NA ZUHURA JABIRI, ZANZIBAR
ZANZIBAR, ni
kisiwa kinachojivunia amani, mshikamano wa kijamii na historia ndefu ya kuishi
pamoja.
Ingawa nyuma ya
taswira hii ya utulivu, kuna sura nyingine isiyoonekana mara nyingi sura ya
watu wenye ulemavu, wanaoendelea kusubiri usawa wa kweli.
Kwa mujibu wa
takwimu rasmi, Zanzibar ina watu 167,308 wenye ulemavu, sawa na asilimia 11.4
ya wananchi wake milioni 1.89.
Hata hivyo, katika meza ya maamuzi, katika ajira
rasmi, na hata katika huduma za msingi, kundi hilo, bado lipo pembeni.
Ijapokuwa sheria
ya Watu Wenye Ulemavu ya nambari 8 ya mwaka 2022, inahakikisha haki sawa katika
elimu, ajira, afya na ushiriki wa kisiasa.
Lakini kati ya
maandishi ya sheria na maisha ya kila siku, kuna pengo kubwa pengo linalowaacha
watu wenye ulemavu wakionekana, lakini hawasikiki.
“Nimejitolea
maisha yangu kupambana na ubaguzi dhidi ya watu wenye ulemavu na kuhakikisha hatusahauliki,”
anasema Salma Saadat, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake Wenye Ulemavu Zanzibar
(JUWAUZA).
Kwa miaka
mingi, Salma amekuwa mstari wa mbele katika harakati za kuunganisha sera na
uhalisia.
Kupitia
JUWAUZA, amefundisha wanawake wenye ulemavu, ujasiriamali na uongozi, akiwapa
zana za kuvunja mitazamo potofu inayowafanya waonekane dhaifu au wasio na
mchango.
“Sisi tuna
uwezo, na tunastahili kuwa katika kila nafasi ambako maamuzi yanafanyika,” anasisitiza.
Kauli yake
inaakisi kilio cha wengi kwamba tatizo si ukosefu wa vipaji, bali ni mifumo
isiyo rafiki kwa kundi la watu wenye ulemavu.
Muhtasari wa takwimu
za Zanzibar wa mwaka 2024 zinathibitisha hali hiyo, maana zaidi ya watoto
60,000 wenye ulemavu wako nje ya mfumo wa elimu.
Watu wazima
wenye ulemavu wanawakilishwa kwa kiwango kidogo sana katika ajira rasmi, chini
ya asilimia 2 katika sekta za umma na binafsi.
Wanawake wenye
ulemavu wanakumbwa na ubaguzi maradufu kwa misingi ya jinsia kwa ulemavu wao.
Kwa wazazi kama
Salma Hamadi Mwarabu, changamoto hizi si takwimu tu bali ni maisha halisi.
Kijana wake wa
kiume mwenye umri wa miaka 24 amekuwa na ulemavu wa miguu na kifafa tangu
utotoni, jambo ambalo kwa baadhi ya wakati huwa ni changamoto ya kukosa haki na
fursa.
“Kila mwaka natafuta programu au fursa kwa
ajili yake, lakini msaada hautoshi,’’anaeleza.
Hata huduma za
kawaida za tiba na urekebishaji ni vigumu kuzipata kama huna fedha.
Hadithi ya
Salma inaonyesha ukweli mpana wa mfumo unaowaacha watu wenye ulemavu na familia
zao wakihangaika.
Ajira ni
kikwazo kikubwa zaidi, akisema maana waliowengi hulazimika kujiajiri si kwa
sababu wamechagua, bali kwa sababu hawana chaguo jingine.
Nassor Juma
Nassor, mwenye ualbino, anakumbuka upweke aliokumbana nao akiwa mtoto huko
Maungani, Wilaya ya Magharibi.
Sasa akiwa na umri wa zaidi ya miaka 50,
anasema uzoefu wake shuleni ulimvunja moyo.
“Sikutendewa kama wingine, maana waalimu
hawakujua jinsi ya kunisaidia, wanafunzi hawakunielewa,’’anakumbuka.
“Watu wenye
ulemavu wana vipaji, ingawa hufifilizwa na jamii na wasisimamizi wa sera, kwa
kule kutowapa haki na fursa zao,” anasisitiza.
Na ndio maana tasisi kama Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania TAMWA-Zazibar inaendelea kuwatafuta wafadhili, ili kuwajengea uwezo waandishi wa habari, kuibua changamoto za watu wenye ulemavu.
Akifungua moja ya mafunzo hayo, Mkurugenzi wa TAMWA-Zanzibar Dk. Mzuri Issa Ali, anasema waligundua watu wenye ulemavu, mafanikio na juhusi zao zao hazitangaazwi na vyombo vya habari.
''Ukisikia taarifa ya watu wenye ulemavu, aidha amebakwa, amedhalilishwa ama amefukuzwa kazi, laki kazi zao na mafanikio husikii sana,''anasema.
Kwa mujibu wa
Hija Shamte, Afisa Mawasiliano wa Shirikisho la Watu Wenye Ulemavu Zanzibar
(SHIJUWAZA), anasema tatizo hili ni la kimuundo.
“Sera zipo ndiyo,
lakini utekelezaji ni wa kusuasua na huwapa mazingira magumu mara mbili kundi
la watu wenye ulemavu,” anasema.
Anasema majengo
mingi ya umma na sehemu za kazi, bado hayana miundombinu rafiki kwa watu wenye
ulemavu, ingawa sera na sheria zinalazimisha hilo.
Anaona taratibu za kuajiri mara chache
huzingatia kundi hilo, kama vile wanalazimishwa tu na sio kwa utekelezaji wa
sheria.
Anafafanua kuwa,
pengo la ajira na uongozi bado ni kubwa, akitolea mfano kuwa, katika majimbo
yote ya uchaguzi ni jimbo moja la Ziwani Pemba, linanaoongozwa na mtu mwenye
ulemavu.
Ukosefu huu wa
uwakilishi unaendeleza mzunguko wa kutengwa kuanzia maamuzi hadi ugawaji wa
rasilimali.
Katika ngazi ya
jamii, athari zake zinaonekana wazi, kama anavyosema Naila Mohamed, Mwalimu
kutoka Jendele, Wilaya ya Kati.
Anasema licha
ya kauli mbiu za ujumuishi, uhalisia ni tofauti, maana watunga sera na watoa
maamuzi bado wamezingiriwa na ubinafsi.
Mratibu wa Baraza
la taifa la watu wenye ulemavu ofisi ya Pemba, Mashavu Juma Mabrouk, anasema mashirika
ya kijamii, vikundi vya watu wenye ulemavu, na wanaharakati wanaendelea kuziba
mapengo yaliyoachwa na mfumo.
Lakini juhudi
hizi haziwezi kuchukua nafasi ya dhamira ya serikali na jamii kwa ujumla, kama
mifumo hiyo haikukaziwa Kamba na serikali kuu.
“Matumaini
yangu ni kuona watu wenye ulemavu wakijumuishwa, kikamilifu katika kila nyanja
ya maisha,” anasema.
Zanzibar ina
kila sababu ya kuwa mfano wa ujumuishi katika ukanda huu, ingawa hadi pale
ambapo mtoto mwenye ulemavu, atapata elimu bila vikwazo na kuingiwa kwenye
mifumo ya ajira.
Katika kisiwa
kinachojivunia amani na mshikamano, swali linabaki, ikiwa je, amani hiyo
itakuwa kamili bila ya kuwepo kwa mifumo jumishi.
Mashavu anaendelea
kuhoji, kwamba watu wenye ulemavu wapo, wana sauti, na wana mchango mkubwa wa
kutoa, ingawa mifumo thabiti na isiyo na kikwazo kama inawezekana.
Kilichobaki ni
jamii na mifumo kuamua je, wako tayari kuwasikiliza na kuwapa nafasi
wanayostahili.
Changamoto nyingine
kubwa inayowakabili watu wenye ulemavu Zanzibar ni mtazamo wa kijamii, kwa kule
kuwaona hawana mchango wowote.
Katika jamii
nyingi, ulemavu bado hutazamwa kama mkosi, laana, au jambo la kufichwa na wakati
mwingine hata kukosa haki za msingi ikiwemo aelimu.
Mtazamo huu
huanza nyumbani, huendelea shuleni, na hatimaye hujikita katika taasisi za umma
na hasa mifumo ya kiajira na fursa za uongozi.
Mkuu wa mkoa wa
kaskazini Pemba Mgeni Khatib Yahya anasema, mtoto mwenye ulemavu anapokosa
kupelekwa shule si kwa sababu hana uwezo wa kujifunza, bali kwa sababu wazazi
au walezi huamini.
Anasema hii ni
aina ya unyanyasaji wa kimnya kimnya unaonyima kizazi kizima haki ya kuota
ndoto.
Akifafanua kuwa,
suala ujumuishi kwa kundi la watu wenye ulemavu, sio jukumu la serikali tu,
bali inapendezea ikianzia ngazi ya familia.
Anasisitiza
kuwa, ni wajibu wa jamii nzima kuanzia familia, taasisi za elimu, waajiri,
viongozi wa dini hadi vyombo vya habari, katika kulifanikisha hili.
Mtoto Daudi
Hija Hassan mkaazi wa Mwembeladu Unguja, mwenye ulemavu wa uoni, anasema kama
ujumuishi haukuanzia ngazi ya familia, kusitarajiwe mabadiliko serikali kuu.
Sheikh Hassan
Omar Kassim wa Chake chake anasema Imani na mitazamo ya dini, ikiwa imejaa
kiroho, yengetosha kuhakikisha kila mtu anapata haki yake.
Eneo la Mkataba
wa Kimataifa wa watu wenye ulemavu wa mwaka 2016, kwenye ibara zake za 34
inazitaka nchi wanachama, kuanzisha kamati za kutetea haki za watu wenye ulemavu.
Ibara ya 27, yenye
ikasisitiza suala la kuwaajiri watu wenye ulemavu, wakiwa ni sehemu ya jamii.
Mwisho





Comments
Post a Comment