NA ZUHURA JUMA, PEMBA@@@@
WAKATI nchi ikielekea kwenye uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29 mwaka huu, wanawake wengi wamejitupa majimboni kwenye kinyang'anyiro cha kugombea uongozi.
Mwaka huu wa 2025 wanaonekana wanawake wengi wakinadi sera zao kwenye mikutano ya kampeni na wengine wakipita nyumba kwa nyumba kutafuta kura ambazo zitamuwezesha kuibuka mshindi kwenye Jimbo lake.
Kuna wanaogombea ubunge, uwakilishi na udiwani, hivyo kila Jimbo unalopita kuna wagombea wanawake wanaosaka kura kwa kishindo.
Hii ni kutokana na kwamba elimu inayotolewa sasa imezaa matunda, kwani wanasimama imara tena bila woga kuomba kura ili kuhakikisha wanaingia kwenye vyombo vya maamuzi kwa ajili ya kuleta maendeleo kwenye majimbo yao.
Mkasi Ali Hamad mwenye umri wa miaka 35 ni mmoja kati ya wanawake waliojitupa majimboni kuwania nafasi za uongozi, ambapo yeye anatafuta nafasi ya ubunge Jimbo la Pandani kupitia ticket ya chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMA).
Mkasi ni mwanamke mpambanaji mwenye lengo la kutatua shida za wananchi kwenye Jimbo lake ili kupata maendeleo endelevu.
Anasema, ni miaka mingi sasa imepita ingawa wabunge waliokuwepo hawakufanya chochote kwenye Jimbo lao, hali ambayo ilimfanya achukue fomu haraka ili awatatulie wananchi kero zilizopo.
Mgombea huyo anasema, iwapo atafanikiwa kupata nafasi hiyo ya ubunge atawasaidia wananchi mmoja mmoja, familia na kutatua changamoto zilizomo kwenye vijiji vya Jimbo lao.
"Zinapotokea shughuli za kijamii kama vile msiba na harusi basi nitoa mchango kwani familia zetu nyingi ni masikini, hivyo nitawasaidia ili ziwawezeshe," anaeleza mgombea huyo.
Mkasi anasema, atawaweka watu maalumu ambao wataibua changamoto zote za Jimbo ambao watashirikiana bega kwa bega na wananchi, hiyo itasaidia kupata changamoto zote na kuweza kuzifanyia kazi.
"Hata wakati nitakapokuwepo bungeni basi shughuli za kuibua kero zitaendelea na watanifikishia ili nipate kuzitetea na nikija mwenyewe tutashirikiana kuziibua, lengo ni kupata maendeleo ya haraka," anaeleza.
Anaeleza kuwa, wananchi watarajie mazuri kwani atahakikisha anafikisha maendeleo kila sekta, ili wananchi wajisikie kwamba wamepata mtetezi wa Jimbo lao.
Anawaomba wananchi wa Jimbo la Pandani wamuunge mkono na wamchague, kwani amepania kuwatatulia changamoto zilizomo kwenye Jimbo na kuwafikishia maendeleo.
"Tumeona hapa miaka mingi imepita lakini tukiwa na tatizo hata tuwaite mwakilishi na mbunge basi wanatupuuza na hawatekelezi, wala hawapokei hata simu zetu, hivyo nichagueni mimi mupate maendeleo," anasema.
Mgombea huyo anasema, kwa upande wa wananchi hajapata changamoto yeyote, ambapo wanamuunga mkono na kumtaka asimame imara kulitetea Jimbo.
Anafafanua kuwa, changamoto iliyomkwaza ni kukosa ruzuku, hali iliyomsababisha afanye kampeni ya nyumba kwa nyumba.
"Nimefanya kampeni ya nyumba kwa nyumba, ingawa ni ngumu sana lakini kwa vile nimedhamiria nikasema ni mwiko kukata tamaa," anaeleza dada huyo.
Mgombea huyo hakushawishiwa kugombea nafasi ya ubunge, ingawa alipoona viongozi wa Jimbo waliokuwepo hawakufanya kitu, ndipo alipoamua kuingia ulingoni kwenye kinyang'anyiro cha kugombea.
Safari yake ya uongozi mgombea huyo ilianza pale tu alipojiunga na chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) mwaka 2010 na kubahatika kuwa Mwenyekiti wa akinamama Jimbo la Pandani na baadae kuwa Mwenyekiti wa akinamama Wilaya ya Wete, nafasi ambazo aligombea na kuibuka mshindi.
Anasema, baada ya kuona Chadema hakikushiriki kwenye uchaguzi ndipo alipoona aingie kwenye chama cha CHAUMA, ili aweze kutelekeza lengo lake alilojiwekea.
"Nimeshazoea harakati za huku na kule, hivyo sikuweza kustahamili, nikaona nijiunge na CHAUMA nipate kuwaletea maendeleo wananchi wa Jimbo langu," anasema.
Anahadithia, baada ya kujiunga na CHAUMA, alipata nafasi ya Mwenyekiti wa Jimbo la Pandani, ambapo anaendelea na nafasi hiyo.
Mume wa mgombea huyo, Omar Khamis Mohamed anasema, katika familia wanamuunga mkono mgombea huyo ili atekeleze majukumu yake vizuri.
Anasema, anaamini kuwa Jimbo hilo atalitumikia vizuri iwapo wananchi watamchagua, kwani ameshaona kasoro za viongozi wa Jimbo waliopita kwamba, hawakutekeleza ahadi zao walizoziweka.
"Tunamuumga mkono na tunaamini kwamba yeye atakuwa tofauti na waliopita na hasa kwa vile ameshaona ile kasoro yao, mgombea huyu ni mkakamavu na anaweza kuleta maendeleo ya haraka," anasema.
Alimtaka atekeleze ahadi ipasavyo iwapo atabahatika kuibuka mshindi wa nafasi hiyo, kwani atakapogeuka itakuwa amefanya vibaya na hatokuwa mfano mzuri kwa jamii.
Naibu Katibu Mkuu wa CHAUMA Zanzibar Mohamed Massoud Rashid anasema, mara hii wamewaingiza wanawake wengi kwenye mchakato wa kugombea uongozi Zanzibar na Tanzania Bara, kwani wanaamini watafanya vizuri kwenye majimbo yao na kutekeleza vyema ilani ya chama chao.
Anasema, atakapopata nafasi kuingia kwenye uongozi akasimamie maamuzi ya viongozi wao pamoja na kutekeleza masuala mbali mbali ya kimaendeleo kwenye sekta zote.
"Watakapofanikiwa kuwa viongozi, tunawataka warudi majimboni kwa wananchi waliowachagua na kuchukua kero zao kwa ajili ya kuzifikisha kwenye vyombo vya maamuzi," anaeleza.
Mgombea huyo ameolewa na ana watoto sita, ambapo ana elimu ya kidato cha tatu aliyoipata katika skuli ya Pandani Wilaya ya Wete.
MWISHO.

Comments
Post a Comment