NA ZUHURA JUMA, PEMBA@@@@
WAGOMBEA kisiwani Pemba wamesema, changamoto yao kubwa inayowakumba katika kipindi hiki cha kutangaza sera zao ni ukosefu wa ruzuku ambayo inasababisha kutokufanya mikutano ya kampeni ambayo wamepangiwa kuifanya.
Walisema, mikutano ya kampeni ndio inayowatangaza kuwa wao ni wagombea, kwani hunadi sera zao ambazo ndizo zinazowafanya wananchi kuwachagua, hivyo kukosa ruzuku imesababisha wafanye kampeni nyumba kwa nyumba, jambo ambalo ni vigumu kuzimaliza nyumba zote kwenye Jimbo.
Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi, wagombea hao wanasema, ruzuku ni muhimu kwao katika kuendesha mikutano yao ya kampeni ambayo wanajitangaza kwa lengo la kupata nafasi ya kuwa kunadi.
Mgombea uwakilishi Jimbo la Wawi kupitia chama cha Wakulima AFP, Farida Juma Khamis alisema, ukosefu ruzuku ni changamoto kubwa iliyomkabili, ambayo inaweza kurudisha nyuma lengo lake.
"Kwa vile nilikuwa na nia niliongozana na mgombea urais kila anapokwenda, hivyo ilikuwa nanadi sera zangu na nashkuru nimekosa mkutano mmoja tu kati ya niliyopangiwa kuifanya," alieleza mgombea huyo.
Kwa upande wake mgombea uwakilishi Jimbo la Kojani kupitia chama cha ADA TADEA Maryam Msanif Ali alisema, amelazimika kufanya kampeni ya nyumba kwa nyumba ili kuomba kura kwa wananchi.
"Nilisema hata ikiwa sina pesa basi, nipite kwa wananchi wa Jimbo langu, iliningharimu lakini nilisema kwa vile natafuta basi ni mwiko kukata tamaa," alifafanua Maryam.
Nae mgombea ubunge Jimbo la Pandani kupitia chama cha Chauma, Mkasi Ali Hamad alisema ametumia nguvu zake mwenyewe kuhakikisha anafanikiwa kuingia bungeni kwa ajili ya kutatua changamoto za Jimbo lake.
"Ingawa ni shida kumaliza nyumba zote lakini kwa jitihada zangu nimezimaliza na nina matumaini nitashinda nafasi ya ubunge, nawaomba wananchi wazidishe imani kwangu," alisema.
Mwenyekiti wa ADA TADEA Wilaya ya Wete Mohamed Khamis Hamad alisema, ukosefu wa ruzuku unawakazwa sana wagombea, jambo ambalo linaweza kuwafelisha.
"Hii hali inaumiza sana wagombea, kwa sababu tumefanya mkutano mmoja tu wa kuwanadi wagombea ubunge, uwakilishi na udiwani, hivyo wamelazimika kufanya kampeni ya nyumba kwa nyumba na sihaba tumefanikiwa kumaliza nyumba zote," alifahamisha.
Salma Khamis Tumu mgombea uwakilishi Jimbo la Tumbe kupitia chama cha Mapinduzi CCM amekishikuru sana chama chake kwa kumpatia fedha ambazo zimemsaidia kufanya mikutano yake ya kampeni na shughuli nyengine zinazohusiana na uchaguzi.
"Ingawa tulichelewa kupata fedha lakini hapo tulipoingiziwa tuliendelea kufanya kampeni vizuri na nashkuru zimeniwezesha sana, hivyo nawaomba wananchi wanichague ili niwaletee maendeleo katika Jimbo letu," alisema mgombea huyo.
Mkurugenzi wa chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Zanzibar, Dk. Mzuri Issa alieleza kuwa, wanawake ni kundi maalumu ambalo kwa miaka mingi limeachwa nyuma, ambapo walivishauri vyama vyote viwe na sera ya kijinsia ambayo wataitekeleza ipasavyo na sio kuwepo tu.
"Moja kati ya jambo muhimu ni kuwatambua wanawake ambao wanahitaji uongozi na kuwapa hizo nafasi na jengine ni kuwapa mashirikiano ya hali na mali, ili kuweza kutekeleza mambo ya ya uongozi vizuri," anafafanua.
Dk. Mzuri alisema, ikiwa wagombea hao hawakupata ruzuku hiyo ni bahati mbaya sana na ni mapungufu makubwa kwa vyama vya siasa, kwani walivishauri mwanzo kwa vile vyama vinavyopata ruzuku viweke fungu maalumu na ambavyo havipati vijue kwamba hilo jambo lipo na vianze kutafuta fedha mapema kuhakikisha wanawake hawapati shida kutokana na fedha.
Msajili Msaidizi vyama vya siasa Sisty Nyahoza alisema, chama chenye usajili kamili kina haki ya kupata ruzuku endapo kina mbunge au diwani wa kuchaguliwa na kimetimiza masharti ya kupata ruzuku, yaliyopo katika sheria ya vyama vya siasa ya mwaka 1992 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2024.
"Mfano kuwa na akaunti ya benki (kifungu cha 15(2), hesabu zake kukaguliwa na CAG (kifungu cha 14 (1) (b) (i) ) na kutumia fedha za ruzuku kwa mujibu wa sheria ya vyama vya siasa inavyoelekeza (kifungu cha 18)," anaeleza.
MWISHO.

Comments
Post a Comment