NA ZUHURA JUMA, PEMBA@@@@
TUKUMBUKE kwamba, zamani
nafasi ya mwanamke haikuikuwa ikionekana na kusababisha kuwekwa nyuma na kukosa
fursa mbali mbali ambazo zingemsaidia kutatua yale ambayo yanawakwaza wanawake
katika jamii.
Wakati
dunia na mabadiliko, ilionekana mwanamke hukosa yale yote ambayo anastahiki
kuyapata, kwa kukosa elimu, pamoja na tamaduni zilizokuwa zikiendelea siku hadi
siku.
Na
vilionekana vikwazo mbali mbali vilivyokuwa vikiwakuta wanawake na kukosa hata
kushirikishwa katika ngazi mbali mbali za maamuzi.
Ingawa
sasa yanaonekana mabadiliko makubwa katika jamii na kuamini kwamba mwanamke
anaweza kushika nafasi mbali mbali za uongozi sawa na mwanamme.
Ali
Hamad sheha mkaazi wa Micheweni anasema, ushirikishwaji wa wanawake upo kwa
kiasi, kwani zinapotokea nafasi wanashirikishwa ingawa kwenye upigaji wa kura
wanawake hawana ushirikiano, hali inayomfanya akose nafasi.
Anasema,
wanawake wakishirikiana wanayo nafasi kubwa ya kumfanya mwanamke mwenzako
afanikiwe, ingawa bado hawajawa tayari, jambo ambalo linawakatisha tamaa baadhi
yao.
"Lakini
mimi naona ni ubinafsi walionao wanawake kwa sababu bado hawajawa tayari kuwepo
kwenye vyombo vya maamuzi," anasema.
Anasema,
kwa vile elimu imeenea katika jamii na wamejitokeza wengi kugombea, iliyobaki
ni nafasi ya wananchi sasa kuwachagua viongozi wanawake kwaji ya maendeleo
endelevu.
Asha
Makame Haji anaeleza, wanahitaji kupeana elimu ya kuwawezesha wanawake wenye
nia ya kugombea uongozi na wawape ushirikiano ili wajivunie kuwa ile nafasi
anayo mwanamke.
Anasema,
ikiwa sehemu hakuna mwanamke basi kunakuwa na mapungufu makubwa, kwa sababu
mwanamke anafanya kazi nyingi na ngumu kuliko mwanamme, hivyo kunakuwa na
mafanikio ya haraka.
"Nimewahi
kufanya utafiti kwenye nyumba nikaona kwamba majukumu ya mwanamke ni mengi
zaidi ya kila siku na anaweza kufika saa nne usiku bado hajapumzika anaendelea
na kazi zake, lakini mwanamme anaenda zake maskani kucheza bao na mambo
mengine," anaeleza.
Anasema,
kwa hiyo wanapaswa kuwashirikisha katika nafasi za uongozi, ili kuhakikisha
wanamkomboa mwanamke na utegemezi, kwani wanapokuwa tegemezi mara nyingi hawana
maamuzi wala hafikii mbali kwa sababu kila kitu anachokihitaji mpaka aombe kwa
mume wake.
Fatma
Hassan Ali mkaazi wa Wingwi anafafanua kuwa, mwanamke anatakiwa na yeye amiliki
mali, awe na uhuru wa maamuzi.
Ingawa
kuna mambo lazima itakuwa yapo chini ya mumewe na mengine anatakiwa sauti yake
mwenyewe, vyenginevyo atakuwa ananyimwa fursa na kudumaza maendeleo yao.
"Lakini
pia kwa nafasi za kugombea, wenyewe tunakandamizana hivyo nawanasihi waache
tabia hiyo, kwani wanawake tuna uwezo wa kutetea, hivyo tuwaunge mkono ili
wafanikiwe kuwa viongozi," anasisitiza.
Fatma
anafafanua, suala la kukandamizana, kupigana na kuumiza vichwa kwamba mwanamke
asipewe nafasi ni choyo cha kibinadamu na ni tabia mbaya, inayosababisha
wasifike mbali.
Khamis
Hamad mkaazi wa Ole anasema, ni vyema mwanamke ashirikishwe kwa sababu kuna baadhi
ya sekta ni lazima awekwe mwanamke, ikiwa ni pamoja na hospitalini kwani wakati
mwengine wanashindwa kuelezea vizuri yanayomsibu anapomkuta mwanamme.
Anasema,
bado kuna watu wana itikadi za zamani kwamba mwanamke ana wajibu wa kulea
watoto tu, ingawa hayo ni mawazo finyu kwani kwa mtu mwenye uelewa wa kina basi
anaamini kwamba mwanamke anaweza kushiriki na kushirikishwa katika mambo ya
kimaendeleo.
"Tukizingatia
kwamba mwanamke au mtoto wa kike anahitaji kuandaliwa mapema kushika nafasi ya
uongozi tangu ngazi ya chini, lakini miaka ya sasa watu wengi wameshapata uelewa
na ndio maana wameingia wingi majimboni," anaeleza
WAGOMBEA WANAWAKE
Mgombea
uwakilishi Jimbo la Tumbe kupitia chama cha Mapinduzi CCM Salma Khamis Tumu
anasema, ameamua kugombea nafasi ya uwakilishi ili awafikishie wananchi huduma
bora za kijamii na kiuchumi.
"Lengo
langu ni kuwafikishia maendeleo wananchi wa Jimbo langu ili tuwe na maendeleo
endelevu, hivyo nawaomba wananchi waniamini na wanichague, changamoto zote
zitaondoka,’’ anaeleza.
Farida
Juma Khamis mgombea uwakilishi Jimbo la Wawi kupitia chama cha Wakulima AFP
anaeleza kuwa, wanawake wanaweza iwapo watapewa nafasi ya kuongoza, hivyo
atahakikisha Jimbo lake linakuwa la mfano katika kulipatia maendeleo.
"Ikiwa
nitafanikiwa kupata uwakilishi basi vijana watapata ajira na wanawake
wataimarika kiuchumi, kwani nitawatafutia miradi mbali mbali kwa ajili ya
kujipatia kipato," anafafanua.
Mgombea
udiwani Wadi ya Ole kupitia chama cha Mapinduzi CCM Mtumwa Suleiman Salum anasema,
sasa wananchi wamepata uelewa wa kutosha kwani, wanawaunga mkono wagombea wanawake
na wanajua kuwa wanawake ni wenye kuleta mabadiliko kwenye majimbo.
‘’Mwaka
huu ni tofauti na miaka iliyopita nyuma kwa sababu, wananchi wanatuunga mkono
na ndio maana tumehamasika zaidi kugombea, tunaamini watatuchagua kwa kishindo,’’
anaeleza.
Khadija
Anuwar ambae ni mgombea uwakilishi Jimbo la Wawi kupitia chama cha ACT
Wazalendo anaeleza, zamani jamii ilikuwa ikiwakatisha tamaa wanawake wengi
wanapohitaji uongozi, ingawa baada ya kupatiwa elimu wameelewa na kwa sasa
wanawaunga mkono.
"Nguvu
ya wananchi kuwakubali wanawake kuwa viongozi ndio iliyotufikisha hapa, kwa
sababu wameelewa kuwa mwanamke anaweza kuleta maendeleo ya haraka, kwa kweli
tunajivunia na tumezidi kujiamini," anasema.
Mgombea
uwakilishi Jimbo la Kojani Mwanaidi Hamad Rashid anasema, kila anapopita
wanajamii wanampa pongezi kwa hatua aliyoichukua ya kugombea, kwani wanaamini
sasa wamepata mtetezi wa Jimbo lao.
‘’Kwa
kweli wananchi hawaniangushi na nategemea kushinda, lengo langu ni kuhakikisha
kero zote zilizopo nazitatua kwa kushirikiana na wananchi wangu,’’ anasema.
Mkasi
Ali Hamad ambae ni mgombea ubunge Jimbo la Pandani anasema, hakushawishiwa na
mtu kugombea nafasi hiyo bali alipoona jamii tayari inamkubali mwanamke, ndipo
alipoamua kujitosa jimboni.
‘’Viongozi
wa jimbo hili waliopita wote hawakufanya kitu na hii ilinishawishi nigombee ili
niwatatulie wananchi kero zao, hivyo naomba wanichague ili niwaletee mabadiliko
ya kimaendeleo,’’ anaeleza.
VIONGOZI WA VYAMA VYA SIASA
Katibu
wa CCM Jimbo la Tumbe Mohamed Mwewe Omar anasema, wanawake wanaweza kuleta
maendeleo ya haraka kwani ni waoga, hivyo wanatekeleza majukumu yao vizuri.
‘’Majimbo
mengi yanayosimamiwa na wanawake yamepata maendeleo makubwa, kwani wanatatua
kero kwa kushirikiana na wanajamii kuibua ili kuzifanyia kazi,’’ anasema.
Yussuf
Maulid Issa ambae ni Katibu Habari, Mawasiliano na Uenezi ACT Wazalendo
anasema, wanawake waliogombea wanapaswa kuungwa mkono ili watimize malengo yao
ya kutaka kuingia kwenye vyombo vya maamuzi kwa ajili ya kutetea mambo
yanayowahusu pamoja na kuwafikishia wananchi maendeleo kwenye majimbo yao.
Mgombea
urais chama cha Wakulima AFP Said Soud Said anasema, wanawapa ushirikiano
wanawake wanaogombea, ili kusudi watimize ndoto zao za kuwa viongozi kwenye
majimbo.
Anawataka
wagombea hao, watakapopata ridhaa ya kuongoza kwenye majimbo yao wahakikishe
wanarudi kwa wananchi kusikiliza kero na kuzitatua kwa wakati, kwani
wataaminika zaidi katika jamii.
Mwenyekiti
wa ADA TADEA Wilaya ya Wete, anawataka wagombea hao iwapo watabahatika
kuchaguliwa na kuingia kwenye vyombo vya maamuzi, wajitahidi kutekeleza ahadi
walizozitoa kwa wananchi kipindi cha kampeni.
‘’Wanawake
ni watendaji wazuri wa kazi, hivyo tunaamini watapita kwenye vijiji kuibu
changamoto na kuzifikisha sehemu husika kwa ajili ya kutatuliwa,’’ anaeleza.
TAMWA
Amina
Ahmed Mohamed ambae ni Kaimu Mratibu wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake
kwa upande wa Pemba, anasema TAMWA imekuwa ikitoa elimu kwa wananchi ili
waondokane na mawazo mgando kwamba mwanamke hawezi kuongoza na ndio maana mwaka
huu wamegombea wengi.
"Jamii
sasa imepata uwelewa na wamejua umuhimu wa mwanamke kuongoza kwa sababu
waliokaa majimboni wote wamefanya vizuri na maendeleo yanaonekana,"
anaeleza.
Kaimu
huyo anasema, pia wanawajengea uwezo wanawake wenye nia ya kugombea uongozi ili
wajiamini, wawe na ujasiri pamoja na kutekeleza yale ambayo wanayaahidi kwa
ajili ya kujenga Taifa lenye maendeleo.
Wagombea
hao ametekekeza haki yake ya kushiriki katika demokrasia na uongozi, kama
Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1964 ilivyoeleza kwenye kifungu cha 21 (2) na
kifungu cha 67 (1) cha Katiba hiyo kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2010.
MWISHO.



Comments
Post a Comment