Skip to main content

SERIKALI YA WANAFUNZI ‘IPA’ PEMBA YAPATA VIONGOZI WAPYA

 



NA MARYAM NASSOR, PEMBA@@@@

UONGOZI wa serikali ya wanafunzi Chuo cha Utawala wa Umma Zanzibar, (IPA) tawi la Pemba, wamewataka viongozi wa chuo hicho, kutatua changamoto zinazowakabili kwa wakati.

Ombi hilo, limetolewa na Naibu waziri mkuu wa Serikali ya wanafunzi chuoni, Rashid Khamis Yussuf, mara baada ya kuapishwa na kupata cheo hicho huko mjini Chake chake.

Alisema, chuo hicho kinakabiliwa na changamoto lukuki, ambazo zinashindwa kupatiwa ufumbuzi kwa wakati sahihi, jambo ambalo linakwamisha maendeleo kwa wanafunzi.

Alisema kuwa, kuna kipindi walikuwa na shida ya huduma maji katika chuo hicho, na ilidumu kwa muda mrefu na muhasibu alishindwa kuchukuwa fedha, ili kulitatua tatizo hilo.

“Kuna wakati tulikuwa na shida ya maji katika Chuo chetu, na tatizo hilo lilidumu kwa muda, bila ya kupatiwa ufumbuzi na muhasibu yupo, ingawa alishindwa kulishughulikia,”alisema.

Mwanafunzi Deo Mabula Alfred, alisema changamoto inayowakera ni kutokupewa vitambulisho, kile cha mitihani na cha wanafunzi kwani walishakutana na tatizo la kutolewa kwenye mashindano ya bonaza, tu kwa sababu hawana kitambulisho.



Alisema kuwa, pia vyeti vya kumalizia masomo hawapewi kwa wakati kwani kuna wanafunzi wameshaingia  ngazi ya diploma lakini vyeti vyao hawajavipata.

Nae, mwanafunzi Ali Mohamed Omar, alisema kuwa tokea ajiunge na chuo hicho, ni mwaka mmoja na nusu sasa, hawajapatiwa hata elimu ya majanga kama moto na ndani ya chuo, mitungi ya kesi ya kuzimia moto yapo.

Alieleza kuwa, hata huduma ya kwanza hawajawahi kufundishwa na wanakaa wanafunzi wengi na kila mtu na maradhi yake, ikitokea mwanafunzi mmoja, kakutwa na majanga, basi watashindwa kumsaidia.

Nae, Rais wa Serikali ya wanafunzi wa chuo hicho, Nagila Abdallah Ali akijibu maswali ya wanafunzi hao alisema kuwa, yeye ni Rais mwanamke wa kwanza katika chuo hicho tokea kianzishwe na ameahidi kuzifanyia kazi changamoto hizo.



Aidha alisema kuwa, viongozi hao waliochaguliwa wafuate nyayo za viongozi waliyopita kabla yao, huku akimtolea mfano aliyekuwa Waziri wa mikopo aliyepita, alikuwa na ushirikiano mazuri na viongozi wenzake.

Aliwataka, viongozi waliyochaguliwa kutoa mashirikiano mazuri na kutatua shida zitakazowakumba wanafunzi, wakiwa wanaendelea na masomo chuoni hapo.

Awali Rais huyo wa Serikali ya wanafunzi, aligawa zawadi ya pedi kwa wanafunzi wa kike wa chuo hicho, kama shukrani ya kuchaguwa kwake na kuwataka viongozi hao waliyochaguliwa, kuwa tayari kwa safari ya kwenda Unguja kwa ajili ya kupatiwa mafunzo ya uongozi.





Katika hafla hiyo, waliapishwa  viongozi mbali mbali akiwemo, Naibu waziri mkuu wa Serikali ya wanafunzi, waziri wa afya na mazingira, waziri wa elimu na waziri wa michezo ambapo mawaziri wawili walikuwa ni wanawake.

                         MWISHO

Comments