NA HAJI NASSOR, PEMBA::
JAMUIYA
ya wakalimani wa lugha ya alama Zanzibar ’JUWALAZA’ imeitaka jamii kujiunga na
jumuiya hiyo, ili kujifunza lugha ya alama, ili kukidhi haki ya mawasiliano kwa
watu wenye ulemavu wa uziwi.
Akizungumza na mwandishi wa
habari hizi kwa njia simu, leo Novemba 18, 2022 Katibu Mkuu wa jumuiya hiyo Kheir Mohamed Simai
alisema, bado jamii haijaona umuhimu, wa kujifunza lugha ya alama, na kuwasaidia
viziwi katika mawalisiliano.
Alieleza kuwa, kundi la
viziwi katika jamii ni sawa na kundi jengine lolote, ambalo linahaki ya
kuwasiliana baina yao na kundi jengine, ingawa wao ni kwa kutumia lugha ya
alama.
‘’Mawasiliano ya wenzetu
hawa ni maalum, hivyo kila mmoja ana haki ya kuhakikisha anawasiliana nao, ili
kutumiza utu na ubinadamu, lakini jambo la kwanza ni kujifunza lugha ya alama,’’alieleza.
Aidha Katibu mkuu huyo,
alisema Jumuiya tokea mwaka 2019, imekuwa na utaratibu wa kufanya maadhimisho
ya siku ya wakalimani, ingawa kwa mwaka huu. siku hiyo imesogezwa mbele kwa
siku moja.
‘’Novemba 18 kwa vile ni
Ijumaa, tumeona bora tuendeshe dua maalum, kwa ajili ya kuwaombea dua viongozi,
watetezi wa haki za watu wenye ulemavu, pamoja na waasisi wa Umoja wa watu
wenye Ulemavu Zazibar, akiwemo maalim Khalfan Hemed Khalfan,’’alifafanua.
Katika hatua nyingine, Katibu
mkuu huyo wa Jumuiya ya wakalimani Zanzibar Kheir Mohamed Simai alisema, wazazi
na walezi ndio kundi la mwanzo, kuhakikisha wanawalinda na kuwapatia haki zao
viziwi.
Mjumbe wa Jumuiya hiyo
kisiwani Pemba, Asha Suleiman alisema, bado jamii haijaona umuhimu wa
kuwashirikisha viziwi katika mipango na mikakati ya kimaisha.
Alieleza kuwa, wenye uziwi
hawaonekani kua wanamchango wowote katika jamii, hivyo huanza kubaguliwa
kuanzia kwenye haki ya msingi ya mawasiliano.
‘’Utaona kiziwi anahitajia
huduma katika eneo fulani, lakini kwa vile muombwa huduma hakujifunza lugha ya
alama, huishia kumcheka na kumdharau, jambo ambalo sio sahihi,’’alieleza.
Issa Haji Mjanakheri wa
Kangangani wilaya ya Mkoani, wenye uziwi alisema, amekuwa akipata shida wakati
anapotaka huduma, hasa kwenye ofisi za umma.
Aisha Omar Ali wa Mtambile,
alisema ni vyema suala la ufahamu wa lugha ya alama, likawa lazima kuanzia
ngazi ya jamii hadi taifa.
‘’Ingawa sasa kuna ahuweni kwenye
ZBC tv, tunaona kuna mtaalamu wa lugha ya alama, na hasa kwenye taarifa ya
habari au shughuli za kitaifa akiwasiliana na viziwi,’’alieleza.
Siku ya wakalamani huadhimishwa
kila ifikapo Novemba 18, ya kila mwaka, ambapo kwa mwaka huu, itaadhimishwa Novemba
19, eneo la Unguja ukuu na mgeni rasmi akitarajiwa kuwa Mkuu wa mkoa wa kusini
Rashid Hadid Rashid.
Upande mwengine ni kuwa,
siku ya Ukalimani wa lugha ya alama duniani, ilianzishwa na Umoja wa Mataifa
UN, mwaka 2017, ambapo Umoja huo, ulipitisha siku hiyo kwa sababu ya shirikisho
la wakalimani duniani ‘FIT’ wamekuwa wakiitumia siku hiyo, kuadhimisha siku ya
wakalima na wafasiri tangu mwaka 1991.
Mkataba wa kimataifa wa haki
za watu wenye ulemavu Ibara ya 21 (b) inaeleza kuwezesha matumizi ya lugha ya
alama, maandishi ya braille kuongoza na kuweka mawasiliano mbadala kwa njia
nyingine na mfumo wa mawasiliano watakaoamua.
Aidha sheria nambari 9 ya
mwaka 2016 ya haki na fursa ya watu wenye ulemavu Zanzibar kifungu cha 15, ni
lazima mawasiliano kwa watu wenye ulemavu utolewe kwa njia mbali mbali, ikiwemo
la nukta nundu na lugha ya alama.
mwisho
Comments
Post a Comment