IDARA ya utambuzi wa ardhi Pemba, imesema ardhi yenye eneo dogo iliyopangwa, kupimwa na kisha mmiliki kukabidhiwa hati ya matumizi, huwa na thamani mara mbili ya eneo kubwa ambalo halikupimwa.
Hayo yameelezwa na Afisa wa Utambuzi wa ardhi Pemba Faki Ali, wakati akijibu maswali ya wananchi wa shehia ya Mfikiwa wilaya ya Chakechake, kwenye mkutano wa wazi ulioandaliwa na na Jumuiya ya wasaidizi wa sheria wilaya ya Chakechake, CHAPO juu ya elimu ya utatuzi wa migogoro ya ardhi kwa njia ya amani.
Alisema, kuna umuhimu mkubwa kwa wananchi, ardhi zao kuzirasmisha kwa kuzitambua na kupata hati maalum za matumizi, ili ziongezeke thamani wakati zinapohitajika kwa matumizi mengine.
Alieleza kuwa, serikali ina nia ya kuipima ardhi yote ya Zanzibar, na kuwapa wananchi hati ya matumizi, bila ya malipo yoyote.
Afisa huyo alifafanua kuwa, tayari shehia tano za Unguja na Pemba zimeshaanza mpango huo kwa majaribio.
"Lazima wananchi waelewa kuwa, ardhi iliyopimwa hiafanani kithamani na nyengine, ambayo haijapimwa, na mgogoro sio rahisi kujitokeza, "alieleza.
Kwa upande wake Mratibu wa Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar, ZLSC tawi la Pemba, Safia Saleh Sultan aliwataka wananchi hao, kutoitegemea sana mahakama, kama msuluhishi mkuu wa migogoro ya ardhi.
Alifahamisha kuwa, njia mzuri ya utatuzi wa migogoro hiyo, ni kuvitumia vikao vya familia, viongozi wa dini, wasaidizi wa sheria na watu maarufu, kukukutana ili kujadili changamoto husika.
Akizungumza kwenye mkutano huo Mkurugenzi wa Jumuiya ya wasaidizi wa sheria wilaya ya Chakechake CHAPO Nassor Bilali Ali, aliwakumbusha wananchi hao kiyatumia mabaraza ya usuluhishi kuondokana na migogoro ya ardhi.
Alielelza kuwa, migogoro inapotatuliwa na jamii yenyewe huondosha visasi kwa waliokosana na amani huwepo ya kudumu miongoni mwao.
Akifungua mkutano huo sheha wa shehia ya Mfikiwa Bimkubwa Rajab Tangwi, alisema migogoro yote ya mada sio vyema walioko kukimbilia mahakamani.
Mwakilishi wa tasisi ya the foundetion for civil society Georgina Lund, amesema kazi inayofanywa na CHAPO, ndio hasa malengo ya tasisi yao ilivyopanga kwenye mradi huo.
"Wananchi wa shehia hii ya Mfikiwa, itumieni kamati yenu ya usuluhishi wa migogoro, maana upatanishi mtakaoupata hapa, utakuwa wa kudumu,"alisema.
Mwananchi Khamis Ali Khamis alisema wakati mwengine, serikali inaweza kuwa chanzo cha migogoro ya ardhi, ikiwa haitowashirikisha wananchi, wanapotaka kuchukua ardhi kwa miradi ya umma.
Nae Khamis Uled Mangi na mwenzake Asha Hassan Ali walisema, kukosekana kwa elimu kama hiyo, ni moja ya chanzo cha uwepo wa migogoro ya ardhi ndani ya jamii.
Hata hivyo mwananchi Zahran Mohamed Yussuf alisema bado kuna kasoro kwenye hati ya umiliki wa ardhi kwa kuwepo neno matumizi ya muda.
Mwisho
Comments
Post a Comment