Joyce Joliga, Songea
Asilimia 97 ya watoto
wanaozaliwa hunyonyeshwa maziwa ya mama, ikiwa asilimia 92 ya watoto
hunyonyeshwa kwa kipindi cha mwaka mmoja na kuendelea.
Hayo yamebainishwa leo
na Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu Mhe.
Mwanaidi Khamis wakati akimwakilisha Waziri wa Afya Mhe Ummy Mwalimu kwenye
uzinduzi wa maadhimisho ya wiki ya unyonyeshaji maziwa ya mama kwa watoto
kitaifa yanayofanyika kwenye halmashauri ya Ikungi Mkoani Singida.
Mhe. Mwanaidi
ameendelea kusema kuwa 43% tu ya watoto ndio hunyonyeshwa hadi kipindi
cha miaka miwili na kuendelea huku takwimu zikionesha 57% tu ya watoto ndiyo
hunyonyeshwa maziwa ya mama pekee bila kuchanganya na chakula kingine wala maji
ndani ya kipindi cha miezi 6.
"Tafiti zinaeleza
kuwa mtoto akizaliwa na kuanza kunyonyeshwa maziwa ya mama ndani ya saa moja
kunaweza kuokoa uhai wake kwani kuchelewa kumnyonyesha mtoto kuna changia kwa
kiwango kikubwa vifo vya watoto wachanga ndani ya siku 28." Aliongeza.
Aidha, amesema hapa
nchini unyonyeshaji wa watoto wachanga ndani ya saa moja umefikia 90% hivi sasa
ikilinganishwa na 54% iliyokuwa mwaka 2018 wakati utoaji wa Vitamini A kwa
watoto wa miezi 6-59 nao umeongezeka kutoka 64% mwaka 2018 hadi kufikia 97% hivi
sasa.
Hata hivyo Naibu
Waziri huyo aliwahimiza wahudumu katika vituo vya kutolea huduma za afya kutoa
huduma kwa wakati husika na kuwaasa wazazi kuendelea kuhudhuria Kliniki kama
inavyoagizwa pia wazazi kuwanyonyesha watoto wachanga maziwa ya mama pekee kwa
kipindi cha miezi sita bila kumlisha chakula kingine wala maji pamoja na
kuwanyonyesha watoto kwa kipindi cha miaka miwili na zaidi.
"Kunyonyesha
maziwa ya mama kuna faida nyingi kwa mama na mtoto kwa kuwa kunaimarisha afya
na ustawi wa mama na mtoto, vilevile unyonyeshaji watoto maziwa ya mama huzuia
aina zote za utapiamlo kwa vile kuna kuwa na uhakika wa chakula kwa watoto
wachanga na wadogo". Alisisitiza
Vile vile amesema ili
kuimarisha na kuendeleza juhudi za kulinda Afya ya watoto kupitia unyonyeshaji
maziwa ya mama, Serikali itaendelea kufuatilia utekelezaji wa sheria, kanuni na
miongozo iliyopo juu ya unyonyeshaji watoto maziwa ya mama, kuendelea kutenga
fedha za kutekeleza afua za kuboresha ulishaji wa watoto ikiwemo elimu ya Afya,
lishe na huduma za msingi kwa wanawake wajawazito na wanaonyonyesha pamoja na
kutoa miongozo na taarifa sahihi kuhusu unyonyeshaji na namna ya kujikinga na
magonjwa hasa ya mlipuko.
Naye, Mkuu wa Wilaya
ya Ikungi Mhe. Jerry Muro amewataka wakurugenzi na watoa huduma ya Afya wa
halmashauri yake kuendelea kutoa elimu juu ya unyonyeshaji na kuwasihi wananchi
kuepukana na mimba za utotoni.
"Changamoto
zinazopelekea wazazi kutonyonyesha watoto zao ni pamoja na mimba za utotoni
kwakuwa hawajui umuhimu wa kunyonyesha na wengine kuwa bize na kazi na hivyo
kuacha kunyonyesha watoto zao." Amesema DC Muro
Aidha, Mkuu huyo wa
Wilaya ametoa rai kwa Serikali kuongeza muda wa ruhusa kwa wazazi wanaofanya
kazi ili kupata muda mwingi wa kuwanyonyesha watoto zao.
Maadhimisho hayo ya
wiki ya unyonyeshaji maziwa ya mama kwa watoto kitaifa yanayofanyika kwenye
halmashauri ya Ikungi Mkoani Singida kuanzia 1-7 Augusti 2022 yenye kauli mbiu
isemayo CHUKUA HATUA ENDELEZA UNYONYESHAJI: ELIMISHA NA TOA MSAADA
Comments
Post a Comment