ZOEZI la upigaji wa kura ya mapema,
lililofanyika Zanzibar, kwa upande wa Pemba liliripotiwa kwenda kwa amani na
utulivu, katika vituo kadhaa, vilivyopangwa kufanyikwa kwa zeozi hilo, leo.
Waandishi wa habari walishuhudia vikosi
vya ulinzi na usalama, vikizunguruka katika miji, mitaa na vitongoji mbali
mbali, kisiwani humo.
Wakati zoezi hilo likiendelea kwa watu maalum,
wakiwemo walinzi wa amani na watendaji wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar ‘ZEC’,
wananchi katika miji ya Chake chake, Mkoani, Wete na Micheweni waliendelea na shuguli
zao.
Ilibainika kuwa, maandalizi ya zoezi hilo
lilofanyika leo Oktoba 28 yalifanyika kuanzia jana Oktoba 27, kwa watendaji,
wasimamizi na wasimamizi wasaidizi wa upigaji kura, kufunga vifaa kwa wakati.
Akizungumza na waandishi wa habari Mratibu wa ‘ZEC’
Pemba Ali Said Ali, alisema hadi leo majira ya saa 6:55 mchana, hakujaripotiwa tukio
lolote, lililozuia au kuashiria kuzuia zoezi hilo.
Alisema, watendaji walioteuliwa na ‘ZEC’,
wanaendelea kutekeleza kazi hiyo kisheria, na kila aliyepaswa kupiga kura ya
mapema, alifanikiwa.
‘’Kwa hakika lazima tuwapongeze wenzetu wa kamati za
ulinzi, maana zoezi hadi nazungumza na wewe, linakwenda vyema katika vituo
vilivyopangwa,’’alifafanua.
Hata hivyo, aliwasisitiza wananchi kisiwani humo,
kuendelea kuheshimu na kutii sheria kama zilivyo, ili uchaguzi wa mwaka huu, uwe
wa kihistoria kwa utunzaji wa amani.
Kamanda wa Polisi mkoa wa kusini Pemba, Abdalla
Hussein Mussa, alisema zoezi hilo liliripotiwa kuendelea kwa amani mkoani humo.
Alisema, vikosi vya ulinzi na usalama, vinaendelea
kuwalinda wananchi, na kuhakikisha hakuna mtu wala kikundi cha watu,
kitakachoharibu amani.
Alieleza kuwa, kura ya mapema ambayo ipo kisheria,
itaendelea na kumalizika kwa amani, kama ilivyopangwa.
‘’Niwashukuru wapiganaji kwa kuendelea kulinda
amani, hasa kwenye siku hii ya kura ya mapema, utulivu umetawala na twashukuru
mno,’’alifafanua.
Mkuu wa mkoa wa kaskazini Pemba Salama Mbarouk
Khatib, akitoa taarifa kwa waandishi wa habari ofisini kwake, majira ya saa 5:20 mchana alisema mkoa huo unaendelea
kutumia neema ya amani.
Alisema hakuna vitisho wala viashiria vya uvunjifu
wa amani ndani ya mkoa huo, wakati zoezi la upigaji wa kura ya awali,
likiendelea.
‘’Niwambie waandishi wa habari kuwa, mkoa wa kaskazini
Pemba, hali ya ulinzi na amani imeimarishwa, hivyo hadi nazungumza na nyinyi
hivi sasa, mkoa uko salama na umejaa amani,’’alisema.
Kwa upande wake, Mkuu wa wilaya ya Mkoani Miza
Hassan Faki, akizungumza na mwandishi wa habari hizi, alisema hadi majira ya
saa 5:15 wilaya hiyo ilikuwa shuwari.
‘’Kila dakika vyombo vya ulinzi vinanipa taarifa,
kuendelea kwa amani, na hakuna hata sehemu ambayo wananchi waliandamana,’’alifafanua.
Nae Mkuu wa wilaya ya Micheweni Khatib Juma Mjaja,
alikiri kuwa, bado wilaya yake ni shuwari, na hakuna taarifa zozote za uvunjifu
wa amani.
‘’Ni kweli leo kuliwepo kwa baadhi ya vituo
ambavyo, vilipigisha kura ya mapema, lakini hadi saa 7:30 hali imeripotiwa shuwari,’’alisema.
Mkuu wa mkoa wa kusini Pemba, Rashid Hadid Rashid alisema, hadi saa 5: 55 mchana wa leo, tayari alishavitembelea vituo saba, kikiwemo cha Gombani, Kwale, Kiwani, Ole,
Pujini, Chambani, na hali inaendelea vyema.
‘’Hapa nilipo sasa naelekea kitu chingine, na hivyo
ambavyo nimeshavitembelea, hali ni shuwari na hakuna vitisho, wala maandamano
yoyote,’’alisema.
Aidha, aliwakumbusha wananchi kuendelea kuilinda
amani na utulivu katika maeneo yao, ili zoezi la uchaguzi, limalizike kwa amani.
Baadhi ya wananchi waliviomba vyombo vya ulinzi na
usalama, kuendelea kulinda amani, hata katika uchaguzi wa wote, unaotarajiwa
kufanyika kesho.
Makame Iddi Makame wa Machomane, alisema kama leo wakati wa zoezi la upigaji kura ya mapema, umefanyika kwa amani, hakuna budi
kuendelea.
Msimu Haji Issa wa Madungu ambae ni mfanyabishara,
alisema aliendelea na bishara zake, kama vile hakuna jambo la kitaifa, kisiwani
Pemba.
Mwisho


Comments
Post a Comment