NA HAJI NASSOR, PEMBA
MKURUGENZI wa Idara ya Katiba na
Msaada wa Kisheria Zanzibar Hanifa Ramadhan Said, amesema msako mkali unakuja
kuwabaini watu na taasisi, zinazofanyakazi za kutoa elimu, ushauri na msaada wa
kisheria, pasi na kujisajili kama sheria inavyotaka.
Alisema, Sheria
ya namba 13 ya mwaka 2018 ya Msaada wa Kisheria Zanzibar, inamtaka mtu yeyote au taasisi
inayotaka kujishughulisha na kazi hiyo, kwanza kujisajili, ili kuwa halali
kufanya kazi hiyo.
Alieleza kuwa,
Idara imebaini wapo watu na hata taasisi zinaendelea kutoa ushauri, msaada na
elimu ya kisheria, bila ya kujisajili, jambo ambalo ni kosa kwa mujibu wa
sheria hiyo.
Mkurugenzi
Hanifa, aliyasema hayo Septamba 16, 2023 ukumbi wa Kiwanda cha Mafuta ya Makoyo
Wawi Chake chake Pemba, wakati akijibu hoja za baadhi wa wahusika wa msaada wa
kisheria, kwenye mkutano wa nusu mwaka, ambao umeandaliwa na Idara hiyo, kwa
kushirikiana na UNDP.
Alieleza
kuwa, msako utanzia katika wilaya za Wete, Micheweni, Chake chake na kumaliza
wilaya ya Mkoani kwa Pemba, kisha kuhamia kisiwani Unguja.
Alieleza kuwa
msako huo, hauna nia mbaya bali ni kuitekeleza kwa vitendo sheria ya Msaada wa
kisheria ya Zanzibar, ambayo imelekeza mambo kadhaa, likiwemo la kujisaliji.
Aidha
Mkurugenzi Hanifa, alisema jingine ambalo wameligundua ni kuwepo kwa Mawakili
nao kijisajili kama wasaidizi wa sheria, jambo ambalo ni kosa kubwa zaidi.
‘’Ni kweli
kati ya wasaidizi wasaidizi wa sheria 250 kwa Unguja na Pemba ambao hadi sasa
walioshajisajili hawafiki hata nusu yake, na kwa upande wa wa Mawakili nao wapo
waliojisajili kama wadaidizi wa sheria, wakae tayari tunakuja,’’alieleza.
Katika hatua
nyingine, Mkurugenzi huyo wa Idara ya Katiba na Sheria Zanzibar kutoka Wizara
ya Nchi, Ofisi ya rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora Zanzibar,
alilipongeza shirika la UNDP kwa kuendelea kuwaunga mkono, katika shughuli zao
mbali mbali.
‘’Hata
mkutano huu wa nusu mwaka kwa wahusika wa msaada wa kisheria Zanzibar, wametusaidia
kwa asilimia kubwa, na ndio maana hata washiriki kutoka kisiwa cha Unguja leo
tunao,’’alieleza.
Aidha
aliwakumbusha wasaidizi wa sheria, kuendelea kuifikia jamii, kuwaelimisha
athari za udhalilishaji, migogoro ya ardhi, utelekezaji na rushwa, kwani ndio
msingi mkuu wa kazi zao.
Hata hivyo
amewakumbusha wasaidizi hao wa sheria kuwa, bado nia ya Rais wa Zanzibar Dk.
Hussein Ali Mwinyi wa ununuzi wa bajaji kwa taasisi 11 za wasaidizi wa sheria
Zanzibar, bado ipo pale pale.
Akifungua
mkutano huo, Afisa Mdhamini wa wizara hiyo Halima Khamis Ali, alisema kazi
inayofanywa na Idara ya Katiba na Msaada wa Kisheria, ni kubwa kwa jamii na
taifa.
Alieleza kuwa,
Mkurugenzi wake amekuwa akizaa mbinu na juhudi binafsi, kuhakikisha wasaidizi
wa sheria na taasisi zao zinafikia malengo yao waliojipangia.
Aidha aliwasisitiza
wasaidizi hao wa sheria, kuendelea kufanyakazi zao kwa ushirikiano, na taasisi
nyingine, ili kuhakikisha wanafikia malengo yao.
Mkurugenzi
wa Jumuiya ya wasaidizi wa sheria wilaya ya Chake chake ‘CHAPO’ Nassor Bilali
Ali, alisema wakati umefika sasa kwa taasisi nyingine, kuongeza ushirikiano na
wasaidizi wa sheria wanapokuwa na shughuli zao.
‘’Kwa mfano
mabaraza ya miji, halmshauri na Manispaa, wanakuwa na shughuli kadhaa, kama za
kuandaa sheria ndogo ndogo, msisite kutushirikisha,’’alifafanua.
Afisa sheria
kutoka Idara ya Katiba na Msaada wa kisheria Zanzibar Ali Haji Hassan, alisema
kazi zinazofanywa na wasaidi wa sheria zitakuwa na uhai, ikiwa wenyewe
watajiendeleza kielimu.
Baadhi ya
washirika wa mkutano huo, akiwemo Fatma Khamis kutoka ZAPAO, alishauri kuwa,
kunapokuwa na mikutano yao mikubwa ni vyema kuwepo na vipeperushi maalum.
Mkutano wa
nusu mwaka ulijadili mambo kadhaa, ikiwemo tathimini na mwelekeo wa maadhimisho
ya wiki ya msaada wa kisheria mwaka 2023, maandalizi ya jukwaa la tatu la mwaka
la maaada wa kisheria pamoja usajili wa watoa msaada wa kisheria.
Mwisho
Comments
Post a Comment