NA HAJI NASSOR, PEMBA
MAHAKAMA
maalum ya makosa ya udhalilishaji mkoa wa kusini Pemba, imemsweka rumande
kijana Nassor Ali Ramadhan miaka 18 wa Msingini wilaya ya Chake chake, kwa
tuhma za ubakaji.
Akiwa juu ya kizimba cha
mahakama hiyo, chini ya hakimu Muumini Ali Juma, Mwendesha mashtaka wa serikali
kutoka Afisi ya Mkurugenzi wa mashtaka Ali Amour Makame, alidai kuwa, tukio
hilo lilitokea Oktoba 10, mwaka huu.
Alidai kuwa, kijana huyo
bila ya halali na bila ya ridhaa ya wazazi wa wa mtoto wa kike, alimbaka mtoto
wa miaka 17, akijua kuwa kufanya hivyo ni kosa.
Alidai kuwa, siku hiyo
mtuhumiwa alimuingilia mtoto, jambo ambalo ni kosa kisheria, kinyume na kifungu
cha 108 (1), (2), (e) na kifungu cha 109 (1) cha sheria ya Adhabu nambari 6 ya
mwaka 2018, sheria ya Zanzibar.
Mara baada ya kusomea maelezo
hayo, hakimu wa mahakama hiyo, alimuuliza mtuhumiwa, ikiwa amefahamu vyema
maelezo yaliotolewa mahakamani hapo.
‘’Mtuhumiwa, je umefahamu
vyema maelezo ya kosa lako, hebu nieleze na mimi ikiwa kweli umeyasikia na
kuyafahamu vyema,’’alisema Hakimu huyo.
Hata hivyo mtuhumiwa huyo,
ambae yuko chini ya wakili wake wa kujitegemea Massoud Mohamed Said, alieleza
kuyafahamu vyema maelezo ya kosa lake, kama yalivyosomwa na Mwendesha mashtaka.
‘’Mheshimiwa hakimu, pamoja
na kuyafahamu vyema maelezo hayo, mimi nakataa kuwa sijambaka mtoto wa miaka
17, siku ya Oktoba 10, mwaka huu, kama ilivyoelezwa,’’alidai.
Hata hivyo upande wa
mashataka ulidai kuwa, tayari ushahidi umeshakamilika na kuiomba mahakama hiyo,
kuliahirisha shauri hilo na kulipangia siku nyingine.
Hakimu Muumini Ali Juma,
baada ya kupewa taarifa hiyo, aliuuliza upande wa utetezi, na kujibu hauna
shaka na kutaka mtuhumiwa apelekwe rumande, na kurudi tena mahakamani hapo Novemba 22, mwaka huu.
Mwisho
Comments
Post a Comment