NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@
SIKU hizi imekua
tofauti na zamani, wanawake kuwa viongozi sio jambo geni kujitokeza kugombea
nafasi hizo na kushinda.
Nchi kadhaa, hivi sasa
zimeendelea kutokana na wanawake kupewa nafasi za uongozi na kufanikiwa kuleta
mabadiliko ya kiutendaji.
Mataifa kama ya Ethiopia, Liberia pamoja na Tanzania, ambazo uchumi wake
umepanda na kupata mabadiliko makubwa katika sekta tofauti.
Ellen Johnson-Sirleaf
ni Rais wa kwanza mwanamke barani Afrika, hata hivyo yeye sio mwanamke wa
kwanza kuongoza nchi barani Afrika.
Maana yupo Malikia
Zauditu wa Ethiopia alieongoza nchi yake kwa miaka 13 toka mwaka 1917 hadi
1930.
Katika miaka michache
iliopita, Tanzania imepata mafanikio makubwa, ikiwa pamoja na utulivu wa kisiasa na
maendeleo katika sekta mbali mbali kufuatia uongozi wa nchi kushikwa na
Rais wa kwanza mwanamke, Dk. Samia Suluhu Hassan.
Mama Samia hivi sasa anahesabika kuwa ni mfano mzuri wa kuigwa na wanawake wa
hapa nyumbani na nchi nyingine.
Mifano mingine ya
wanawake wanaofanya vizuri kweye nafasi za uongozi ni balozi Amina Salum Ali
ambae ni Waziri wa Fedha, Anna Makinda aliyekuwa Spika wa Bunge la Jamuhuri ya
Muungano wa Tanzania.
Kawaida familia nyingi
humlea mtoto wa kike kwenye utamaduni na mifumo isiyowaweka tayari kuingia katika
uongozi na humuwekea mazingira ya mtumishi wa kazi za ndani kitu kinachojenga
taswira mbaya katika makuzi ya watoto.
Licha ya vikwazo na changamoto mbali mbali wanazopitia watoto na vijana wakike, bado uwezo wao wa kuongoza ni mkubwa, na hili linadhirika mara tu anapopewa nafasi.
Tukumbuke kuwa Idadi ya vijana wenye umri wa miaka 15 hadi 35 imefikia,
699,845, wanawake 368,066 na wanaume 331,779, ni wazi kuwa vijana wakike ni
wengi kuliko wakiume.
Aidha idadi ya vijana
kuanzia umri wa miaka 15 hadi 24, imefikia 384,647 wanawake ni 202,067 huku
wanaume ni 182, 580.
Sham Haroub Said, Katibu
wa sheha Wawi, anasema anasema wanawake wana mchango mkubwa katika jamii na
familia zao licha ya changamoto za kifamilia kuwarudisha nyuma.
Kawaida familia nyingi
humlea mtoto wa kike kwenye utamaduni na mifumo isiyowaweka tayari kuingia
katika uongozi, badala yake humfanya kama mtumishi wa kazi za ndani na mtoto wa
kiume kama muangalizi wa familia.
Mwakilishi wa Jimbo la
Chambani Bahati Khamis Kombo, anatarajia kuwaona wanawake, sasa wakiwa mbele
katika nafasi ya uongozi, hasa baada ya mazingira kuwa rafiki.
Anasema hata serikali ya awamu ya nane, imekuja kuwapa heshima yao wanawake katika safu ya uongozi, kwa kuwepo wakuu wa mikoa wawili wanawake, kati ya watano.
Mkuu wa Mkoa wa kaskazini
Pemba Salama Mbaruk Khatib, anasema uwezo wa wanawake katika uongozi, sasa
unaonekana maana Dk. Mwinyi amewaanini mno kwa utendaji wao wa kazi.
‘’Kwa mfano nafasi ya
Katibu Mkuu Kiongozi na katibu wa Baraza ka Mapinduzi Mhandisi Zena Ahmed Said,
amekuwa wa kwanza tokea Zanzibar ijitawale mwaka 1964,’’anasema.
Eneo jingine anasema,
ni kuwapo wa wakuu wa wilaya wawili kati ya wilaya nne za Pemba, jambo ambalo
halijwahi kutokezea kwa historia ya mwanamke na uongozi.
JAMII
Ali Salim Hamad wa Mchanga mdogo, anasema, ile dhana ya 50 kwa 50 kwa wanawake katika ngazi ya maamuzi, imeanza kunukia mno, maana wapo hata masheha wanawake.
Omar Haji Hasnuu wa Wawi, anasema Katibu wa sheha ni mwanamke anaefanyakazi kwa bidii na kumsaidia kwa kiasi kikubwa sheha wao.
Maryam Hassan Kombo wa Mizingani Mkoani,
anasema kasi ya Dk. Mwinyi inayochagizwa na wanaharakati kama TAMWA, imeonesha
uhodari wa utendaji kazi wa wanawake.
‘’Kwa mfano Mkuu wetu wa wilaya ya Mkoani ni
mwanamke, lakini tunaoona anavyoendesha wilaya, kw ahakika kweli wanawake
wanaweza,’’anasifia.
Hidaya Mjaka Ali mwenye ulemavu wa viungo
anaeishi Vitongoji wilaya ya Chake chake, anakiri kuwa sasa juhudi za wanawake
katika safu ya uongozi inaonekana kwa ufanisi.
‘’Ukitaja Tanzania rais wetu ni mwanamke,
ukienda wilaya ya Chake chake, mkoa wa kaskazini Pemba na hata Katibu mkuu kiongozi
na Katibu wa baraza la Mapinduzi, nae ni mwanamke,’’anasema.
YALIKUJAJE HAYA
Mkurugenzi wa Chama cha waandishi wa habari Wanawake Tanzania
TAMWA-Zanzibar Dk. Mzuri Issa Ali, anasema zipo juhudi kadhaa wao
walizozifanyia kuanzia zaidi ya miaka 25 iliyopita.
Anasema, katika siku za hivi karibuni,
walikuwa wanaendesha mradi wa kuinua
wanawake na uongozi na demokrasia SWIL, ambao unalenga kuwaonesha haki za uongozi
na nafasi yao katika jamii.
Dk. Mzuri anakiri kuwa, kwa muda mrefu,
wanawake wamekua na nafasi ndogo katika nafasi za uongozi na ngazi za maamuzi,
na ndio maana waliamua kuwajengea uwezo na kuwashajiisha watumie fursa ziliopo za
kugombea.
Anasema, tathmini inaonesha idadi ya wanawake nchini, inaendelea
kuongezeka za uongozi kutokana na elimu inayotolewa katika jamii na utayari wa
mtoto wa kike mwenyewe, kujitokeza mbele na kuongoza.
Akizungumza katika moja ya mafunzo ya kuwajengea uwezo vijana wa kike kwa lengo
la kuisaidia jamii, aliwahi kusema kuwa, wameamua kuwakutanisha vijana wakike wenye
vipaji tofauti na uthubutu, ili kusaidia wanawake na jamii kiujumla.
Alisema dunia imeamini
kuwa wanawake wana uwezo katika nafasi za uongozi kama anavyoweza kulea
familia, vijana wa kike wakikaa pamoja na kupeana mawazo na kufanya maamuzi ya
kusaidia jamii kufika sehemu nzuri.
Alitumia nafasi hiyo
kuwataka vijana wakike kuitumia vizuri nafasi hiyo, kwa kuendeleza vipaji na
kuiga mfano kutoka kwa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia
Suluhu Hassan.
Akitolea mfano
alipokua kijana, Dk. Mzuri alisema alipata nafasi ya kuajiriwa serikalini
lakini hakuona kama nafasi nzuri kwake ya kuitetea jamii hasa wanawake, hivyo
aliamua kujiunga na taasisi binafsi kwa lengo la kuisaidia wanawake kwenye
nafasi za siasa, uchumi wa masoko na uongozi.
"Mfano sheria
iliyotumika ya 1985, zilimkandamiza mtoto wa kike na kulazimika, wanaopata
ujauzito kufungwa, kupitia nafasi hiyo walifanikiawa kufanya utetezi kwa sheria
zenye madhara na mifumo dume zilizowakandamiza wanawake zifutaw,"alisema.
Kwa mwaka 2020, wanaume waliojitokeza kugombea
uwakilishi Zanzibar 190, walioshinda 42 na wanawake 61 na waliobahatika
kushinda ni wanane (8) tu.
Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi kwa kutambua umuhimu
wa wanawake na kuwaaamini kwenye uongozi, amewapa nafasi mbalimbali ikiwemo
nafasi za mawaziri, makatibu wakuu.
Dira ya mpango wa
Maendeleo ya Zanzibar yamwaka 2020 hadi 2050 imeelezea kuboresha mfumo wa
kisisa, kupitia taasisi mbalimbali katika masuala ya uongozi.
Kwa mijibu wa
makubaliano ya Maputo Protocol yaliyofanyika Julai 11, 2003 nchini Msumbiji,
kipengele namba 9 imeonesha haki ya wanawake kushiriki katika siasa
na mchakato wakushiriki katika vyombo vya kutoa maamuzi.
SWIL
Utekelezaji wa mradi
huo ambao ulitarajiwa kuwafikia na kuwawezesha wanawake 6,000 kwa Unguja na
Pemba, katika kudai haki zao ili nao waweze kuwawezesha wengine, tayari
umeonyesha njia katika kufikia hatua ya kudai haki zao za uongozi.
Mradi huo wa
SWIL ambao unafadhiliwa na ubalozi wa Norway umetekelezwa maeneo mbalimbali
ambapo kwa upande wa Pemba tayari umeshawafikia
wastani wa wanawake zaidi ya 4,000.
Kamati hizo
zinajulikana kwa jina la kiutaalamu 'citizen brigged' asilimia 60 ni wanawake
na 40 ni wanaume ambao ndio walengwa wakuu wa kutowa ushirikiano kufikia
malengo ya mradi huo.
Mkurugenzi Mtendaji wa
mradi wa ‘SWIL’ kutoka PEGAO Hafidh Abdi Said, anasema kwa wilaya za Pemba,
mradi umevuuka lengo kwani wameshajengewa uwezo zaidi ya watu waliokusudiwa.
Anasema
uhamasishaji huo haukulenga kuwajengea uwezo wanawake hao kuwa viongozi
serikalini, wala vyama vya siasa pekee bali hadi ndani ya sekta iliyomo ndani
ya jamii.
Aliyekuwa Mratibu wa
mradi huo kutoka TAMWA Pemba, Fat-hiya Mussa Said, anasema tayari mradi
umefikia hatuwa ya lengo lililokusudiwa, ambapo ndio tarajio lake kwani mradi huu
unawawezesha wanawake na jamii.
Anaeleza kuwa
utekelezaji wao mkubwa ndani ya mradi huo, kuwawezsha waandishi wa
habari, ili wapate uweledi wa masuala ya
wanawake na uongozi.
“Tunaamini kama
tukiwawezesha vizuri waandishi wa habari watakuwa na maono mapana na
kuondokana na dhana zilizo ndani ya jamii, juu ya wanawake na uongozi.
WAHAMASISHAJI
JAMII KUPITIA MRADI
Nachia Khamis
Mohamed wilaya ya Mkoani anasema katika kutembelea vijijini, wamebaini
changamoto mbalimbali zinazosababisha wanawake wasifikie malengo ya kuwa
viongozi, ikiwemo uwelewa hafifu.
Anasema wamebaini
wanawake wengi wanakuwa na lengo la kugombea nafasi za uongozi, ingawa
wanakwazwa ikiwemo ndoa kwani hupambana na wivu kwa wanaume zao.
Ali Abdalla
Juma wa Chake chake anasema kutokujiamini, jamii kuwa na uwelewa
mdogo, unaohusiana na wanawake na uongozi ni eneo jingine la changamoto.
WANAHARAKATI
Khadij Henock
Maziku, anasema hata nafasi za usheha, udiwani na nyingine katika jumuiya
mbalimbali, zinaonekana kukamatwa na wanawake, jambo ambalo hapo zamani
halikuwepo.
Uthibitisho wa hilo
ni pale tunapoona kuongezeka idadi ya masheha katika wilaya zilizopo kisiwa cha
Pemba, kwa upande wa wilaya ya wete inayo masheha wanawake 14 kati ya shehia 36
jambo ambalo hapo nyuma hawakuwepo.
Sifuni Ali Haji anasema,
lazima wenye mamlaka waone aibu pale wanapowaacha wanawake katika nafasi za uongozi,
kwa vile wanapopewa nafasi hizo, hufanya vizuri.
VIONGOZI
WA DINI
Sheikh Said Ahmad
Mohamed kutoka ofisi ya Mufti, anasema mwanamke hajakatazwa kuwa kiongozi na
hasa, akiwa atazingatia maadili, mila na desturi za dini na jamii yake.
Father Zeno Marandu wa
Kanisa Katoliki Chake chake, anasema hajakatazwa mwanamke kuongoza, kwani
anasema hakuna kondoo mwanamke kuchungwa na mwanamme, hivyo lazima na wanawake
nao wafike kwenye zizi, ili kuwaangalia .
MWISHO.




Comments
Post a Comment