NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@
‘’HESHIMA, bidii ya kazi, upole, ustahamilivu
na kufanya uamuzi sahihi, ndio njia moja wapo za kuwatumikia watu,’’anasema
Mkuu wa wilaya ya Mkoani Miza Hassan Faki.
Anasema inawezekana waliowengi, wandhani ili uwe kiongozi
mzuri, lazima uchupe mipaka, kimavazi, heshima, uondoe upole, ukiuke sheria,
jambo ambalo ni tofauti.
Anahadithia wakati wakiwa mtendaji wa Tume ya Uchaguzi,
miaka 15 iliyopita, alichunga sana nidhamu na heshima yake, huku akihakikisha
halazi kazi.
Alizingatia mno kivazi cha heshima, kujenga mapenzi ya kazi
kwa kila mmoja, na kuhakikisha kitengo chake hakifeli kwa jukumu, walilopewa.
''Kuna wakai tunasafirisha vifaa tena siku ya mvua, ilipofika
majira ya saa 5:50 usiku, wapo walionitaka nirudi nyumbani kumpunzika na wao
wataendelea na kazi, niligoma,''anakumbushia.
Aliwaambia kama ni wakati wa kazi wanafanya kwa pamoja na
wakati wa kumpunzika, wanapumzika kwa pamoja, maana kazi ndio kazi.
‘’Siku hiyo kila mmoja aliniona kama sio mwanamke wa
kawaida, maana nilichapa kazi, hadi tunamaliza zoezi la usambaazaji vifaa ni saa
12: 00 alfajiri, nimeroa chapa,’’anasema.
Mkuu huyo wa wilaya ya Mkoani Miza Hassan Faki, anasema utii
wa kazi kwa mwanamke, ni njia sahihi na kulinda heshima na nidhamu yake na kwa
wingine.
Anakiri kuwa, hakuna uhusiano wowote wa mwanamke kuwa
kiongozi na kuvunja mipaka, maadili na heshima yake, na ikiwa wako wanaofanya
hivyo, ni mwenendo na malezi yao ya asili.
Akawataka wanawake wanaosaka uongozi, kwanza kuondoa hofu
kwamba kwa sababu ya jinsia yao, ikiwa wanaweza kutekeleza majukumu ya umma.
'’Utumishi wa umma, tayari miongozo, sheria na kanuni zimeshawekwa, unapofika kwenye nafasi ya uongozi, iwe usheha, ukuu wa wikaya, Katibu mkuu na hata Waziri, ni kuifuata tu,’’anasema.
Kumbe anaona hakuna
tofauti ya kutisha kati ya mwanamke na mwanamme, kwenye utekelezaji wa majukumu,
na hasa ikiwa mwanamke huyo, anataka kweli kuwatumikia watu.
Anakumbuka akiwa Katibu Tawala wilaya ya Mkoani, aliwasaidia
sana wakuu wake wa wilaya, akiamini wakiharibu wao, ndio ameharibu yeye.
Siri nyingine ambayo anasema waliowingi hawaifahamu,
wanadhani anapoharibu mkuu wake wa kazi, kama vile muhudumu ama dereva hahusiki,
jambo ambalo sio sahihi.
‘’Niwatake wanawake ambao wanahudumu kwenye nafasi mbali
mbali au wanaowania nafasi, kufanyakazi kwa bidii na wawe na bango, hakuna
kushindwa,’’anasema.
Mkuu wa wilaya ya Chake chake Mgeni Khatib Yahya, ambae
alihamishiwa wilaya hiyo akitokea wilaya ya Micheweni, anasema hakuna kazi
kwenye kuongoza.
Akawaelekeza wanawake wenzake, kuzingatia mambo makubwa
matano, ambayo hayo akifanikiwa anaweza kuongoza hata taifa, sembuse shehia ama
mkoa.
Moja, ni huruma kwa unaowaongoza, ili kuhakikisha majukumu
ya kazi yanakamilika, ni kuweka kando uongozi wa maguvu na vitisho.
Jingine ni kufuata maadili na kujenga heshima kwa kila
mtumishi, jambo ambalo litakupa marafiki kuanzia muhudumu, mtunza fedha hadi
dereva.
‘’Jingine Mkuu huyo wa wilaya, analoliona linafaa kwa
wanawake kulifuata ni kujua walau kidogo kanuni, sheria na miongozo ya utumishi,
ili uwe mtatuzi mzuri wa migogoro,’’anasema.
Akawakumbusha wanawake wanaowani uongozi kuwa, jambo
jingine na muhimu la kuzingatia, ni kuwajua watu tabia zao, kuanzia mkuu wako
wa kazi hadi unaowaongoza.
Kujiamini kunakofuatana na kupenda ushauri, ni eneo jingine
ambalo kiongozi mwanamke, anatakiwa kuwa nalo hilo na kujiondoa kwenye safu
kuwa anajua kila kitu.
‘’Tena hili, wapo wengi wanaolipuuza na wakati mwingine
hata kupekelekea kuzikosa nafasi, iwe za uteuzi ama za kupigiwa kura,’’anawakumbusha.
Dc Mgeni, anawakumbusha wanawake, kuwa wasiwe na woga wa
kuzitafuta nafasi, maana hakuna katiba, sheria, miongozo wala kanuni, iliyomzuia
mwanamke.
‘’Mimi mwenyewe nilianzia ngazi ya shehia, jimbo na kisha
nikabahatika kuwaongoza wananchi kuanzia wilaya za Wete, Micheweni na sasa nipo
Chake chake,’’anasema.
Anasema, wanahofu kuwa, kila kiongozi mwanamke kama vile ni
mvunja maadili au anaeipa kisogo familia yake, jambo ambalo sio sahihi.
‘’Na kwanza Tanzania kumpata Rais mama Samia, kwangu
amekuwa ni muongozo wa utendaji kazi, pamoja na namna anavyoshughulikia shida
za wananchi, bila ya ubaguzi,’’anasema.
Ndio maana akawataka wanawake wenzake, kuiba nyenendo,
tabia, hulka, misimamo na kuchangamana na watumishi, kama anavyofanya Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Samia Saluhu Hassan.
KIPI WANAWAKE WANAOTAKA UONGOZI WAKIEPUKE?
Mkuu wa wilaya ya Mkoani Miza Hassan Faki na mwenzake wa
Chake chake Mgeni Khatib Yahya, wanasema ni matumizi mabaya ya ofisi.
Wakifafanua kuwa, wapo baadhi wanapopata nafasi, mfano
usheha huanza kunuka na kutoa harufu za tabia mbaya, kwa matumizi mabaya ya
cheo.
Jingine wanawashauri wanawake, wasiache kuzishughulikia
familia, maana wajibu huo, hauondoki maana ni kutoka kwa Muumba.
Eneo jingine, ni kutoacha kuzibebe shida za wananchi kama zao
binafsi, na kuhakikishi hawalali, hawali, hawanywi ikiwa ufumbuzi haujapatika.
WANAHARAKATI WANASEMAJE?
Dk. Mzuri Issa Ali, ni Mkurugenzi wa Chama cha waandishi wa
habari wanawake Tanzania TAMWA-Zanzibar, anasema ujasiri wa mwanamke kiongozi,
huanzia kwenye utekelezaji wa majukumu yake.
‘’Tunapotaka wanawake waingie kwenye safu ya uongozi, ni
kuwataka kuwatumikia wananchi na sio jambo jingine lolote,’’anasema.
Katibu Mkuu wa Mwenvuli wa asasi za Kiaria Pemba ‘PACSO’
Sifuni Ali Haji, anasema vikwazo vilivyopo kwa wanawake wanaowania uongozi, wa kuviondoa
ni wanawake wenyewe.
‘’Njia moja ni kuvunja ukimya, wanapoona nafasi zao
zinachukuliwa ni kusema, kugombea, kurekebisha ama kukataa,’’anaeleza.
Mohamed Hassan Abdalla Msaidizi wa sheria wilaya ya Chake
chake, anasema miongozo ya kisheria, ipo wazi juu ya kila mmoja kuomba nafasi.
Anasema, wanawake waendelee kujengewe uwezo, maana kwa karne
moja iliyopita, waliachwa nyuma na kuonenakana kama bihdaa ya kukaa ndani, jambo
ambalo sio sahihi.
MIONGOZO INASEMAJE
Katiba ya Zanzibar ya 1984, kwenye kifungu cha
11 na cha 14, vimeweka wazi kuwa kila mzanzibari anayo haki na uhuru wa
kushiriki kwa ukamilifu katika kufikia uamuzi juu ya mambo yanayomuhusu.
Dira ya Zanzibar ya 2050 imeelezea jinsi gani
masuala ya usawa wa jinsia, juu ya kuondoa unyanyasaji na kuimarisha mifumo ya
uwezeshaji wanawake.
Sera ya jinsia inaeleza ushiriki wa wanawake
katika vyombo vya utoaji maamuzi, katika ngazi zote ni mdogo na kwa hivyo
serikali, kwa kushirikiana na wadau wingine, itafanya juhudi kuona makundi yote
na yaliyopembezoni.
Jumuiya ya Maendeleo ya nchi za Kusini mwa
Afrika (SADC), ambayo mkataba wake ulitiwa saini mwaka 2008 inaeleza, kutaka
kuondoa utafauti na kuwatenga wanawake katika nyanja mbalimbali za maendeleo.
Makubaliano yanayojulikana kama ‘Itifaki ya
Maputo’ ambayo yalifanyika Msumbiji mwaka 2003, inacho kipengele kinachoonyesha
haki ya wanawake, ikiwemo kushiriki katika siasa na vyombo vya kutoa
maamuzi.
Mkataba wa kimataifa wa kutokomeza aina zote
za ubaguzi, (CEDAW) wa mwaka 1979 ambao unapinga aina zote za udhalilishaji na
kusisitiza, ushiriki wa wanawake katika uongozi.
Mpango wa Utekelezaji wa Beijing mwaka 1995,
ibara ya 7 inataka ushiriki katika vyombo vya maamuzi kwa kuzingatia uwiano wa
kijinsia kwenye ngazi zote za uongozi.
NINI ATHARI YAKE
Hidaya Mjaka Ali mwenye ulemavu wa viungo, anasema ni
kuendelea kukukosa huduma stahiki, kama za afya ya uzazi, kwa kule kukosa mtetezi
wa moja kwa moja.
Mkuu wa mkoa wa kaskazini Pemba Salama Mbarouk Khatib, anasema
ni kuendelea kudhalilishwa kidemokrasia na kiuongozi,’’anasema.
NINI KIFANYIKE
Mkuu wa wilaya ya Mkoani Miza Hassan Faki, anasema kwa
nafasi ambazo ni za uteuzi wanawake, waendelee kuaminiwa na za kura wapigiwe.
Haji Kassim Haji wa Mchanga mdogo, anasema wakati umefika
kwa wanaume, kuwakatia minyororo ya utumwa wanawake, na sasa kuwapa haki zao,
ikiwemo ya uongozi.
Mwanafunzi wa kidato cha sita skuli ya Madungu Hafsa Issa
Khamis, anasema elimu ya uongozi, ianzie ngazi ya elimu ya maandalizi, ili
kuwajengea uthubutu mapema.
Rais wa Zanzibar Dk. Hussein Ali Mwinyi, kwenye sherehe za
kutimiza miaka mwili ya uongozi wake, zilizofanyika Wete, aliahidi kuwapa
nafasi zaidi wake.
mwisho


Comments
Post a Comment