NA SAMIRA ABDALLA, ZANZIBAR
UCHAGUZI mkuu wa mwaka 2025 unafanyika kesho,
na suala la ushirikishwaji kamili wa watu wenye ulemavu, linazidi kuwa muhimu.
Zanzibar, kama
sehemu nyingine ya dunia, imejitolea kuhakikisha haki za watu wenye ulemavu, zinalindwa
na kutekelezwa, ikiwemo haki yao ya kupiga kura na kugombea uongozi.
Makala haya yatafanya uchambuzi wa kina kuhusu
ushirikishwaji wao, kuelekea uchaguzi mkuu wa 2025.
Licha ya kuwa wengi wetu walikuwa wakifikiria kwamba watu
wenye ulemavu, hawana haki na wala hawafai kushiriki katika uchaguzi, jambo
ambalo sio sahihi.
Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, kama sheria mama,
inatoa msingi wa ulinzi wa haki za binadamu kwa raia wote kuanzia kifungu ch 11
hadi 25A.
Ingawa haitaji moja kwa moja watu wenye ulemavu,
inasisitiza usawa mbele ya sheria na kutobaguliwa kwa misingi yoyote.
Hata hivyo, sheria ya Watu Wenye Ulemavu ya Zanzibar nambari
8 ya mwaka 2022, inatoa mwelekeo mpana na wa kina zaidi kuhusu haki na
ushirikishwaji wao.
Sheria hii
inatambua haki ya kundi hilo, kushiriki kikamilifu katika maisha ya kisiasa na
umma, ikiwemo haki ya kupiga kura, kugombea na kushika nafasi za uongozi.
Tena sasa kifungu cha 17 cha sheria hiyo, kinazungumzia
haki ya kushiriki katika siasa na maisha ya umma.
Kikisisitiza kuwa, serikali na taasisi zake zitahakikisha
watu hao, wanaweza kushiriki kikamilifu katika michakato ya kisiasa na umma.
Zanzibar, kupitia Tanzania, imeridhia mkataba wa
Kimataifa wa Haki za Watu Wenye Ulemavu wa mwaka 2006, (CRPD).
Ambapo unatoa mwongozo wa kimataifa kuhusu jinsi nchi
zinapaswa kuhakikisha haki za watu wenye ulemavu, zinalindwa na kutekelezwa.
Ibara ya 29 mkataba huo, inazungumzia ushiriki katika
maisha ya kisiasa na umma, kikisisitiza haki yao ya kupiga kura na kugombea
katika uchaguzi.
ZEC INASEMAJE?
Mjumbe wa Tume ya uchaguzi Zanzibar ZEC, Awadh A. Said
amesema, Ttume hiyo inalojukumu muhimu katika kuhakikisha uchaguzi huru na wa
haki.
Anabinisha kuwa, kuhakikisha ushirikishwaji wa makundi yote
ya jamii, wakiwemo watu wenye ulemavu.
Jingine muhimu kwa kundi hilo ni upatikanaji wa vituo vya
kupigia kura tena viwe rafiki, ambavyo vinafikiwa kwa urahisi.
Kamishna wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar Idrissa Haji
Jecha, amewataka watu wenye ulemavu kushiriki katika elimu ya mpiga kura na kuhudhuria
na kushiriki katika programu za elimu hiyo.
Kwa mujibu wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC)
watu wenye ulemavu wapatao 8,021 wanatarajiwa kushiriki katika uchaguzi mkuu
mwaka huu Zanzibar.
Ilifahamika kuwa, kati ya hao wapo viziwi 1,667
wenye ulemavu wa ngozi wakifikia 102 na wasioona 678.
WANASIASA WANAMAONI GANI
Mgombea uwakilishi wa jimbo la Mfenesini kwa tiketi ya CCM,
Machano Othman Said, amevitaka vyama vya siasa, kuhakikisha kuwa jukumu muhimu
katika kuhamasisha na kuwezesha ushirikishwaji watu wenye ulemavu.
Vyama hivi vinapaswa kujumuisha katika miundombinu yao
kwa kuhakikisha watu hao, wanawakilisha katika ngazi mbalimbali za uongozi kuanzia
kwenye vyama.
Akili au ubongo unaweza kufikiri kwa kuandaa sera zinazojali
watu wenye ulemavu, na kuunda na kutekeleza sera za vyama, zinazozingatia
mahitaji na haki zao.
Mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya ADC Hamad Rashid Mohamed, anakiri kuwa imekuwa vigumu wakati mwingine kuweka mazingira kamili kwa ajili ya watu wenye ulemavu.
WATU WENYE ULEMAVU WENYEWE
Aisha Rajab Ali mwenye uleamvu, amesema kuwa licha ya hatua zilizopigwa, bado kuna
changamoto kadhaa, katika ushirikishwaji wao, kuelekea uchaguzi mkuu wa 2025 kesho.
‘Kumbuka kuwa vikwazo vya kimazingira kwa baadhi ya vituo vya kupigia kura na maeneo ya
mikutano, bado hayafikika kwa urahisi kwetu,’’analalamikia.
Mratibu wa baraza la taifa la watu wenye ulemavu Pemba,
Mashavu Juma Mabrouk, anasema mazingira kwa kiasi yameimarishwa, ikilinganishwa
na chaguzi zilizopita.
Mwenyekiti wa
Juamuiya ya wasaioona Pemba Suleiman Mansour, anasema ijapokuwa zipo kura za
nukta nundu kwa ajili yao, lakini bado mazingira sio rafiki sana.
Kwa mfano, kwenye
kupiga kura ni hatua moja, lakini kufuatilia na kuzifahamu sera za wagombea wa
vyama vyote, ni jambo muhimu na la kwanza.
‘’Vyama bado
havijajipanga, kuona watu wenye uziwi nao wananufaika na uwasilishaji wa sera
zao, hivyo ni kusema mazingira hayakuwa rafiki sana kwetu,’’anafafanua.
WANAHARAKATI
Kaimu Mratibu wa TAMWA-Ofisi ya Pemba Amina Ahmed,
anasema hasa kundi la viziwi wamekuwa wakikosa sera za vyama, kwa kukosekana
wakalimani.
‘’Ni kweli tumekuwa tukipiga kelele kila uchao, ili
kuona wakati huu vyama vikinadi sera, zinakuwa sera jumuishi kwa wenzetu
hawa,’’anasema.
Mkataba wa
kimataifa wa haki za watu wenye ulemavu wa mwaka 2006 (CRPD), ibara ya 29 (a),
inazitaka nchi wanachama, kuhakikisha kuwa, watu wenye ulemavu wanashiriki
kikamilifu katika medani ya siasa.
Ukataba ukafafanua kuwa, tena iwe kwa misingi iliyo
sawa na wingine, ikiwa ni pamoja na fursa ya kuchangua na kuchaguliwa.
‘’Watu wenye ulemavu, wanatakiwa kuwekewa mazingira
sahihi ikiwemo kupata taarifa, ili kushiriki kikamilifu katika masuala ya umma
bila ya ubaguzi wowte,’’umefafanua mkataba huo.
Sheria ya watu wenye ulemavu Zanzibar nambari 8 ya
mwaka 2022, kifungu chake cha 29 kinaeleza umuhimu wa watu wenye ulemavu kuweza
kufikia miundo mbinu mbali mbali pamoja, taarifa mawasiliano na haki zote za
kibinaadamu za msingi.
Ikifafanua kuwa, suala la kuwepo kwa wakalimani
kumbe kwa mujibu wa kifungu hicho na kile cha 28 (1)(d), kinachofafanua suala
la kupata taarifa, ni jambo la lazima kwao.
Ndani ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 kifungu
cha 11 na 12, kikabainisha kuwa, usawa kwa binaadamu wote mbele ya sheria,
binaadamu wote huzaliwa kupata uhuru, anastashiki heshima ya kutambuliwa
kuthaminiwa utu wake wanayo haki bila ya ubaguzi wowote.
Hata kile cha 18, kinasisitiza haki ya kupokea,
kutoa na maoni ni haki ya kikatiba, ingawa haikuwataja watu wenye ulemavu,
ikijumuisha raia wote.
WANAJAMI
Fatma Ali Hamad, jamii anaeshiriki kwenye kampeni
za vyama vya siasa, anasema watu wenye ulemavu wa uziwi, bado hawajazingatiwa
mahitaji yao, katika kufikiwa na sera za vyama.
Issa Haji Mohamed, asema inawezekana vyama
havihitaji kura za viziwi ndio maana, vimekuwa vizito kuwawekea mkalimani
kwenye mikutano.
Mwanaisha Hassan Khamis, anasema sheria na mikataba
hazijawasahau watu wa kundi hilo, ingawa baadhi ya vyama bado ni changamoto.
VYAMA VYA SIASA VINAJIBU NINI
Katibu wa CCM mkoa wa kusini Pemba Kajore
Vyohoroko, anasema wamekuwa wakiwatumia wakalamani hasa wanapokuwa na wagombea
ngazi ya urais, kusudi viziwi wapate sera.
Maana Katiba ya chama hicho, ya mwaka 1977 toleo la
2007, linaeleza kua CCM, kinaamini kwamba watu wote ni sawa.
Mwenyekiti wa chama cha ACT –Wazalendo Mkoa wa
kusini Pemba Mohamed Abdallah anasema, hutumia watu wa karibu na viziwi, katika
kufikisha ujumbe uliokusudiwa.
Anasema kuwa, bado chama kinaupungufu wa wataalamu
wa lugha ya alama, hivyo inawawia vigumu kupata wataalamu wa kutosha wa
kuwatumia katika mikutano yao.
‘’Tutafanya
jitihada zetu ipasavyo kuhakikisha kundi hilo muhimu linapata ujumbe
unaokusudiwa,’’ anasema.
Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Alliance Afrika
Farmers Party (AAFP) Omar Juma Said, anasema bado wako nyuma hawajapata muamko
na elimu ya kuwafikia watu wenye ulemavu wa uziwi.
Anasema anajua kuwa, watu wenye ulemavu wana haki
za msingi ya kuchagua, kusikiliza pamoja na kupata taarifa, ingawa kwa sasa
suala la kuwapatia taarifa halijafanyika.
‘’Ni kweli watu wenye ulemavu wa uziwi
hatujawashirikisha katika kusikiliza ilani ya chama chetu, mikutano yote
tuloifanya hapakuwa na mkalimani wa lugha za alama,’’ anakiri.
Chausiku Khatib Mohammed ni Mgombea mwenza wa Urais
wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzani kwa tiketi ya NLD, anakiri kuwa,
hawajawashirikisha na wamesahau kama kuna watu wenye ulemavu wa uziwi.
‘’Kwa sisi tumesahau kabisa, kama kuna watu
wenye ulemavu wa uziwi, mpaka sasa hatujawashirikisha juu ya kusikiliza ilani
ya sera za chama chetu, na kura zao tunazihitaji,’’anafafanua.
Asha Said Suleiman ni Mgombea
Uwakilishi wa Jimbo la Mtambile Chama cha ADA-TADEA
anasema, hawajawashirikisha watu wenye ulemavu katika kunadi sera zao.
Anasema hata kama
wamepewa mafunzo na TAMWA juu ya ushirikishwaji wa watu wenye ulemavu, ingawa,
hushindwa kwa gharama ya mkalimani.
‘’Mkakati wetu ni kupita nyumba kwa nyumba,
kutangaza sera ya ilani ya chama chetu, kwa kila mwenye ulemavu wa uziwi, ili
wasaidizi wao waweze kuwasaidia,’’anasema.
TUME YA HAKI ZA BINAADAMU NA UTAWALA BORA
Suleiman Salim Ahmad ni Afisa Mfawidh Tume ya haki
za binaadamu na utawala bora Pemba, anasema ni kweli tume imegundua pengo lipo
hasa katika mikutano ya hadhara.
Anasema wamekuwa wakitoa mafunzo kwa vyombo vya
habari, ili kupeleka ujumbe juu ya haki za binadamu kwa kufanya makala vipindi
na hata habari.
MWISHO


Comments
Post a Comment