Skip to main content

WAANDISHI WA HABARI 272, VYOMBO VYA HABARI 94 VYAKUMBWA NA MADHILA TANZANIA

 



Ikiwa ni miaka 30 tangu Mei 3 ya kila mwaka ilipotangazwa kuwa siku rasmi ya kuadhimisha Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani (WPFD) na Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UNGA) mwaka 1993, matukio mengi ya madhila dhidi ya uhuru wa waandishi na vyombo vya habari hapa nchini yameendelea kutotolewa taarifa.

Waandishi wa habari wamechukulia kukumbana na madhila kama unyanyaswaji, kupigwa, kunyang’anywa vifaa, na kutishiwa kama ‘ajali kazini’ na hivyo kutoyatolea taarifa. Msukumo wa taarifa umekuwa ukiwekwa kwenye matukio makubwa yanayohusisha kujeruhiwa, kutekwa ama kupoteza maisha; hivyo taarifa nyingi za madhila hazipo kwenye kumbukumbu.

 

Uanzishwaji wa Kanzidata na Malengo yake

Kutokana na changamoto hii, mwanzoni mwa mwaka 2012 Baraza la Habari Tanzania (MCT) lilianzisha kanzidata ya kitaifa kwa ajili ya kurekodi  madhila wanayopata waandishi wa habari ama vyombo vya habari. Lengo likiwa ni kuwa na ushahidi wa kitakwimu na uhalisia kwa ajili ya kufanya uchechemuzi  wenye ushahidi.

Malengo mengine ni kutambua na kuwaumbua wanaonyanyasa na kuumiza wanahabari, ili kupata msaada wa kikanda na kimataifakuelimisha umma, kuwaambia waandishi wa habari kuwa kupatwa na madhila siyo ajali kazini na siyo changamoto za kitaaluma; na kuondoa kutokujali kwa wale wanaofanya madhila hayo.

 

Madhila yanayorekodiwa na MCT

Madhila yanayorekodiwa na kanzidata hiyo katika kipindi cha miaka kumi (2012 – 2022) ni kunyimwa taarifa, kutishiwa, kukamatwa, chombo cha habari kufungiwa, kutekwa, kuingiliwa kwa uhuru wa uhariri, kupigwa faini kwa chombo cha habari, vifo, kuharibiwa vifaa vya kazi, kuondolewa katika eneo la tukio kinyume cha sheria na kujidhibiti (self-censorship).

Kanzidata hiyo imekuwa ikipokea taarifa zake kupitia vyombo vya habari, waandishi wa habari, waratibu wa klabu za waandishi wa habari na kupitia mitandao ya kijamii.

 

Idadi ya waandishi waliokumbwa na madhila

Katika kipindi cha miaka kumi toka kuanzishwa kwa kanzidata hiyo jumla ya waandishi wa habari 272, kati yake wanaume 219 na wanawake 53 walikumbwa na madhila mbali mbali kama yalivyoainishwa hapo juu na katika kipindi hicho hicho, vyombo vya habari 94 vilikumbwa na madhila hayo. Matamshi au vitendo  19 vilielekezwa kwa waandishi na vyombo vya Habari kwa ujumla.

 

Idadi ya madhila yaliyoripotiwa na kurekodiwa

Madhila ambayo yamerekodiwa katika kanzidata ya MCT katika kipindi hicho ni 271, ambapo kukamatwa kwa waandishi wa habari wakiwa kazini, kuliongoza kwa kuwa matukio 52, ikifuatiwa na vitisho kutoka kwa watoa taarifa mbali mbali matukio 50 na waandishi wa habari kunyimwa taarifa matukio 45.

Madhila mengine ni mashambulio ya mwili (assault) matukio 25, kufungiwa vyombo vya habari (29), faini (14), kuondolewa katika eneo la kazi au eneo la tukio kwa nguvu au kwa vitisho (10), kutekwa waandishi wa habari au kutoweka katika mazingira ya kutatanisha matukio sita, kudhalilishwa matukio 13, na kujidhibiti kwa chombo cha habari matukio manne.

Pia kuna matukio 15 ya waandishi wa habari kuharibiwa na kutaifishwa vifaa vyao vya kazi, huku uminywaji wa mitandao ya kijamii matukio matatu, mauaji matukio matatu, na kuingilia uhuru wa uhariri matukio mawili.

 

Wahusika wa matukio hayo

Kanzidata inaonyesha kuwa taasisi iliyoongoza kwa matukio mengi dhidi ya  uhuru wa habari ilikuwa ni polisi ambayo ilikuwa na matukio 51.

Wahusika wengine ni pamoja na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) matukio 21, wizara mbali mbali matukio 14, wakuu wa wilaya matukio tisa, mashabiki wa mpira matukio matano, wakulima na wafugaji  matukio mawili na watu wasiojulikana matukio kumi. Idara ya Habari Maelezo (Bara) haikubaki nyuma nayo ilikuwa na matukio nane na wakuu wa mikoa matukio saba.

Wahusika wengine wa madhila yaliyowapata waandishi wa habari katika kipindi hicho ni mgambo, madiwani na watendaji kata matukio manne, Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) matukio matatu, Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) matukio matatu, mahakama matukio matatu, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), matukio mawili, Chama cha Mapinduzi (CCM) tukio moja, Tume ya Utangazaji Zanzibar matukio mawili, maafisa maendeleo ya jamii matukio mawili na Mwananchi Communications Limited matukio mawili.

Wahusika wafuatao wamefungana kwa kuwa na tukio moja moja, nao ni viongozi wa dini, Azam Media Group, wapiga kura wa Msikiti wa Makanyagio, Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano.

 


Matukio hayo yalitokea wapi

Katika mikoa 26 ya Tanzania Bara madhila kwa uhuru wa habari yaliyorekodiwa yalitokea katika mikoa 25. Kwa mujibu wa taarifa zilizoripotiwa katika kipindi hicho cha miaka kumi, mkoa wa Songwe haukuwa na madhila.

Ifuatayo ni mikoa kumi ya Tanzania Bara iliyoongoza kwa madhila na idadi yake. Mkoa wenye matukio mengi zaidi ni Dar es Salaam matukio 43, Shinyanga (18), Arusha (17), Dodoma (15), Mara (13), Kagera (12), Kilimanjaro (11), Tanga (10), Ruvuma na Singida matukio nane kila mmoja; na Mwanza, Rukwa na Pwani matukio saba kila mmoja. Kwa upande wa Zanzibar (Unguja na Pemba), jumla ya madhila 15 yaliripotiwa katika kipindi hicho.

Taarifa ya idadi ya madhila iko kama ifuatavyo 2013 (38), 2014 (27), 2015 (20), 2016 (32), 2017 (5), 2018 (24), 2019 (40), 2020 (41), 2021 (26) na 2022 (18).

Kutokea kwa madhila kumeendelea kujenga hofu miongoni mwa waandishi wa habari na vyombo vya habari na kusababisha uandishi wa habari usio wa kina  na kukosekana kwa habari za kiuchunguzi.

Matukio haya pia yameendelea kuishusha Tanzania katika sura ya kimataifa. Kwa mfano, katika ripoti za World Press Freedom Index, Tanzania imeendelea kushuka katika viwango vya uhuru wa habari kutoka nafasi ya 70 mwaka 2013 mpaka nafasi ya 124 mwaka 2021 na mwaka 2022 nafasi ya 123.

 

Wito kwa wanahabari

MCT inawahimiza waandishi wa habari kufanya kazi kwa uhuru, weledi na kufuata maadili, na pale kunapokuwa na changamoto kuwasiliana na Baraza. Madhila kwa waandishi wa habari yasichukuliwe kama ni ‘ajali kazini’, bali ni mambo yanayotakiwa kuripotiwa na kurekodiwa ili Tanzania iwe na rekodi ya madhila ambayo waandishi wanakutana nayo. Uwepo wa taarifa utasaidia kuonyesha ukubwa wa tatizo na kuongezwa kwa jitihada za kutafuta suluhu. Jitihada hizi zitakuwa na mashiko zaidi pale kunapokuwa na ushahidi wa kitakwimu.

Waandishi wa habari na taasisi za kihabari ziendelee kuunga mkono juhudi za Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan za kuhakikisha tasnia ya habari inafanya kazi kwa uhuru lakini kwa kufuata maadili na kwa weledi.

Pia MCT inawahimiza waandishi kuendelea kufanya kazi kwa kufuata kanuni za maadili ya uandishi wa habari ambayo tumejiwekea wenyewe ili yaendelee kuongoza katika utendaji wetu na namna tunavyoandika habari zetu.

Ni jukumu la kila mwandishi kuhakikisha anaripoti matukio yote ya kumdhalilisha au kumsababisha asiweze kufanya kazi zake kwa uhuru na weledi. Tafadhali ripoti matukio hayo MCT au Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), kwa hatua zaidi.

Wakati huo huo tunazikumbusha taasisi na watendaji mbalimbali kuwa haki ya kupata taarifa na habari ni haki ya kikatiba kwa wananchi wa Tanzania. Kukwaza uhuru wa habari pasipo sababu halali ni kuwanyima wananchi haki yao.

Taarifa hizi pia zinapatikana kwenye kanzidata ya MCT www.pressviolation.or.tz au kwenye ripoti za UTPC ambazo pia zinapatikana katika tovuti ya www.utpc.or.tz  au tembelea ofisi hizo kwa taarifa zaidi. (CHANZO MCT)

 

Comments

BLOG'S VISITORS

DAKTARI MWENGINE CHAKE CHAKE KULA SIKUKUU POLISI, NI KWA TUHUMA ZA KUMBAKA MGONJWA WAKE

NA WAANDISHI WETU, PEMBA::: DAKTARI anaetoa huduma kwa wagonjwa kituo cha afya cha serikali cha  Gombani wilaya ya Chake Chake Pemba, Is-haka Rashid Hadid, anaendelea kushikiliwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa kaskazini Pemba, akituhumiwa kumtorosha na kisha kumbaka mtoto wa mwenye umri wa miaka 16, mkaazi wa Gombani. Daktari huyo miaka 35 ni mkaazi wa Kangagani Wilaya ya Wete mkoani humo, ambapo anadaiwa alimchukua mtoto huyo kutoka kwa rafiki yake, na kumpeleka kwenye nyumba anayoishi eneo la Kangagani. Mtoto aliefanyiwa kitendo hicho alisema kuwa, April 21 mwaka huu alikwenda kituo cha afya Gombani, kwa ajili ya matibabu na baada ya kupatiwa huduma na daktari huyo, alimuomba nambari yake ya simu. Alisema ilipofika usiku, walikuwa wanawasiliana kupitia ujumbe mfupi (sms) kwa lengo la kwenda kuchukua dawa nyingine ambazo kwa mchana huo alizikosa hospitalini hapo. "Nilikwenda hospitali kutibiwa, baada ya kufanya mapele katika sehemu zangu za siri, lakini akaniambia mpaka aje da

'MKAPA' NA WENZAKE PEMBA WALAZWA RUMANDE

  NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@ MAHKAMA kuu Zanzibar kisiwani Pemba, chini ya Jaji Ibrahim Mzee Ibrahim, imewapeleka rumande watumuhimwa wanne wanaokabiliwa na tuhuma za kuua kwa makusudi, akiwemo Ali Mussa Omar ‘ Mkapa’ mkaazi wa Wawi wilaya ya Chake chake Pemba. Watuhumiwa wengine walioanza maisha mapya ya rumande ni mtuhumiwa Yassir Mohamed Juma miaka 23, Anuwari Mussa Omar miaka 30 pamoja na mtuhumiwa Yassir Mussa Omar ‘ Makababu ’ miaka 29, wote wakaazi wa shehia ya Wawi, wilaya ya Chake chake Pemba. Awali watuhumiwa hao waliwasili mahakamani hapo, kwa mara ya kwanza, kwa ajili ya kusomewa tuhma zinazowakabili za kumuua kwa maksudi Said Seif Kombo. Ilidaiwa mahakamani hapo na Mwendesha Mashtaka kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashataka Seif Mohamed Khamis akiambatana na mwenzake Mussa Khamis Ali kuwa, watuhumiwa hao kwa pamoja wanadaia kufanya mauwaji hayo kwa maksudi. Ilidai kuwa, watuhumiwa wote kwa pamoja, walitenda kosa hilo Oktoba 16, mwaka huu, baina ya saa 7:00 mchan

HII KALI MBUNGE ASIYA AMKOGESHA MWANANCHI HADHARANI KISA HICHI HAPA......

  NA HAJI NASSOR, PEMBA MBUNGE wa viti maalum nafasi za wanawake mkoa wa kaskazini Pemba Asiya Sharif Omar, amewataka wananchi wa kijiji cha taifu, shehia ya Kinyasini jimbo la Gando wilaya ya Wete Pemba, kuyalinda miundombinu ya maji safi na salama, ili yawe endelevu kwao. Kauli hiyo ameitoa wakati alipokuwa akizungumza na mwandishi wa habari hizi, mara baada ya kuwasili kijijini humo, na kumkogesha mwananchi mmoja kama ishara ya uzinduzi wa mradi wa maji safi na salama, ulioasisiwa na mbunge wa Jimbo la Gando. Alisema, hawana mbadala kwa sasa bali ni kuilinda miundombinu ya huduma hiyo, hasa baada ya mbunge wa wao Salim Mussa Omar, kuwarejeshea huduma hiyo. Alieleza kuwa, inafahamika kuwa kwa miaka 14 waliikosa huduma hiyo hasa kwa vile viongozi waliokuwepo hawakujali kuwatatulia tatizo hilo, hadi juzi ilipofanywa na mbunge wao. “Baada ya huduma hii sasa kurejeshwa na mbunge wa jimbo la Gando, kazi iliyobakia kwenu wananchi ni kila mmoja kuwa mlinzi wa miundombinu hii,’’ali

TUHMA ZA DAKTARI PEMBA KUCHIWA HURU: POLISI KASKAZINI KUTOA TAARIFA RASMI LEO

  NA HAJI NASSOR, PEMBA KAMANDA wa Polisi mkoa wa kaskazini Pemba, Juma Saad Khamis, amesema leo Mei 9, mwaka huu atatoa taarifa rasmi, juu ya kuendelea kumshikilia au kumpa dhamana ya Polisi, daktari wa Kituo cha Afya Gombani Is-haka Rashid Hadid, anayetuhumiwa kwa ubakaji. Alisema, kwa vile alikuwa katika mapumziko mafupi, haelewi jambo lolote linaloendelea kwa mtuhumiwa huyo, juu ya kuendelea kushikiliwa kwake kituoni hapo. Alieleza kuwa, leo Mei 6 (jana), hajapata taarifa za ndani za mtuhumiwa, huyo na kuwataka wananchi na wanaharakati, wasubirie hadi Jumatatu ijayo. Akizungumza na waandishi wa habari kwa nyakati tofauti Kamanda huyo, alisema hana taarifa zozote za kupewa dhamana mtuhumiwa ndani ya kituo chake cha Polisi au kuendelea kuwepo. ‘’Ilikuwa mimi sipo kazini kwa muda, kuanzia anakamatwa hadi anafikishwa Polisi, kwa sasa siwezi kueleza jambo lolote kwa mtuhumiwa huyo, hadi Jumatatu,’’alieleza. Aidha Kamanda huyo alieleza kuwa, kwa sasa hawezi kutoa ufafan

MADAKTARI KUTOKA CHINA WAOKOA MAISHA YA MTOTO PEMBA

  HABIBA ZARALI, PEMBA TIMU ya 32 ya madaktari wa kichina katika hospitali ya Abdalla Mzee Mkoani wamefanikiwa kufanya upasuaji mkubwa wa mtoto mwenye umri wa miaka 15 mkaazi wa Chole Kengeja, baada ya kuchomwa na jiti sehemu ya njia zake za mfumo wa uzazi. Mtoto huyo ambae alianguka hivi karibuni katika mti na baadae kuchomwa na jiti hilo na kumsababishia kutokwa na damu nyingi katika sehemu ya nyonga, alifanyiwa upasuaji uliodumu kwa muda wa saa tatu na   kuokolewa maisha yake. Akizungumza mara baada ya operesheni huo kiongozi wa timu hiyo Dr Jiang Jinhua, alisema mara baada ya mtoto huyo kufikishwa hospitalini hapo na kufanyiwa vipimo na kuonekana   ilibidi apatiwe rufaa ya kwenda katika hospitali nzuri yenye kutibu tatizo lake huko nchini Kuwado ambapo haikuwezekana kutokana na hali ya umaskini wa f amilia ya mtoto huyo . Alisema timu ya madaktari hao itaendelea kutowa huduma za matibabu   kwa wananchi kisiwani humo,   ili kuwaondolea gharama ya kutafuta matibabu nje ya nch