NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@
MKUU wa wilaya ya Micheweni Pemba, Khatib Juma Mjaja,
amewatakia kheir na amani wananchi wa wilaya hiyo, kuelekea zoezi la
kidemokrasia, la kuwachagua wagombea wa urais, ubunge, uwakilishi na udiwani.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa njia ya simu, alisema
zoezi hilo, lipo kwa mujibu wa sheria na kanuni, hivyo kwake yeye, ni kuwatakia
kheir wananchi hao.
Aliwataka wananchi hao, kuziacha nyumbani jazba, hasira, uchungu
na chuki na badala yake, waliendee zoezi hilo, wakiwa na furaha na amani moyoni
mwao.
Mkuu huyo wa wilaya alieleza kuwa, zoezi la upigaji wa kura sio
jambo geni kwa wananchi wa wilaya hiyo, sasa ni vyema wakaliendea kwa upole na
shauku, huku ulinzi ukiimarishwa.
Alifafanua kuwa, kwa vile Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar na ile
ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ‘INEC’
imeshateua wasimamizi, zoezi hilo litakuwa jepesi.
‘’Niwaombea sana wananchi wa wilaya ya Micheweni, wale wenye
sifa, kwanza kujitokeza kwa wingi kupiga kura, tena iwe kwa amani na utulivu, maana
ndio moja ya sifa ya wananchi hao,’’alifafanua.
Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa wilaya ya Micheweni Khatib
Juma Mjaja, aliwakumbusha wananchi, kuwa wanaowajibu wa kulinda amani iliyopo.
Alieleza kuwa, taifa hili ni mali ya wananchi wenyewe, hivyo
hawanabudi, kushirikiana kwa karibu na vyombo vya ulinzi na usalama,
kuhakikisha amani inadumu.
‘’Kila mmoja leo ni shahidi, kuwa yapo mataifa kama ya Sudan,
Congo, Libya, Ukrein na Urusi, sasa hayakaliki, kutokana na amani kuchafuliwa,’’alifafanua.
Hata hivyo, aliwakumbusha watendaji wa Tume za uchaguzi,
kufika mapema vituoni, na kuanza kazi kwa mujibu wa taratibu, ili wananchi
wenye sifa, wapige kura na kurudi nyumbani.
Mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya ADA-TADEA Juma Ali
Khatib, akizungumza kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika Konde, aliwakumbusha wananchi,
kulinda amani.
Alisema, tunu ya kwanza kwa taifa la Tanzania, ni uwepo kwa
amani na utulivu, jambo ambalo kama ikipotea, hakuna chama, wala kiongozi wa
dini, atakaehubiri.
‘’Kwanza wakati tukielekea kwenye uchaguzi mkuu wa saba wa vyama
vingi nchini Tanzania, kila mmoja awe mwalimu kwa mwenzake, juu ya kuilinda na
kuienzi amani iliyopo,’’alifafanua.
Mapema Mkuu wa mkoa wa kaskazini Pemba Salama Mbarouk Khatib,
aliwataka wananchi, kuondoa woga na kujitokeza katika zoezi la upigaji wa kura.
Mwisho
Comments
Post a Comment