NA HAJI NASSOR, PEMBA::::
WAJUMBE
wa kamati maalum ya kuelekea siku 16 za kupinga ukatili wa wanawake na watoto,
kisiwani Pemba, wametakiwa kutoa michango yao ya hali na mali, ili kufanikisha
shughuli hiyo.
Kauli hiyo imetolewa leo Novemba 17, 2022 na
Mwenyekiti wa kamati hiyo Nassor Bilali Ali, wakati akizungumza kwenye kikao
kazi cha kamati hiyo, kilichofanyika Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar ‘ZLSC’
chenye lengo la kupanga mikakati ya kufanikisha shughuli husika.
Alisema, kwa wakati na siku
zilizobakia, ni lazima kwa kila taasisi ambayo inaunda kamati hiyo, kutoa fedha
au kitu kinachotakiwa kufanikisha shughuli hiyo, ikiwa ni pamoja na maji,
chakula na usafiri.
Alisema, kama jambo hilo
walilianzisha kwa furaha na bashasha, sasa wakati wa kulimaliza umefika, kwa
wajumbe wa kamati hiyo, kuanza wao kutoa michango yao, kabla ya kuzifuatilia
tasisi zilizoombwa.
‘’Kwanza wajumbe waache
dharura ambazo sio za msingi, pili ni wakati na wao kuwasilisha michango yao, ili
kiwango cha zaidi ya shilingi milioni 6 zilizopangwa kufanikisha, shughuli hiyo
zipatikane,’’alisema.
Mwenyekiti huyo, alisema
zipo baadhi ya taasisi kama TAMWA, TUJIPE, KUKHAWA, PEGAO, ZLSC, PAFIC, ZAPDD
pamoja na jumuia za wasaidizi wa sheria za wilaya, zimeshaonesha moyo wa kutoa
michango hiyo.
Katika hatua nyingine
Mwenyekiti huyo wa kamati ya maandalizi ya kueleka siku 16 za kupinga ukatili
na dhalilishaji Nassor Bilali Ali, alisema kuanzia wiki ijayo hakuna mapunziko
kwa wajumbe wote, hadi pale watakapofanikisha.
Mjumbe wa kamati hiyo Tatu
Abdalla Msellem, alisema Jumuiya ya TUJIPE, itahakikisha inafikisha mchango
wake, kwenye kamati hiyo, ili kufanikisha azma hiyo.
‘’Tunaahidi kuchangia kiasi
fulani cha fedha, ili kufanikisha shughuli hii, maana na sisi TUJIPE inatugusa
hasa kwa vile wanaotetewa ni wanawake na watoto,’’alisema.
Mjumbe kutoka TAMWA Fat-hya
Mussa Said, alisem TAMWA itahakikisha, inachangia kiasi kikubwa cha fedha,
utaalamu na uchapishaji mabango ili kufikia lengo hilo.
‘’Hata maji, mabango na
vipaza sauti naahidi kuwa TAMWA itachangia, ili kufanikisha shughuli hii, maana
sisi anapotajwa mwanamke na mtoto huwa ni eneo letu pia,’’alifafanua.
Kwa upande wake mjumbe wa
kamati hiyo Khalfan Amour Mohamed kutoka ZAPDD alisema, ili kufanikiha shughuli
hiyo, atakaa na viongozi wenzake.
Hata hivyo Katibu wa kamati
hiyo, Safia Saleh Sultan na mjumbe Hafidh Abdi, walisisitiza wajumbe kushiriki
katika vikao mbali mbali, ili kufanikisha shughuli hiyo.
Kamati hiyo inatarajia
kukutana na waandishi wa habari Novemba 24, mwaka huu katika ukumbi wa TAMWA Chake
Chake Pemba, ili kutoa taarifa ya kuelekea uzinduzi a siku 16 za kupinga
ukatili na udhalilishaji.
Aidha kazi nyingine ambayo
itafanywa na kamati hiyo ni matembezi, makongamano, mikutano ya elimu kwa
wilaya nne za Pemba, kwa kukutana wazazi, waalimu na wanafunzi wa madrassa.
Pamoja na shughuli nyingine
kama vile vipindi vya redio, kilele cha maadhimisho hayo kinatarajiwa kufanyika
ukumbi wa Samail Gombani Chake chake Disemba 10, mwaka huu.
Mwisho
Comments
Post a Comment