhimu kwetu,
ni kuilinda amani na utulivu, ili kila kitu kifanyike kwa nafasi pana,’’alifafanua.
Mapema Waziri ya
Uchukuzi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambea ni Mgombea Ubunge wa Jimbo la
Mkoani Prf: Makame Mbarawa Mnyaa, alisema, ujenzi wa uwanja ndege wa
Pemba, ambao unatarajiwa kuanza wakati wowote, mwaka huu.
Alisema, utakuwa na urefu wa kilomita
2.5 ambao utajumuisha pia jengo kubwa la abiria, litakalo kuwa na uwezo wa
kuhudumia abiria 300,000 (laki tatu) kwa mwaka.
Akizungumzia ujenzi wa barabara ya
Chake chake- Mkoani, alisema ndani ya mwezi huu, Rais wa Zanzibar Dk. Hussein
Ali Mwinyi, atazindua ujenzi wa barabara hiyo, kwa kumkabidhi mkandarasi kazi
‘’Barabara hii yenye urefu wa kilomita,43.5
itakuwa na njia nne, mbili za kwendea na mbili za kurudia, ambayo, itaunganishwa
na ile ya Chanjaani- Uwanja wa ndege, itakayokuwa na taa maalum na za kisasa,’’alifafanua.
Aidha aliwaomba wananchi, kumpa kura
za ndio Dk. Samia ili awe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, pamoja na
Dk. Hussein Ali Mwinyi awe kwa upande wa Zanzibar.
Nae Mbunge mteule wa CCM kwa Mkoa wa kaskazini Pemba, Asya
Sharif Omar, amesema kwa sasa hadi mama mtilie, wanaendelea kufaidika na
matunda ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kuwezeshwa kuichumi.
Kwa upande wake Maryam Azan Mwinyi kwa nafasi kama hiyo
kwa mkoa wa kusini Pemba, alimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
kwa kuwapeleka TASAF, na kuwanufaisha wanawake na watu wenye uleamvu, na sasa
wapo wanaojitegemea kupitia mpango huo.
Alisema, kwa sasa wapo wanawake, ambao wamekua na kipato
cha hali ya juu, kutokana na kuingizwa kwenye mpango wa kunusura kaya maskini,
na wakiendelea kujitegemea kibiashara.
Mgombea Ubunge wa Jimbo la Kojani Pemba, Hamad Chande,
alisema yapo mingi aliyofanya Dk. Samia, ikiwemo ahadi ya ujenzi ya uwanja wa
ndege wa Pemba na barabara Chake chake Mkoani, na zaidi ya shilingi bilioni 886
zikitarajiwa kutumika.
Alisema, fedha nyingine ni shilingi bilioni 327, ambazo
zinaendelea kutumika, kwa ujenzi wa bandari ya Shumba Micheweni, na kuifanya fedha
yote ilioyoingia Pemba, kwa miradi hiyo, kuwa ni shilingi trilioni 1.26.
‘’Kwa haya ambayo Dk. Samia ameyafanya, nna hakika
wananchi watamchangua ifikapo Oktoba 29, mwaka huu, nakurejea ili kuendeleza mema
kwa watanzania,’’alisema.
Nae Mgombea Uwakilishi Jimbo la Konde Zawadi Amour
Nassor, alisema kwenye sekta ya afya, sasa huduma zinatapatikana saa 24,
ikiwemo chakula cha uhakika kwa wagonjwa.
‘’Huduma za afya zimeimarika, na moja wapo ni kuwepo kipimo
cha kisayansi cha magonjwa ya ndani ya mwili na mishipa midogo ‘MRI’ ambapo hapo
kabla, hakikuwepo,’’alisema.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa kusini Pemba, Yussufu Ali Juma,
alisema hana wasiwasi wa Dk. Samia kurejea tena madarakani, kutokana na
kutekeleza miradi ya kibinaadamu mkoani humo.
‘’Tumejengewa hospitali ya Mkoa ya kisasa yenye huduma muhimu,
pamoja na ujenzi wa matenki mtatu ya kuhifadhia maji safi na salama, na kila
moja likiwa na ujazo wa lita milioni 1,’’alifafanua.
Mjumbe wa kamati kuu ya CCM taifa, Mohamed Aboud Mohamed,
alisema sasa watanzania wana heshima kubwa kimataifa, kutokana na maono na
juhudi za Dk. Samia kwa kuwaunganisha na mataifa mingine.
‘’Kwa mfano filamu ya kiutalii ‘royal tour’
sasa imeifungua Zanzibar kiutalii, na kila mmoja anaendelea kunufaika na matunda
ya utalii, hivyo ikifika Oktoba 29, mwaka huu kura ni kwako,’’alifafanua.
Mwisho

Comments
Post a Comment