JESHI la Polisi mkoa wa kusini Pemba,
limewataka wananchi wote wenye sifa ya kupiga kura, kujitokeza kwa wingi Oktoba
29, mwaka huu, kutumia haki yao ya kidemokrasia, huku ulinzi ukiimarishwa.
Kauli hiyo imetolewa jana na Kamanda wa Polisi mkoani humo,
Abdalla Hussein Mussa, ofisini kwake Madungu Chake chake, wakati akizungumza na
waandishi wa habari, juu ya namna jeshi
hilo, lililivyojipanda na ulinzi.
Alisema, Jeshi hilo lipo kwa mujibu wa kanuni na sheria za
nchi, na likiendelea kuwalinda raia na mali zao, hivyo kwa wananachi wasiwe na
hofu, kwa siku kupiga kura.
Alieleza kuwa, tayari limeshajipanga kila eneo la mkoa huo
na mipaka yake, ili kuwapa nafasi wenye sifa za kupiga kura kufanya hivyo, bila
ya vitisho vyovyote.
Kamanda huyo alieleza kuwa, haiwezekani hata kidogo kujitokeza
kwa kundi la wananchi, kutaka kuwazuia wenzao wasitekeleza haki hiyo, ndani ya
mkoa huo.
‘’Niwaombe wananchi wote wa mkoa wa kusini Pemba, kwanza kuondoa
hofu na usalama wao, na jingine kila mwenye sifa ya kupiga kura, aende kwenye
kituo chake, bila ya wasiwasi,’’alifafanua.
Aidha Kamanda huyo wa Polisi mkoa wa kusini Pemba, Abdalla
Hussein Mussa, alieleza kuwa, jeshi hilo halipo kwa ajili ya kumuonea mtu
yeyote, bali linafanyakazi kwa mujibu wa sheria na kanuni.
‘’Kwa mwananchi ambae ana sifa kama atatoka kwenda kituoni
kupiga kura kwa amani, na kukaa kwenye foleni kwa usalama, hatoulizwa na Jeshi
la Polisi,’’alisema.
Katika hatua nyingine, Kamanda huyo wa Polisi, aliwaasa wananchi
au vikundi vya watu, waliojipanga kutaka kufanya vurugu, wahakikishe
watakumbana na mkono wa sheria.
‘’Ikiwa mwananchi anajiamini na anauwezo wa kupambana na vyombo
vya ulinzi na usalama, ajaribu kutaka kulichafua zoezi la upigaji kura, anaweza
kujutia,’’alifafanua.
Hata hivyo, aliwakumbusha wananchi, mara wamalizapo zoezi
la kupiga kura, kurudi kwenye makaazi yao, na wenye mamlaka wataendelea zoezi
la kura.
Mapema Mkuu wa Mkoa wa kusini Pemba Rashid Hadid Rashid,
aliendelea kuwasisitiza wananchi, juu ya kuilinda amani iliyopo, kabla, wakati na
baada ya uchaguzi.
Mkuu wa wilaya ya Mkoani Miza Hassan Faki, aliwakumbusha
vijana, kutokubali kutumiwa vibaya, na baadhi ya watu, wasiowatakia mema.
Akizungumza kwenye kongamano la amani, lililofanyika umoja
ni nguvu Mkoani, alisema wapo baadhi ya watu, wanakusudia kuwatumia vibaya
vijana kwa lengo la kuharibu amani.
Sheikh Said Ahmad, kutoka ofisi ya Mufti Pemba akizungumza
kwenye kongamano, lililofanyika ukumbi wa Kiwanda cha Makonyo Wawi, aliwatadharisha
wanasiasa, kutotumia lugha za kebehi.
Wananchi wa Mkoani, akiwemo Omar Haji Mbwana na Hamada Ussi
Makame wa Mwambe, waliliomba Jeshi la Polisi, kuimarisha amani karibu na vituo
vya kupigia kura.
Hidaya Mjaka Ali mwenye ulemavu wa viungo, alisema athari
ya vurugu zinapotokezea, waathrika wakubwa ni wao na watoto, kisha ndio jamii.
Zoezi la upiga kura kwa wagombea urais, ubunge, uwakilishi
na udiwani kwa nchi nzima, linatarajiwa kufanyika Oktoba 29, mwaka huu.
Mwisho


Comments
Post a Comment