NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@
WANANCHI wa shehia ya Mgogoni wilaya ya Chake chake, wameliomba Jeshi la Polisi mkoa wa kusini Pemba, kuharakisha upelelezi wao, ili kumbaini mtu aliyedaiwa kumbaka na kisha kumuua mwanamke mmoja wa kijiji hicho mwenye miaka 55.
Wananchi hao walisema, kitendo alichitendewa mwananchi mwenzao, sio cha kiungwana na kinafaa kulaaniwa na kila mmoja, na kuliomba Jeshi la Polisi kuharakisha upelelezi wao.
Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi, walisema wanasikitishwa mno na mzazi mwenzao, kufanyiwa kitendo hicho na kisha mwili wake, ukiwa hauna nguo kutelekezwa kichakani.
Mmoja kati ya wananchi hao, Mohamed Juma Maalim, alisema kilichobakia kwa sasa pamoja na kushirikiana na Jeshi la Polisi, lakini wanalisubiri kuona upelelezi wao unazaa matunda gani.
“Ni kitendo kinachoumiza hadi ndani ya miili yetu, kuona mtu aliyefanya kitendo hicho, hakuishia tu kwenye kumdhalilisha kingono, lakini kisha kuondoa uhai wake,’’alisema.
Nae Khadija Mjaka Makame, alisema walikuwa wamezoeana mno na mama huyo kabla ya kufanyiwa unyama huo, ingawa kwa sasa wamekosa amani ndani ya mioyo yao.
‘’Amani mtaani kwetu imepotea, maana mzazi wetu aliyekuwa mshauri wetu mkuu, amefanyiwa unyama mara mbili, hivyo kwa sasa tunaliangalia Jeshi la Polisi na upelelezi wake,’’alisema.
Kwa upande wake Asha Muhsin Ameir, alisisitiza haja kwa Jeshi la Polisi, kuharakisha upelelezi wao, kwani kwa sasa wanashindwa hata kula na kunywa, kwa kuumwa na tukio hilo.
‘’Kwa sasa hatuna furaha hapa mtaani, maana tukio hili limetuumiza mno, kuona mama yetu huyu asiye na hatia amefanyiwa udhalilishaji na ukatili mkubwa,’’alifafanua.
Mapema Kamanda wa Polisi mkoa wa kusini Pemba, Abdalla Hussein, akiri kutokea kwa tukio hilo, na kusema tayari Jeshi la Polisi limeshaanza upelelezi wa kina.
Alisema, Jeshi litahakikisha kuwa, linawatia mikononi wahusika wa tukio hilo, na kisha kuwafikisha mbele ya vyombo vya sheria, kujibu madai hayo.
Alieleza kuwa, baada ya kupata taarifa ya tukio hilo, walifika eneo la tukio na kuona kuwa, marehemu huyo, hakuwa na hali nzuri, baada ya kufanyiwa ukatili.
‘’Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi wa matukio ya kihalifu ni sehemu ya wajibu wetu, na tukio la mama huyo kudaiwa kubakwa na kisha kuuliwa, tunaendelea kulifanyia kazi,’’alifafanua.
Katika hatua nyingine Kamanda huyo wa Polisi mkoa wa kusini Pemba, aliwataka wananchi kuwa watulivu katika kipindi hiki, wakiendelea na uchunguuzi wao.
‘’Kubwa tunaloomba kwa wananchi ni kuhakikisha, wanashirikiana kwa karibu na Jeshi la Polis, ikiwemo kutoa taarifa za siri, pindi wakihisi kuna mtu wanamdhania,’’alifafanua.
Baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo, walisema wakati wanakwenda kwenye shughuli zao za kawaida, waliona nguo za marehemu pembezoni mwa mto, katika eneo lisilo mbali na shamba lake.
Walisema, baadae waliposikia taarifa hizo, walirudi tena kushirikiana na wananchi wenzao, waliokuwa wakimtafuta, na kisha kuuona mwili wa marehemu, ukiwa kichana na hauna nguo.
‘’Eeneo alilofanyiwa udhalilishaji na ukatili mama huyu, ndio eneo hilo hilo, alilofanyiwa jaribio la kubakwa kwa mwanafunzi mmoja mkaazi wa Vikutani Wawi, wakati anakwenda skuli mwaka jana,’’alieleza shuhuda mmoja.
Mama huyo anaekisiwa kuwa na umri wa miaka 55, ni mkaazi wa shehia Mgogoni wilaya ya Chake chake, ambapo mwili wake ulipatikana kichakani, majira ya saa 7:00 mchana.
Matukio ya jinai, inaonesha ongezeko la makosa 32, 221 kutoka matukio 574,881 yaliyoripotiwa katika kipindi cha Januari hadi Disemba mwaka2022.
Ikilinganishwa na matukio 607,102 yaliyoripotiwa katika kipindi kama hicho kwa mwaka 2023, ripoti ya Jeshi la Polisi Tanzania ya mwaka 2023 inafafanua.
Ingawa ripoti hiyo ikafafanua kuwa, kati ya matukio hayo ya jinai, mwaka 2022 pekee, kuliripotiwa matukio 2,464 ya watu kuuliwa, na kuwepo punguzo la matukio 161, kwenye mwaka 2023, kati ya matukio 2, 303 waliouliwa kwa Tanzania nzima.
Hata hivyo, kwa upande wa matukio ya ubakaji, ripoti ikaelekeza kuwa, kwa Zanzibar yenye mikoa mitano, kuliripotiwa matukio 44 ya mauwaji na watu 927 waliripotiwa kubakwa.
Kwenye mkoa wa kusini Pemba, mwaka 2023 pekee kuliripotiwa watu wawili (2) waliouawa na 86 waliripotiwa kubakwa, ripoti hiyo ikazidi kufafanua.
Mwisho
Comments
Post a Comment