NA SAIDA ALI, PEMBA@@@@
Mkuu wa mkoa wa kaskazini Pemba Salama Mbarouk Khatib, amesema serikali
itaendelea kulijali kundi la watu wenye
ulemavu, ili kuhakikisha wanapatiwa haki zao msingi, ikiwemo za uongozi na
uchumi.
Hayo aliyasema leo Septemba 16, 2025 kwenye hutuba yake, iliyosomwa kwa niaba yake na Katib tawala wilaya
ya Micheweni Sheha Mpemba Faki, alipokuwa akifungua kongamano la wadau wa
maendeleo jumuishi katika jamii, lililofanyika skuli ya Utaani Pemba.
Mkuu huyo mkoa alisema,
serikali imewapa haki na fursa na kuwathamini pamoja na kuwaunga mkono, watu
wenye ulemavu kama walivyo watu wingine.
Alieleza kuwa, watu
wenye ulemavu wamepewa fursa kubwa ya kushiriki katika kupiga kura na kuchagua
viongozi, wawatakao, kama msingi wa sheria mama katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984,
ilivyoekeleza kifungu cha 7 na ch 12.
"Niwatoe hofu nyinyi watu wenye ulemavu, mnayo fursa kubwa ya kushiriki kikamilifu katika harakati mbali mbali zikiwemo za kisiasa na uongozi,’’alifafanua.
Akizungumzia suala
la amani, kuelekea uchaguzi mkuu, Mkuu huyo wa mkoa wa kaskazini Pemba Salama
Mbarouk Khatib, alieleza kuwa serikali imejipanga kikamilifu, kusimamia amani
na utulivu wa nchi, na kuondosha changamoto zote hatarishi dhidi yao.
Hata hivyo, alilipongeza
shirikisho la jumjuiza za watu wenye ulemavu Zanzibar ‘SHIJUWAZA’ kwa kuzaa fikra
ya kulileta kongamano hilo, wakati taifa likielekea uchaguzi mkuu wa vyama
vingi.
Mapama Mkurugenzi
Mtendaji kutoka shirikisho la jumuiya za watu wenye ulemavu, Ali Machano alisema kuwa, juhudi kubwa
zinachukuliwa na shirikisho hilo, ili kuhakikisha haki na fursa za watu wenye
ulemavu, zinapatikna.
Alisema kuwa, wamekuwa mstari wa mbele kutetea na kupaza sauti zao, kupitia makongamano na mikusanyiko mbali mbali, ili kuhakikisha watunga sera na waandaji mipango, ujumbe unawafikia.
"Tumekuwa
tukitetea haki na fursa za watu wenye ulemavu, kupitia makongamano, vyombo vya
habari na hata mitandao ya kijamii, ili kuhakikisha changamoto hazijitokezi,
katika maisha yao,"alifafanua.
Meneja Program kutoka shirikisho la jumuiya za watu wenye ulemavu, Sophia
Azidihery Leghela alisema, lengo la kongamano hilo ni kujadili, namna bora ya
watu wenye ulemavu wanashiriki kikamilifu katika maisha muhimu ya kiuchumi,
kijamii na kimaendeleo.
Alisema kuwa jukwaa hilo la maendeleo jumuishi, linalenga kuwaweka pamoja viongozi
wa serikali, asasi za kiraia, watu wenye ulemavu, mabaraza na jumuiya za
watu wenye ulemavu.
"Jukwaa hili litasaidia kuibua changamoto zinazowakumba watu wenye ulemavu,
na vipi tutaziimarisha haki na fursa zitakazowafikia, kusudi waishi maisha
mazuri kama wingine,’’alifafanua.
Mratibu wa Baraza la taifa la watu wenye ulemavu Ofisi Pemba, Mashavu Juma Mabrouk
alisema, serikali imekuwa ikiwajali mno, watu wenye ulemavu kwa kuwawekea
chombo kinachosimamia haki na fursa zao.
"Mimi mjumbe la baraza la watu wenye ulemavu, kwanza niipongeze serikali, kwa kutuwekea chombo chetu kinachosimamia haki na fursa zetu, maana awali tulikuwa hatuna jukwaa la kupazia sauti zetu kwa pamoja,’’alifafanua.
Awali Afisa ufuatiliaji na tathmini Ofisi ya Mrajis wa NGO's Pemba Aziza Yussuf
Saleh, alisema watu wenye ulemavu wanauhitaji mkubwa wa kupatiwa elimu, na haki
zote za harakati za kisiasa.
Akilifunga kongamano hilo, Mwakilishi wa Afisa Mdhamini Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Pemba, Shaaban Mohamed Abdalla, alisema baraza, shirikisho na jumuiya za watu wenye ulemavu, zimekuwa na mchango mkubwa wa kusaidia, kutambulika kwa haki mbali mbali za watu wenye ulemavu.
Kauli mbiu la kongamano hilo ni "haki za watu wenye ulemavu ni haki za bnaadamu"
hakikisha ushiriki wa watu wenye ulemavu kwenye siasa na uongozi.
MWISHO.
Comments
Post a Comment