NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@
HEDHI ni damu
maalum, anayotoka mwanamke pekee, mwenye umri maalum na kwa siku maalum.
Tena mwenye
umri wa kubeba ujauzito, ambapo mabadiliko hayo, hata uwe fukara, fakiri,
maskini na tajiri hujitokeza.
Naam….damu hii
haitoki eneo jingine la mwanamke, bali ni kwenye sehemu yake ya uke tu, tena ni yenye rangi, harufu na uzito kama damu ya kawaida.
Tulishazoea
kila atokae damu, huwa ni kwa ugonjwa, ajali, kuumia, ingawa kwa ii, ndio
uzima na umadhubuti wa mwanamke kiafya.
KWA NINI DAMU HII ITOKEA?
Kwamba, kiyai kilichokomaa na kutoka nje ya kifuko kisipopata mbegu
ya mwanamme ‘sperm’ baada ya siku moja, kinaharibika haraka haraka.
Hapo ngozi nyembamba ya tumbo au mji wa uzazi, iliyotanuka
kwa damu, ili kupokea na kulisha mimba, inachanika chanika na kutoa damu.
Kumbe mbegu ikikifikia kijiyai, mimba inapatikana na
kujishikiza kwenye kuta ‘wall’ za tumbo la uzazi, ili
iendelee kukua.
Ingawa, kama mimba ikishika rasmi, hapo huwa vigumu mno
damu kutoka, na ujauzito hujitokeza.
Mizunguko mingi ya hedhi, huwa na siku kadhaa za mwanzo,
ambapo mimba haiwezi kupatikana muda wa kutoshika, kabla ya kudondosha kijiyai.
Siku ya kwanza ya kuvuja damu, inahesabiwa kuwa siku ya
kwanza ya mzunguko wa hedhi.
Mbinu mbalimbali za kufahamu uwezo wa kushika mimba,
huhesabu kwa njia tofauti kidogo kipindi ambapo kuna uwezekano wa kupata mimba,
yaani hutumia ishara za msingi, za uwezekano huo.
JE UNAYAJUA MAUDHI YA HEIDH?
Yapo aina mbali mbali, kwa kila mwanamke, ingawa lazima yatafautiane kati
ya mmoja na mwengine.
Kwa mfano, yapo maumivu ya heidhi aina ya kwanza ambayo ni ya kawaida ‘Primary Dysmenorrhea’ haya kwa wanawake, wanapopitia kipindi
hiki, ambacho hujirudia kila mwezi.
Ambapo kwa
kawaida, huanza kati ya siku moja ama mbili, tena kabla ya hedhi kuanza
kutoka, mwanamke hujiskia mamumivu haya kwenye tumbo la chini, nyonga, na kiuno.
Maumivu
haya yanaweza kuwa madogo au makali, na huishia ndani ya saa 12 mpaka 72 huku
yanaweza kuambatana na kujitokeza kizunguzungu.
Yapili
ni yale maumivu yasio ya kawaida ‘Secondary Dysmenorrhea’ ambapo haya, hutokana na tatizo la kiafya, kwenye
via vya uzazi, kama vile uvimbe ambao sio wa saratani ndani ya mfuko wa mimba ‘uterine
fibroids’.
Maumivu haya, yanaweza pia
kusababishwa kwa athari za bakteria na virusi katika via vya uzazi,
ambapo kwa kawaida, maumivu haya huanza mapema zaidi wakati wa hedhi.
JE HEIDH INA MUDA MAALUM?
Mtaalamu wa afya ya uzazi kutoka hospitali ya Chake
chake Pemba, Rahila Salim Omar, anasema kwa kwaida, hedhi haina muda maalum.
Miongoni mwa wanawake kuna anayeingia hedhini, kwa
muda wa siku tatu, nne, ingawa muda wake sana huwa ni kati ya siku sita au saba.
Aligusia kuwa, suala la lishe bora, mazoezi, kupata
muda wa mapunziko, kupunguza mawazo na uchangamshi, ni vichecheo vya kupata
mzungumko bora na imara wa hedhi.
HEDHI SALAMA KWA WANAFUNZI NI
IPI?
Hedhi kwa wanafunzi, ni jambo
lisilozungumzwa hadharani, katika jamii nyingi Tanzania, kutokana na imani za
kidini na kitamaduni.
Aisha Haji Omar miaka (71) wa Machomane
anasema, achia mbali kwa wanafunzi, hata kwa wanawake wengine, inaonekana kama
vile ni aibu.
‘’Usiri huu ndio unaochangia, wanawake
wengine kupata madhara kwenye via vya uzazi, kwani inaonekana kama vile ni
matusi, kuzungumza hedhi salama hadhari,’’anasema.
Mayasa Haji Vuai (45) wa Mwambe,
anasema kwa umri wake, alipata elimu mara moja tu alipohudhuria kliniki, juu ya
hedhi salama.
Mtaalamu wa afya ya uzazi hospitali ya
Chake chake Dk. Rahila Salim Omar, anasema usiri uliopo wa kuizungumzia hedhi
salama, huzaa matatizo kadhaa, ikiwemo hata kuharibika kwa njia za uzazi.
‘’Via vya uzazi vinahitajika kuhifadhiwa
kwa vitambaa ama vifungashio vilivyo salama na hata sehemu ya kuanikia, ambapo
haya hayatojulikana, ikiwa kuna usiri wa elimu ya hedhi salama,’’anasema.
Mwanafunzi wa skuli ya Madungu Aisha
Hassans, anasema hedhi salama bado ni changamoto kwake, kuanzia matumizi ya
vitambaa na namna ya kujihifadhi.
‘’Mimi na wenzangu hadi leo ikitokezea
hedhi, huwa vigumu kuhudhuria masomoni, na furaha yetu ni kubakia
nyumbani,’’anaeleza.
Radhia Issa Maliki wa skuli ya Kiuyu,
anasema usiri ulioanzia ngazi familia na skuli, unawafanya wakose furaha,
kipindi cha hedhi.
Maua Mkubwa Haji na mwenzake Hanifa
Juma Hamad wa skuli ya Mwambe wanasema, hedhi salama wanavyojua wao, ni
kutokuumwa na tumbo pekee.
‘’Wakati mwengine hata vitambaa sisi
tunaazimana, kama ikitokezea mwenztu amepata hedhi, tuko safarini, na hadi leo
sijapata maumivu,’’anasema Maua.
Akizungumzia kuhusu hedhi salama, Balozi wa Flowless Sanitary Pads, Dk. Romana Malik anasema, kama mwanamke anaandaliwa kubeba mimba hapo baadae, jamii izingatie misingi ya hedhi salama.
“Hedhi salama hufanyika pale ambapo
binti au mwanamke yuko katika mazingira rafiki ya kupata taulo salama, zenye
ubora kwa afya yake hasa kwenye via vya uzazi.
Akasema jambo la kuzingatia pamoja na
taula ama vitambaa maalum, lakini maji safi na salama pamoja na sabuni, viwepo
kwa ajali ya kukoshea vitambaa anavyotaka kuvirudia.
Pamoja na Umoja wa Mataifa ‘UN’ na
Jumuiya za Kimataifa ikiwemo taasisi isiyo ya kiserikali WASH United ya
Ujerumani, ziliamua kuitangaaza Mei 28 ya kila mwaka, iwe siku ya hedhi salama,
bado changamoto kwa wanafunzi ipo.
DHANA POTOFU KWA WENYE HEDHI
Kampeni hizi zinaibua hisia tofauti,
miongoni mwa jamii, wapo ambao wanachukizwa wakiamini kuwa si jambo sahihi
kuzungumzia suala la hedhi salama.
Wapo wanawake na wasichana, hukanywa
na jamii zao juu ya kutofuata mambo kadhaa kwa sababu ya kuwa na hedhi, ikiwemo
kutohudhiria misiba na harusi hasa
nyakati za usiku.
WIZARA INAFANYA NINI KWA WANAFUNZI?
Afisa Mdhamini Wizara ya Elimu na
Mafunzo ya Amali Pemba Mohamed Nassor Salim, anasema, wizara inachukuwa
juhudi ya kupambana na hedhi salama kwa wanafunzi, kwakuwapa elimu ya stadi za
maisha .
Anaeleza kuwa stadi za maisha hizo ni
pamoja na kujitambuwa na udhalilishaji, kuwa salama na hedhi na kuimarisha
miundombinu hususani yvoo.
Wizara pia imewawezesha waalimu wa
kutosha wa ushauri nasaha wa madarasa ya msingi na sekondari, na kwamba kila
skuli, lazima wawepo waalimu wa aina hiyo.
Anasema wamekuwa wakishirikiana na hata wadau wa maendeleo, ili kupata taula za
kike, kama ambavyo mwaka jana, walikabidhiwa pedi 3,000 na kuzigawa kwa wanafunzi 314.
Wamekuwa wakipata wahisani mbali mbali wanaotoa elimu ya kujihifadhi kwa
wanafunzi hao kama vile Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania ‘TAMWA’,
UNICEF na Serikali kuu.
Taasisi kama ni KFHI kupitia ‘mradi wa kuwajengea uwezo waalimu katika mazingira
rafiki ya moto wa kike’ unaofadhiliwa na Korea ambao kwa Zanzibar umeshatoa
mafunzo kwa skuli tano, ikiwemo ya sekondari Shumba Vyamboni na Chwaka Tumbe.
Ambapo Mkurugenzi wa mradi huo Esther Mwakarobo, anaeleza Lengo la mradi
huo, ni kutaka kutengeneza mazingira rafiki kwa wanafunzi hasa wa kike, kwenye
hedhi salama.
Anaona usafi usipozingatiwa katika
kipindi cha hedhi kunaweza kusababisha maambukizi, katika mfumo wa uzazi na
kwenye njia ya mkojo.
Mwalimu Mkuu wa Skuli ya Sekondari Shumba Vyamboni Khatib Rashid Mwinyi,
anasema anona utoro wa wanafunzi na kuumwa, hasa kipindi cha hedhi,
ikisababishwa na kutokuwa na elimu ya hedhi salama.
TAMWA INAFANYA NINI?
Afisa Mradi wa afya ya uzazi Zaina
Abdalla Mzee, anasema wameibua mradi wa mwaka mmoja, kwa ajili ya kuwajengea
uwezo waandishi wa habari.
Kwani utafiti waliofanya kabla ya
kutekeleza mradi huo wa majaribio, waligundua kuwa uelimishaji juu ya afya
uzazi, kupitia vyombo vya habari uko chini.
‘’Tumeshakutana na waandishi wa
habari wa Unguja na Pemba, kuwajengea uwezo kupitia wataalamu wa afya ya uzazi,
sasa tunategemea mno kuona inaeleweka maana ya afya uzazi,’’anasema.
Kwake anaona mafanikio makubwa iwe,
kwanza wanawake na wasichana wa mjini na vijijini wanauwelewa haki ya afya ya
uzazi.
Jingine ni kwa vyombo vya habari,
kukuza na kuenedeleza uwelewa kwa jamii, ili sasa suala la afya ya uzazi
lisionekane kama vile ni kwa kundi maalum.
MIKATABA
YA KIMATAIFA
Mwaka 2001, nchi za Afrika zilikutana
Abuja na kutangaaza ili ziweke angalau asilimia 15 ya bajeti zao, kuimarisha
sekta ya afya, ikiwemo afya ya uzazi.
Imebainika kuwa, sasa nchi za Afrika
zinatumia dola 8 hadi 129 kwa kila mtu kwa afya, ikilinganishwa na nchi zenye
kipato cha juu, zinzotumia zaidi ya dola 4,000.
Mkataba wa kutokomeza aina zote za
ubaguzi dhidi ya wanawake ‘CEDAW’ wa mwaka 1979, unazitaka nchi wanachama,
kuchukua hatua kuhakikisha zinaheshimu utu wa bindamu na kuondoa ubaguzi.
Lengo la tatu kati ya 17 ya Maendeleo
Endelevu ‘SDGs’, inazitaka nchi wanachama kuhakikisha maisha bora yenye afya na
kukuza ustawi kwa watu wote.
MWISHO
Comments
Post a Comment