NA ZUHURA JUMA, PEMBA@@@@
Farida Juma Khamis mwenye
umri wa miaka 59 mkaazi wa Kichangani shehia ya Mgogoni Wilaya ya Chake Chake,
ni miongoni mwa wanawake wanaosaka uongozi kwenye majimbo yao.
Farida
ni mgombea uwakilishi Jimbo la Wawi kupitia tiketi ya chama cha Wakulima (AFP) ambae
ana lengo la kushirikiana na wananchi katika kuibua changamoto ndani ya vijiji
na kuzichukuwa kwa ajili ya kwenda kutatuliwa.
Mgombea
huyo uwakilishi anasema, atakapopata nafasi ya kuliongoza Jimbo atahakikisha
kila mwananchi anapata fursa ya kushiriki katika vikao vya kuibua kero
zinazowakabili, ambazo atazichukuwa na kuzitetea kwenye chombo cha maamuzi.
Anasema,
uongozi ni dhamana, hivyo akifanikiwa kuwa mwakilishi atarudi kwa wananchi ili
kuwaletea maendeleo endelevu katika Jimbo.
Farida
hakushawishiwa na yeyote kugombea nafasi hiyo, bali alipoona kwenye Jimbo kuna
changamoto mbali mbali ambazo hazijafanyiwa kazi, aliona ni vyema agombee ili
apate nafasi ya kuzitatua.
"Hao
viongozi waliopita kwenye jimbo hili hawakutuletea maendeleo, hivyo kwa vile
mimi ni mwanamke na ni mama, kuliona Jimbo hivi siridhiki," anasema.
Amepania
kuliweka Jimbo hilo katika hali nzuri, kwa kuondoa matatizo yote yaliyopo na
kuhakikisha analeta maendeleo.
Mgombea
huyo anasema, hatokuwa tayari kuona elimu ya vijana wa Jimbo hilo inatumiwa kwa
uhalifu, bali atawakomboa kwa kuwapatia na shughuli mbali mbali za kufanya ili
wajipatie kipato.
Anasema,
vijana wengi wanamaliza masomo yao hawana kazi ya kujipatia riziki, hivyo
atahakikisha anawatafutia miradi ambayo itawawezesha kuwainua kiuchumi.
"Vijana
hawana kazi, hivyo muda wote unawakuta maskani, hali ambayo inasababisha
kujiingiza kwenye makundi ya kihalifu ikiwemo, madawa ya kulevya, wizi na hata
udhalilishaji," anasema.
Anasema
kwa vile vijana ndio nguvu kazi ya Taifa, hana budi kuekeza katika kundi hilo
ili kujenga jamii iliyobora ambayo itajitekemea kiuchumi na hayo ndio maendeleo
wanayoyataka.
Kundi
la pili atakaloliangalia mgombea huyo ni wanawake, ambapo anafahamisha kuwa
atahakikisha wanapata elimu itakayowasaidia kuanzisha vikundi vya ushirika, ili
kujipatia kipato kitakachowasaidia na familia zao.
"Kuna
wanawake wajane na waliotelekezwa na waume zao na wana watoto wanataka huduma,
hivyo nitawahamasisha kufanya miradi mbali mbali wapate kujikomboa kiuchumi,"
anafafanua.
Anasema,
Serikali inatoa mikopo kwa wajasiriamali wote na pia kuna mikopo kwa ajili ya
wanawake pekee, hivyo atahakikisha wanautumia mkopo uliopo kwa ajili ya kupata
mtaji kwa kuendesha shughuli zao za ujasiriamali.
Farida
alijiunga na chama hicho tangu mwaka 2006 na ilipofika mwaka 2017 aliteuliwa
kuwa Mjumbe wa Bodi kwenye chama hicho, ambapo nafasi hiyo ameshaitumia kwa
miaka tisa sasa.
"Mwaka
huu wa 2025 nimeamua kuingia jimboni kugombea nafasi ya uwakilishi na nashkuru
wajumbe wamenipitisha na kwa sasa nipo kwenye kinyang'anyiro cha kulitafuta
jimbo," anasema.
Aliwaomba
wananchi wamchague ili aweze kuwatatulia changamoto zilizomo kwenye Jimbo lao
ambazo zimekuwa kero kubwa la kudumaza maendeleo yao.
Mgombea
huyo, anasema hakuhamasishwa na mtu yeyote kugombea uongozi, lakini alipoona
hali ya Jimbo kimaendeleo haiko vizuri, ndipo alipoona ili alikomboe ipo haja
ya kuwa kiongozi.
"Zamani
nilikuwa na hofu kugombea lakini kwa sasa jamii imekuwa na uwelewa wa kutosha
juu ya umuhimu wa mwanamke kuongoza, hivyo nimeona nitimize lengo langu,"
anaeleza.
Farida
anaeleza, tangu zamani alikuwa na ujasiri wa kuongoza ingawa alikosa kujiamini
kwani alihisi kama jamii haitomkubali, ingawa alipoamua kugombea wananchi wamemuunga
mkono kiasi ambacho kimempa hamasa zaidi.
Mgombea
huyo anasema, atakapofanikiwa kuwa mwakilishi atahakikisha atakeleza vyema
majukumu ya nyumbani na ya kazi kwa wakati wake bila kuathiri upande wowote.
"Pamoja
na nafasi niliyonayo kwenye chama lakini pia ni Msaidizi mwalimu Mkuu na
natekeleza vyema majukumu yangu ya uongozi na ya nyumbani, hivyo hata nikipata
nafasi ya uwakilishi nawaahidi wananchi kuwa nitatekeleza vizuri,"
anafahamisha.
Anataja
changamoto iliyomkwaza kuwa ni kukosa ruzuku ya kufanyia mikutano ya kampeni,
hali ambayo ilikaribia kumkatisha tamaa.
"Kwa
vile ilikuwa nimeshatia nia ya kugombea, nilisema nitahakikisha natumia nguvu
yangu ya kifedha kufanya mikutano, ili kuwaomba wananchi kura za ndio,"
anafafanua.
Mume
wa mgombea huyo ambae pia ni Mgombea Urais kupitia chama hicho, Said Soud Said
anasema, mke wake wanampa ushirikiano katika familia yao na ndio maana
amejiamini kuingia jimboni kugombea.
Anasema,
pia wananchi wa Jimbo lao wanampa ushirikiano kwani wametambua kwamba mwanamke
ni mlezi na ana imani, hivyo wamemuahidi kumchagua ili awatatulie matatizo yao.
"Naamini
kwamba wananchi wa Jimbo hili watamchagua kwa sababu ni mwanamke jasiri,
anaejiamini na ana uwezo wa kuongoza," anasema.
Alimshauri
mgombea huyo, atakapopata ridhaa ya kuongoza Jimbo, ahakikishe anarudi kwa
wananchi kusikiliza kero zao na kuzitatua kwa wakati, kwani wataendelea kujenga
imani kwake na kuendelea kumchagua kwenye miaka mengine ijayo.
Mgombea
huyo urais pia aliwaomba wananchi wamchague mgombea huyo uwakilishi, ili wapate
maendeleo ya uhakika katika Jimbo lao.
Mama
huyo ameolewa na ana watoto nane, ambapo ana elimu ya cheti katika fani ya
uwalimu aliyoipata katika chuo cha Nkuruma mwaka 1987.
Amina
Ahmed Mohamed ambae ni Kaimu Mratibu wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake
kwa upande wa Pemba, anasema TAMWA imekuwa ikitoa elimu kwa wananchi ili
waondokane na mawazo mgando kwamba mwanamke hawezi kuongoza na ndio maana mwaka
huu wamegombea wengi.
"Jamii
sasa imepata uwelewa na wamejua umuhimu wa mwanamke kuongoza kwa sababu
waliokaa majimboni wote wamefanya vizuri na maendeleo yanaonekana,"
anaeleza.
Kaimu
huyo anasema, pia wanawajengea uwezo wanawake wenye nia ya kugombea uongozi ili
wajiamini, wawe na ujasiri pamoja na kutekeleza yale ambayo wanayaahidi kwa
ajili ya kujenga Taifa lenye maendeleo.
Mgombea
huyo ametekekeza haki yake ya kushiriki katika demokrasia na uongozi, kama
Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1964 ilivyoeleza kwenye kifungu cha 21 (2) na kifungu
cha 67 (1) cha Katiba hiyo kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2010.
MWISHO.


Comments
Post a Comment