NA HAJI NASSOR, PEMBA:::
KANUNI ya
Utumushi wa Umma ya Zanzibar ya mwaka 2014, imeundwa na vifungu wastani wa 134.
Kanuni hii, ni zao la sheria ya Utumishi wa Umma ya Zanzibar,
ambayo nayo ilitungwa na Baraza la Wawakilishi, kwa lengo la kubainisha na
kuweka wazi haki, wajibu wa watumushi wa umma.
Kanuni hii, imekuja kufafanua na kuweka
taarifa kwa upana zaidi kwa watumishi wa umma wa Zanzibar, ili kuongeza kasi,
ari, hamasa na juhudi za kuwahudumia wananchi.
Kanuni hii ya utumushi wa umma ambayo ilisainiwa Mei, 29 mwaka
2014 kazi iliyofanywa na aliyekuwa Waziri wa nchi ofisi ya rais, kazi, na
utumishi wa umma Zanzibar Haroun Ali Suleiman.
UTEKELEZAJI
WA KANUNI HIYO
Watumishi waliowengi wa umma Zanzibar, kwao kanuni hii
imekuwa maarufu na kuitekeleza kwenye vifungu vichache ambavyo, pengine
vinamsaidia mwajiri na sio mwajiriwa.
Kwa mfano, wengi wa watumushi wa umma, wanaelewa kuwa kanuni
hiyo inavifungu vya kuhimiza kufika kazini saa 1:30 na kuondoka saa 9:30 kama
sio vyenginevyo, kwa wale watumishi wanaonyonyesha.
Lakini vifungu vyengine maarufu kwa watumishi wa umma ni cha
58 kinachogusa likizo la mwaka, kifungu cha 61 cha likizo la uzazi iwe pacha au
mtoto mmoja, kifungu cha 59 cha haki ya likizo la dharura pamoja na ya muda na
kile cha 60 cha likizo ya maradhi.
Kwenye kanuni hiyo, kifungu chengine ambacho ni maarufu kwa
watumishi wa umma, ni bwana mkubwa, yaani kupewa mshahara, ruhusa ya kuondokewa/filiwa
baba, mama, mke, mtumishi mwenyewe au mtoto.
Vifungu hivyo na vyengine vimekuwa maarufu, maana watumishi
wanapoajiriwa wamekuwa wakielezwa na muajiri, ingawa vyengine huelezwa pole
pole, kadiri matukio yanapotokea.
VIFUNGU
VIZURI VISIVYOTANGAAZWA HADHARANI
NA BAADHI YA WAAJIRI
Kwa uwingi wa vifungu vya aina hiyo, vilivyomo ndani ya Kanuni
ya Utumushi wa Umma ya Zanzibar ya mwaka 2014, leo tosheka na vifungu vifuatavyo,
ili kuvijua uzuri wake.
Kifungu cha 15 kinachoelezea upandishwaji daraja kwa watumushi
wa umma, ambapo kifungu kidogo (1), kinaeleza kuwa ‘kwa kuzingatia masharti ya kifungu cha 64
cha Sheria, Katibu Mkuu au Mkuu wa taasisi, atapendekeza kwa Tume ya Utumishi
husika kumpandisha daraja mtumishi yeyote wa umma’.
Kifungu
kikazidi kufafanuwa kuwa, mtumushi huyo ni mwenye sifa na ujuzi wa nafasi
zinazotarajiwa kujazwa kwa masharti yafuatayo, ikiwa ni pamoja na nafasi hiyo,
iwe inafahamika katika miundo ya kada za utumishi.
Na mtumishi wa kujaza
nafasi hiyo achaguliwe kwa mujibu wa masharti ya Sheria, ambapo kupandishwa
cheo kutafanyika kwa mtumishi atakayethibitika kuwa, anao uwezo wa kushika
madaraka katika nafasi zilizowazi na inayohitaji kujazwa.
Kifungu
chengine, ambacho kama hakitangaazwi sana vile na muajiri, ni kile cha 17,
ambacho kinampa haki mtumishi wa umma, aidha kukataa au kukubali cheo
alichopandishwa.
Ingawa
inamtaka mtumishi huyo, ikiwa anataka kukataa cheo hicho, afanye hivyo kwa muajiri
wake, kwa muda usiozidi mwezi mmoja, baada ya kuarifiwa kwake juu ya cheo hicho.
Kifungu
chengine ni kile cha 26, ambacho kimempa haki mtumishi mjamzito kikieleza kuwa,
‘ni
marufuku kwa Katibu Mkuu au Mkuu wa taasisi baada ya kupata uthibitisho kutoka kwa
daktari, kwa usalama na kwa afya ya mtumishi huyo, kumpangia kazi za usiku au
za ziada.
Kifungu
hicho kikaenda mbali zaidi kikieleza kuwa, ‘ni marufuku kuajiri au kumpangia mtumishi wa kike kufanya kazi
katika eneo lolote, lenye kutumika madawa ya kemikali za sumu, benzino au
mionzi, ambayo yatapelekea kuathiri uzazi au ujauzito wake.
Utamu
mwengine uliomo kwenye kanuni ya utumishi wa umma ya mwaka 2014, ni kwa wale
wenzetu wenye ulemavu, maana kifungu cha 30, kinaeleza wazi kuwa, ‘itakapotokezea
watu wa makundi maalum wana sifa sawa na watu wengine, katika masharti ya ajira,
kipaumbele kitatolewa kwa watu wa makundi maalum.
Kipo kifungu
cha 62 nacho sio maarufu sana, kinachompa haki mume, ambae ni mtumishi wa umma,
cha mapunziko ikiwa mke wake hata amabe sio mtumishi amejifungua, kupumzika.
Kifungu
hicho kinachoundwa na vifungu viwili vidogo kinafafanua kuwa, ‘mtumishi
wa umma ambae mkewe amejifungua, ataruhusika kupewa likizo ya malipo, kwa muda
wa siku tano za kazi.
Vifungu
hivyo pacha vikaeleza kuwa, ’likizo hilo litachukuliwa ndani ya siku
saba, baada ya mtoto kuzaliwa na halitoathiri likizo yake ya mwaka, na litatolewa
kila baada ya miaka mitatu.
Zuri zaidi
kanuni haikuwasahau wale, watumishi wenye mke zaidi ya mmoja iksema kuwa, ‘mtumishi
mwenye mke zaidi ya mmoja atastahiki likizo la kila mke atakapojifungua, hata hivyo,
endapo atakaekuwa anajifungua kila mwaka ni mke huyo huyo, mmoja atastahiki
likizo hilo kila baada ya miaka mitatu.
HALI IKOJE KWA WATUMISHI?
Mkuu wa
shirika la Magazeti Pemba Bakar Mussa Juma, anasema amekuwa akiwapa ruhusa
wafanyakazi ambao wake zao wamejifungua.
‘’Hivi sasa
kunamfanyakazi yuko mapunziko ya siku tano za kazi, na mwengine ameripoti
Septemba 15, mwaka 2022 akitokea kwenye mapunziko kama hayo,’’anasema.
Anasema
vifungu hivyo anaona sio maarufu kwa sababu havitumiki mara kwa mara, ingawa
kubwa zaidi ni watumushi kutozisoma kanuni husika
Fauzia Mussa
Alawi, asiyeoona ambae ana shahada uhasibu, anasema kanuni ya kuwapa kipaumbele
watu wenye ulemavu katika uajiri, haitekelezwi kwa kina.
‘’Mimi
nishawahi kufanya usaili nikiwa na wanaume wawili na mimi peke yangu, lakini
mwisho wa siku sikuajiri na aliajiriwa mwanamme,’’alieleza.
Mfanyakazi
wa wizara ya Habari Pemba Ali Suleiman, anasema sasa ana watoto wanne, ingawa
ni mtoto mmoja pekee, ndio alipata haki ya kupata mapunziko ya siku tano kwa mke wake kujifungua.
‘’Ni kweli
muajiri, zipo haki nyingine huzikalia kwa watumishi wao, na wanachojua wao ni
kutimiza wajibu kwa mtumishi ikiwemo kufika kazini na kuondoka kwa
wakati,’’anasema.
Aisha Hassan Mzee mtumishi wa wizara ya elimu, anasema inawezekana haki nyingi watumishi hawazijui, kwasababu wanaposmeshwa haziguswi.
Halima Iddi
Omar anayefanyakazi wizara ya Maji kwa miaka 28 sasa, anasema hakumbuki
kupandishwa daraja kama kanuni ya utumishi wa umma, inavyoelekeza.
Aliyekuwa Afisa
Utumishi wizara ya Ardhi Pemba Fatma Salim Matta, anasema aliwahi kutoa
mishahara ya watumishi wake wanne kuikabidhi kwa familia, wenyewe baada ya kufariki.
‘’Sisi huwa
makini kwenye haki za wafanyakazi au wategemezi wao, na ndio maana, tumeshawahi
kuitekeleza kanuni hiyo, baada ya watumishi wanne kufarika kwa wakati
tofauti,’’alieleza.
IPA
Chuo cha Utawala wa Umma Zanzibar 'IPA' kimekuwa kikiwasisitiza waajiri kuwasomesha watumishi wa umma kanuni na sheria za kazi, ili waepuke kuingia kwenye migogoro.
''Kwa mfano mwishoni mwa mwaka huu watumishi 1400 wa wizara ya elimu wakiwemo waalimu walisomeshwa sheria saba zinazohusu utumishi, hili ni jambo jema,''alisema muwezeshaji kutoka IPA Abubakr Nuhu.
ATHARI YAKE
Mfanyakazi wa wizara ya elimu Pemba, anasema moja ni kuwatayarisha watumishi kuwa wizi wa mali za umma.
''Ikiwa haki za wafanyakazi hasa ngazi za chini hazitekelezwi na kwa wakubwa zinatekelezwa, ni kuwatengeneza watumishi kuwa wizi, ili kufidia haki zao, blaming claim of right,''anasema.
Aisha Sudi kutoka wizara ya Miundombinu, anasema athari nyingine ni kuwadumaza watumishi na kuwanyima haki na fursa watumishi wa umma.
NIN KIFANYIKE
Watumishi wa umma wamesema ifike wakati sasa, muajiri kuweka darasa maalum kuwasomesha kanuni watumishi, hata kabla ya kuajiriwa.
Muwezeshaji kutoka Chuo cha Utawala wa Umma Zanzibar IPA Khamis Nassor, anasema watumishi lazima wajifunze kujisomesha kanuni na sheria.
Mwisho
Comments
Post a Comment