NA ZUHURA
JUMA, PEMBA
WAFANYABIASHARA
na wajasiriamali kisiwani Pemba wametakiwa kuwa na utayari katika kufanya
shughuli zao za kibiashara, ili kufikia lengo walilokusudia.
Akifungua mkutano ulioandaliwa na Jumuiya ya kitaifa ya
Wafanyabiasha Zanzibar (ZNCC), Meneja wa Benki ya NMB Pemba Hamad Mussa Msafiry
alisema, kuna baadhi ya wafanyabiashara wapo tayari ingawa hawana mtaji.
Alisema kuwa, benki hiyo ipo tayari kuwasaidia wafanyabiashara
wenye utayari, kwani wanaamini kuwa uwezo wao ni mkubwa katika kufikia malengo
yao waliyoyakusudia.
‘’Wapo ambao wana uwezo lakini hawapo tayari, lakini kuna hawa
wenye utayari lakini hawana uwezo hivyo ni rahisi kuwajenga na benki yetu ipo
tayari kuwasaidia’’, alisema Meneja huyo.
Alieleza kuwa, lengo la Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni
kuhakikisha wanawawezesha wajasiriamali wadogo wadogo kujiajiri kwa kujipatia
kipato kitakachowakwamua na maisha duni.
‘’Zile ajira laki tatu zilizoahidiwa na Dk. Hussein Mwinyi
tunataka zitoke hapa, hivyo muwe na mipango mizuri ili kuona kwamba
tunafanikisha’’, alifafanua.
Kwa upande wake Mratibu wa Jumuiya ZNCC Pemba Khalfan Amour
Mohamed alisema, wameona kwamba kuna haja ya kuwapa mafunzo wajasiriamali na
wafanyabiashara hao, ili kuwasaidia katika shughuli zao.
‘’Katika mkutano huu watafunzwa namna ya kutumia fursa za
kibenki, namna ya kuzitumia na namna ya kutunza kumbu kumbu’’, alieleza Mratibu
huyo.
Akitoa mada muwasilishaji kutoka Ofisi ya Wakala wa Usajili wa
Biashara na Mali Pemba (BPRA) Mohamed Ali Maalim alisema, ni muhimu kwa kila
mfanyabiashara kusajili biashara yake.
Alisema kuwa, usajili huo utamsaidia kupata haki na fursa ya
kufanya biashara bila vikwazo, kupata fursa ya mikopo ili kupata mtaji, kupata
taarifa na takwimu sahihi kwa watakaohitaji.
‘’Unachotakiwa ni kusajili kampuni, majina ya biashara, tasnia
za mali bunifu, usajili wa nyaraka, mikataba ya amana kwa mali ziazohamishika,
hizi zitawasaidia katika biashara zenu ikiwemo kupata mkopo kwa urahisi’’,
alieleza.
Nao washiriki hao wameomba kuwa, elimu hiyo itolewe katika
vijiji mbali mbali ili jamii ipate uelewa wa kutosha, kwani wengi wao wamekosa
elimu hiyo ambayo ni muhimu katika uendeshaji wa biashara zao.
Mkutano huo wa siku mbili umeandaliwa na Jumuiya ya Kitaifa ya
Wafanyabiashara Zanzibar (ZNCC) kwa lengo la kuwafahamisha mambo mbali mbali
yatakayoweza kuwasaidi katika biashara zao, ikiwa ni pamoja na kujipatia
kipato.
MWISHO.
Comments
Post a Comment