NA HAJI NASSOR, PEMBA:::
WATETEZI wa haki za watu wenye ulemavu kisiwani Pemba, wamepongeza
hatua ya Mahakama maalum ya makosa ya udhalilishaji, mkoa wa kaskazini Pemba,
kumuhukumu kutumikia chuo cha mafunzo miaka 7, mshtakiwa Nuhu Kombo Nuhu, baada ya kupatikana na hatia ya
kumlawiti, kijana mwenye ulemavu wa akili.
Walisema, uamuazi wa mahakama hiyo,
kutenda haki katika kesi hiyo ambayo ilishaanza kukumbwa na changamoto hasa ya
mshtakiwa kujifanya ana umri wa miaka 17, lakini hatimae haki ilitendeka.
Wakizungumza na mwandishi wa
habari kwa nyakati tofauti, baada ya hukumu hiyo, walisema kitendo alichokifanya
mshitakiwa huyo, cha kumlawiti kijana (19) mwenye ulemavu wa akil, sio cha
kibinadamu na kinafaa kulaaniwa.
Mmoja kati watetezi hao, Safia
Saleh Sultan kutoka Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar ZLSC, alisema kama
mahakama zintaendelea na masimamo huo, kundi la watu wenye ulemavu litaheshimaka.
Alieleza kuwa, watu wenye ulemavu
hasa wa akili, lazima waangaliwe vyema wanapotoa ushahidi, na ikiwezekana
wasaidiwe ili kunyoosha maneno vizuri.
Nae Mratibu wa Jumuiya kwa ajili
ya watu wenye ulemavu wa akili Zanzibar ‘ZAPDD’ Khalfan Amour Mohamed, alisema
ingawa hatia hiyo ni ndogo, lakini imesaidia kwa kundi la watu wenye ulemavu.
‘’Sio kawaida sana kukutana na kesi
za watu wenye ulemavu kushinda, maana yale mazingira waliyonayo, huwa ni
kichaka kuziua kesi, lakini kwa hii kwa kiasi fulani tunapongeza,’’alieleza.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa
Jumuia ya wasioona Zanzibar ‘ZANAB’ Pemba Suleiman Mansour, alisema ushirikiano
kati ya wazazi wa kijana mwenye ulemavu wa akili, na vyombo vya sheria,
ulichangia kutiwa hatiani kwa mshitakiwa huyo.
Mwakilishi wa kundi la vijana
wenye ulemavu, katika baraza la vijana Zanzibar Katija Hamad, alisema hatua
iliyochukuliwa na vyombo vya ulinzi na usalama, imesaidia kupatikana kwa haki.
‘’Bado niendelee kuwasisitiza
wazazi na walezi, kuwawekea ulinzi maalum watoto wao wenye ulemavu, maana
wadhalilishaji sasa wameamua kulikimbilia kundi hilo,’’alisema.
Mkuu wa mkoa wa kaskazini Pemba,
Salama Mbarouk Khatib, amekuwa akirejea tamko lake, la kuwataka wazazi kukataa
kuzifanyia sulhu kesi za udhalilishaji, na badala yake waviachie vyombo vya
sheria kuamua.
Wazazi wa mtoto aliyelawitiwa,
walisema hawakuamini kuwa haki ya mtoto wao ingepatikana, kutokana na
changamoto walizopitia, ikiwa ni pomoja na mshitakiwa kupunguziwa umri.
‘’Awali mshitakiwa tuliambiwa ni
mtoto, hivyo kesi yake ilishaanza kusikilizwa mahakama za watoto, lakini baada
ya vipimo ikaonekana ni mtu mzima, hadi sasa kufikia kufungwa miaka saba,’’walisema.
Nuhu Kombo Nuhu (19) mkaazi wa
Kijichame wilaya ya Micheweni Mkoa wa kaskazini Pemba, sasa anaendelea kutumikia
chuo cha mafunzo kwa miaka saba (7), na kulipa fidia ya shilingi milioni 1, baada
ya kupatikana na kosa la kumlawiti, kijana mwenzake mwenye ulemavu wa akili
miaka 19.
Hakimu wa mahakama maalum ya makosa
ya udhalilishaji mkoa wa Kaskazini Pemba, Abdulrahman Ali Abdul Rahman, alisema
kesi hiyo imesikilizwa ikiwa na mashahidi wa watano, ambao ushahidi wao ulitosha
kuishawishi mahakama kumtia hatiani.
Tukio hilo lilitokea Disemba 13,
mwaka 2021, majira ya saa 1:30 asubuhi eneo la Kijichame wilaya ya Micheweni
mkoa wa Kaskazini Pemba, ambapo mshitakiwa huyo, alimlawiti kijana mwenye
ulemavu wa akili.
Kufanya hivyo ni kosa kinyume na
kifungu cha 116 (1), cha sheria Adhabu nambari 6 ya mwaka 2018 sheria ya
Zanzibar.
Mwisho
Comments
Post a Comment