NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@
‘’NA mwaka 2030, najitupa tena jimboni,
na napandisha ngazi, nitaomba Ubunge jimbo la Kojani,’’ndivyo alivyoanza Katija
Mbarouk Ali.
Akiwa pembezoni mwa nyumba yao, eneo
la Kiuyu Minungwini, akijivalia kanga za chama cha Mapinduzi, huku akichezea
simu yake.
Katija, ni mcheshi, mweye sura ya
bashasha pamoja na kwamba, anawania kuwa kiongozi, kwa sasa ni mjasiriamali.
Akizungumza nami huku, akiangaza
macho yake usoni kwangu, na kwa upole, analiambia safari ndio kwanza, inaanza.
Kumbe kwa uchaguzi wa 2025, Katija
pamoja na ulemavu wake wa viungo, aligombea nafasi ya Uwakilishi jimbo la
Kojani, na kisha wajumbe kumkataa.
‘’Si wajumbe mara hii bado wameniona
ni mchanga, mwaka 2030, roho zikifika najitupa tena jimboni humo, kwa nafasi ya
ubunge,’’anasisitiza.
Nilipomuuliza, kama ameyapata
machungu kwa uchaguzi wa mwaka 2025, anasema, ameyaona kama mbolea na
kumuongezea mwendo.
‘’Hakuna kukata tamaa, maana sheria,
katiba na mikataba yote ya kikanda na kimataifa, haijamzuia mwanamke kugombea,’’anasisitiza.
Sio Katija pekee, ambao kwa uchaguzi
wa 2025, wajumbe na wapiga kura wamewakataa, lakini kwa Pemba wapo wanawake 25,
kwa nafasi mbali mbali.
Mwingine aliyegombea nafasi ya
Uwakilishi Jimbo la Mtambile Asha Said Suleiman, kwa tiketi ya ADA-TADEA,
anasema neno kuvunjika moyo kwenye maisha yake, halijazaliwa.
….aaaa…..kumbe Asha, anataka kuishi
kwenye msemo wa wahenga, kuwa mgaa gaa na upwa, abadani hali ugali mkavu.
Anaamini kugaa gaa, ni kule kuendelea
kuchukua tena fomu, mwaka 2030, na anaamini kula ugali na samaki, ni kushika madaraka
ya uongozi.
Anasema, moja ya changamoto alizoziona
ni, wagombea wanaume, kujiona kama vile nafasi za uongozi, zimeumbiwa wao.
‘’Nilikwenda kijiji kimoja ndani ya
Jimbo la Mtambile, wakati wa kampeni zangu za nyumba kwa nyumba, niliulizwa
kama nastahiki kuwa Mwakilishi,’’anakumbusha.
Anaona, kuanzia wapiga kura na jamii
kwa ujumla, haimini kuwa mwanamke, anahaki ya kuwa kiongozi na kuleta mabadiliko.
Lakini kumbe hata Khadija Anuwari,
aliyegombea nafasi kama hiyo jimbo la Wawi, kwa tiketi ya ACT-Wazalendo, bado
anasema vipo vyombo vyenye mamlaka, sio rafiki kwao.
‘’Bado inaonekana mwanamke kama vile
hawezi kushika nafasi, tena hata ya usheha, achia mbali ubunge, na uwakilishi,’’analalamika.
Anasema, wakati kampeni zake na hasa
za mtaa kwa mtaa, wapo waliomkebehi kwa kumwambia, wanawake ni wa jikoni tu.
‘’Wingine wananiambia kwamba,
ningejaribu nafasi za wanawake viti maalum, lakini sio jimbo,’’anafafanua.
Anachoomba ni uhai kutoka kwa Muumba,
maana mapema 2030, amefika tume ya Uchaguzi, kuomba tena kuchukua fomu.
Tatu Abdalla Msellem wa Ole Chake chake,
mwaka 2015 nae alijitupa jimboni kusaka nafasi ya uwakilishi, anasema hatosahau,
dharau alizofanyiwa.
‘’Moja ni kufananishwa na malaya,
muhuni na mtu niliyekosa kazi, lakini baya zaidi ni kwa wapiga kura, kuniomba
rushwa ya ngono,’’anasema.
WANAWAKE WALIOWAHI KUFANIKIWA
Bahati Khamis Kombo, anaewania kwa
awamu ya tatu, nafasi ya Uwakilishi Jimbo la Chambani, kwa tiketi ya CCM,
anasema wanawake hakuna kurudi nyuma.
Anaeleza, kuwania jimbo ambalo
wanaume wanadhani ni mali yao, sio kazi nyepesi, lakini umakini na ustahamilivu
ndio ngao.
Bahati kuanzia mwaka 2015 na mwaka
2020, alifanikiwa kupenya na kuwatumikia wananchi wa Jimbo hilo, kwa heshima.
Na sasa anasubiri huruma za wapiga
kura, kama wakiridhia wanaweza kumrejesha tena jimboni humo, kuendelea kuwa
mtumishi wao.
Sheha wa Chumbageni Mgeni Othman
Shaame na Katibu wa sheha Wawi Sham Haroub Said, wanasema hakuna kuwa laini,
kwenye kuwatumia wananchi.
Wananchi hawaamini kuwa wanawake,
wanaweza kuwa viongozi, sasa nafasi zinapopatikana, lazima umakini na uchapa
kazi uwepo.
Mkuu wa Mkoa wa kaskazini Pemba,
Salama Mbarouk, akaendelea kuwasisitiza wanawake wenye nafasi, kufanyakazi kwa bidii.
‘’Wanawake ambao wamo kwenye nafasi
za uongozi, wafanye kazi vizuri na kwa bidi, ili jamii ione na ifahamu nguvu ya
mwanamke,’’anasema.
WANAHARAKATI WA HAKI ZA WANAWAKE
Aliyekuwa Mratibu wa TAMWA-Pemba
Fat-hya Mussa Said, anasema hoja ya mwanamke kuwa kiongozi, isiwe ajenda, maana
katiba haijabagua.
Anawakumbusha wanaume, kuacha kuwatisha
na kuwapandikiza chuki wanawake, aidha walioviongozi ama wanaogombea nafasi mbali
mbali.
Katibu Mkuu wa Mwemvuli wa asasi za
kiraia Pemba ‘PACSO’ Sifuni Ali Haji, anasema changamoto za wanawake kuziogopa
nafasi za kugombea, ni mifumo dume iliyotawala.
‘’Inatokezea mwanamke anagombea na
mwanamme, basi wanawake wenzake wanatumika vibaya, ili aachie nafasi hiyo,’’anaeleza.
Msaidizi wa sheria, shehia ya Wawi Fatma
Hilali Salum, anasema mikataba na sheria, imeweka njia huru kwa kila mmoja
kugombea, ingawa hoja ya kutojiamini na kujengwa uwelewa kwa wanawake, hutanda.
Mkurugenzi wa Jumuia ya wasaidizi wa
sheria wilaya ya Chake chake ‘CHAPO’ Mohamed Hassan Abdalla, anasema jamii
isipowawapa nafasi wanawake, zipo huduma zitaendelea kudumaa.
WANANCHI WA KAWAIDA
Zamzam Khamis Sabour wa Kengeja,
anasema mitazamo ya jamii, juu ya wanawake na uongozi, huwaweka njia panda, kuomba
nafasi za uongozi.
‘’Sisi wanaume, inaonekana bado
tumelewa na madaraka, na kumuona mwanamke kama sio sehemu ya jamii, kuleta
mabadiliko,’’anasema Juma Haji Hakim wa Mtambile.
Aisha Hassan Juma wa Mbuyuni na mwanafunzi
wa kidato cha sita skuli ya Madungu Fatma Juma Nassor, wanawake wanaweza kuleta
mabadiliko, wakipewa nafasi.
MIKATABA/SHERIA
Sheria ya watu wenye Ulemavu nambari
8 ya mwaka 2022, kifungu cha 28 (1) (e) chenyewe kimetamka haki ya kushiriki,
katika shughuli za kijamii, ikiwemo siasa.
Mkataba wa kimataifa wa haki za watu
wenye ulemavu mwaka 2006, Ibara ya 29 (b) (i), kwamba watu wenye ulemavu, wana
haki ya kujumuishwa kisiasa.
Mkataba wa kimataifa wa
kutokomeza aina zote za ubaguzi dhidi ya wanawake ‘CEDW’ wa mwaka 1979, Ibara
ya 7, ukasisitiza kwamba, lazima hatua zichukuliwe, kuhakikisha wanawake
wanakuwa na ushiriki sawa kwenye ulingo wa siasa.
Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 kifungu cha 21(1), kinafafanua,
watu wote ni sawa mbele ya sheria, na wanayo haki bila ya ubaguzi, kupata haki
mbele ya sheria.
NINI ATHARI YAKE
Haji Mohamed Omar wa Kojani, anasema
kwanza ni kuporomosha huduma za wanawake na watoto katika jamii.
Wakili wa serikali Safia Saleh Sultan,
anasema ni kudumaza demokrasia, sheria na mikataba inayozungumzia, haki za
jamii.
NINI KIFANYIKE
Mwakilishi wa Chambani Bahati Khamis
Kombo, anashauri wanawake, wapewe darsa la kuwajengea uthubutu.
Asha Haji Said wa Mtambile, anasema
sheria zizidi kutangaazwa, juu ya uhuru na haki za wanawake, ikiwemo kugombea
nafasi mbali mbali.
Mkurugenzi wa Chama cha waandishi wa
Habari Wanawake Tanzania TAMWA-Zanzibar Dk. Mzuri Issa Ali, anasema ni
kuendelea kuwakosesha haki zao za kidemkrasia.
Mwisho




Comments
Post a Comment