NA FATMA HAMAD, PEMBA
MKURUGENZI wa Jumuiya ya Wanasheria wanawake Zanzibar ZAFELA, Jamila Mahamoud Juma, amezitaka asasi za
kiraia, kushirikiana kwa pamoja na kuwajengea uwezo watoto wa kike, waliyokatisha
masomo, ili waweze kurudi na kupata haki yao ya msingi.
Mkurugenzi
huyo, aliyasema hayo katika mkutano wa kuutambulisha mradi wa Malala,
utakaoendeshwa na ZAFELA, Zanzibar kwa muda wa mwaka mmoja, kikao
kilichowajumuisha asasi mbali mbali za kirai kisiwani Pemba.
Alisema
katika utafiti wao walioufanya, waligundu kuwa, kuna wimbi kubwa la watoto wa
kike wamekuwa wakikatisha masomo yao, kutokana na sababu mbali mbali, ikiwemo
kuolewa, kupata mimba za utotoni pamoja na kufanyishwa kazi za nyumbani.
Alisema,
wamekuwa wakipokea kesi nyingi za watoto wa kike, kudai haki zao, aidha
waliolewa au waliojihusisha na mahusiano, ambao ukiwangalia umri wao
unapaswa wawe wako masomoni.
‘’Tumeamua
kuleta mradi huu wa ‘Malala’ kwa ajili
ya kumuezesha na kumsaidia mtoto wa kike, ili aweze kurudi masomoni, na
kumaliza masomo yake, angalau elimu ya lazima,’’alisema Mkurugenzi huyo.
Alifahamisha
kuwa, mrahidi huo umelenga kuwafikia watoto 3,000 kwa Unguja na Pemba, hivyo
amezitaka asasi za kiraia, kuzidisha ushirikiano wao na ZAFELA, ili kufikia
lengo la mradi huo.
Aidha
kwa upande mwengine Mkurugenzi huyo wa ZAFELA, aliwataka wanajamii kukaa karibu
na watoto wao, na kuwasikiliza matatizo yao, ili wawe na uthubutu wa kueleza
changamoto zinazowatokezea katika harakati zao za kimasomo.
‘’Inawezekana
mtoto anaacha masomo kutokana na vikwazo tu vinavyo mkwaza aidha njiani au skuli,
hivyo tujenge urafiki nao, ili tuwanusuru na kadhia kama hizo,’’ alifafanua.
Mapema
Msimamizi wa mradi huo Hairun Abass Rajab kutoka ZAFELA, alieleza kuwa hadi
sasa, bado zipo familia ambazo hazimpi fursa mtoto wa kike, kupata haki yake ya
elimu kuanzia ya msingi hadi vyuo vikuu.
Alifahamisha kuwa, lengo la mradi huo ni kuwasaidia
watoto walioacha masomo, na walio katika mazingira magumu, ili kuhakikisha
wanapata elimu na kufikia ndoto zao.
Akichangia
katika mkutano huo, mwanaharakati wa kulinda na kutetea haki za wanawake na watoto kutoka wilaya ya
Mkoani, Saada Mohamed Othman, alisema ni
vyema kuweko na mkakati madhubuti ya kuwaekea usimamizi wa hali ya juu wanafunzi hao.
‘’Kuna
watoto waliokaa nje kwa muda mrefu, na tayari walishaathirika na ulevi,
ulawiti, ubakaji, hivyo ni vyema tuwe makini nao, wakati tunapowarejesha masomoni,’’alifahamisha.
Nao
washiriki Ali Mohamed Ali na Salim Said, walisema ili kumaliza vitendo viovu
katika jamii, ni lazima kila mmoja kwa nafasi yake, kuchukua jitihada za
makusudi, jambo ambalo litasaidia kupata kizazi chenye madili mema.
Mwisho
Comments
Post a Comment