Skip to main content

KUTOKA SKULI YA MWANZO JAMBANGOME HADI MSITU, ILIHAMISHIWA UWELENI MIAKA 300 ILIYOPITA

 



NA MOZA SHAABAN, PEMBA@@@@

KISIWANI Pemba, kuna kijiji kimoja chenye historia ya pekee, kijuilikanacho kwa jina la Jambangome.

Kijiji hicho kipo katika maeneo ya karibu na Wambaa, wilaya ya Mkoani, mkoa wa kusini Pemba.

Kipo umbali wa kilometa 31 kutoka mji mkuu wa Pemba wa kisasa Chake chake, ambapo ni umbali wa dakika 49  hadi saa moja, kwa usafiri wa gari  ambayo si ya abiria.

Jambangome ina historia kubwa na yakuvutia inapoelezwa kwa vizazi vya sasa na wageni wanaoingia na kutaka kuujuwa kiundani mji huo.

Kwani inaaminika mji huo, ndio wa kwanza kuhamiwa na kukaliwa na watu katika kisiwa hicho cha Pemba.

Historia inatueleza kuwa, Jambangome ilikaliwa na wahindi wa jamii ya Mabohora, ambao asili yao ni “Wagujurati” kutoka India.

Walihamia, baada ya kushauriwa na mababu zao kutafuta fursa mpya za kibiashara, katika ukanda wa Afrika mashariki, baada ya kupatwa na njaa kali huko katika jamii zao.

Neno hili “Bohora” linatokana na neno la kigujurati lenye maana biashara, ambalo asili yake ni India, na ni neno la utambulisho wa kihistoria kwa wafanyabiashara.

Inaaminika kuwa, Jambangome ulikuwa ni mji wa bandari na kitovu kikubwa cha kibiashara kisiwani Pemba, hususani kwa mkoa wa kusini.

 Na mji huo ulidumu kuanzia karne ya 18 hadi 20, kuanzia mwaka 1911/12.

Mataifa mbali mbali ya Asia, Europe na hata Afrika hasa Afrika ya Mashariki, walifika katika eneo hilo, kwa shughuli za kibiashara.

Ambazo zilifanya mji huo enzi hizo, kuwa ni miongoni mwa miji mikubwa ya Afrika mashariki na kati, kwa shughuli za biashara.



Ilikuwa ni jambo rahisi sana kwa wafanyabiashara hao kuingia katika mji huo kwa kutumia bahari ya Jambangome kutokana na jiografia yake.

Huku ikielezwa usafiri wa karne hizo, ulikuwa ni Mabedeni, Majahazi, na Mashua.

Wanahistoria wanaeleza, ingawa teknolojia ya ujenzi  haikuwepo enzi hizo, lakini majengo mazuri  na yenye thamani kwa wakati huo yalijengwa, huku mingine yakibeba shughuli za utawala na uongozi.

Hii ikiwa na maana, kulikuwa na maofisi mbali mbali ya kiutawala kama vile Polisi, Mahakama, Magereza na skuli ya mwanzo ilianzia hapo.

Na yote hayo yaliendeshwa na kusimamiwa na waarabu na wahindi, huku yakifanya kijiji hicho kuingia katika machapisho ya historia.

Kwa mujibu wa historia, inayoelezwa na Afisa mambo ya Kale Pemba Haji Seif Yussuf, anasema mnamo karne 19 mji huo, ulikaliwa na wahindi wa jamii ya mabohora na miongoni mwa majengo waliojenga ni skuli.



Anaeleza kuwa, eneo hilo lilijengwa kwa ajili ya watoto wao, ambayo ilibeba kumbukumbu ya kua skuli ya mwanzo, kujengwa katika kisiwa hicho kwa mujibu wa historia.

Anasema inagawa wahindi hao, walifika katika eneo hilo kwa ajili ya shughuli za biashara za bidhaa za viungo kama vile karafuu, lakini walijiimarisha na kuufanya mji huo kua ni wenye kuwavutia wengi.

ILIVYOJENGWA SKULI YA KWANZA PEMBA

Akitoa historia ya ujenzi wa skuli hiyo, ofisa huyo anasema hadi sasa, historia haijaweka wazi skuli hiyo ilikua na vyumba vingapi.

Na hii ni kutokana na kutofanyiwa utafiti wa kitaalamu, unaolenga kugundua mabaki ya vitu mbali mbali vya zamani yaani (Excavation).

“Kihistoria inaaminika skuli ya mwanzo kujengwa kisiwani Pemba, ilikua ni katika kijiji cha Jambangome wilaya ya Mkoani, ila bado hakujafanyika utafiti wa kitaalamu wa kugundua mabaki ya vitu vya zamani.

Kwa mujibu wa historia inayoelezwa na Afisa huyo  jengo hilo lilijengwa kwa zana za asili kama, mawe na chokaa, ambavyo kwa wakati huo, ndio vifaaa maarufu vya kujengea.

Ingawa vifaa vyake havikua vya kisasa, ila jengo hilo  lilikua na umadhubuti wa hali ya juu, uliosababishwa na utaalamu waliokua nao wajenzi wa jengo hilo, ambao ni wahindi wenyewe.

“Jengo la skuli ya mwanzo Pemba, lilojengwa Jambangome kwa kutumia mawe na chokaa, vifaa hivi sio vya kisasa, ila kwa wakati huo lilikua imara kuliko yanayojengwa sasa,’’anasema.

Wakati wa ujenzi wake, kazi zenye hadhi na thamani kama za usimamizi, zilikua zikifanywa na wenyewe wahindi, na wazawa walitumiwa kufanya kazi za nguvu ambazo hazikuhitaji ujuzi kama kubeba mawe na chokaa.

Jengo hilo halikuchukua muda mrefu kukamilika, kutokana na ufanisi na utayari waliokua nao wahindi, ambao ndio wajenzi wakuu wa skuli hiyo.

ELIMU ILIOSOMESHWA

Kwa mujibu wa ufafanuzi uliotolewa na Ofisa huyo, ni kwamba elimu iliotolewa ilikuwa ni hesabu ili kuwaandaa wanafunzi kua na uwezo wa  kudhibiti mali za mabwana (watawala) wa enzi hizo.

Soma la lugha ya kiengereza ilitolewa, ili watoto wao wapate fursa za kujumuika kibiashara kutoka kwa wafanyabiasha wa kiengereza, amabo walionekana kua na nguvu kubwa za kibiashara.

Mbali na lugha, inaaminika kwamba elimu ya  maadili na utawala ilitolewa, ili iweze kuwasaidia kuimarisha mahusiano ya kibiashara baina yao, pamoja na kujua mbinu za kiutawala na kuandaana katika uongozi.

“Skuli hii wanafunzi walisomeshwa masomo kama hesabu, ili waweze kusimamia biashara, maadili na lugha ili kuimarisha mawasiliano na mahusiano ya kibiashara, pamoja na utawala,’’anafafanua.

Kumbe wazawa wa Jambangome, hawakupata fursa za kusoma kwa wakati huo na  walibaki  kuwa ni wakulima ama wachukuzi (wapagazi), wavuvi au wafanyakazi wa majumbani pekee.

NJIA, VIFAA VILIVYOTUMIKA   KUSOMESHEA

Kwani mnamo karne ya 19 na 20, njia za kufundishia na kujifunzia zilikua si rasmi na muda mwingi, waalimu walitumia vifaa vya asili kulingana na mazingira yao.

Inasadikika waalimu waliosomesha skuli hiyo, walitumia vitabu na baadae kuhifadhisha wanafunzi kama ni njia yao kuu ya kufundishia.

Kwa njia hii, wanafunzi walilazimika kuhifadhi elimu waliopewa na waalimu wao, ili waweze kujibia mitihani pamoja na kuitumia katika maisha yao ya kila siku.

“Hapakua na njia rasmi ya kufundishia na kujifunza, hivyo waalimu walitumia njia za asili za kujifunzia, na walitumia vitabu kufundishia, wanafunzi walihifadhi kichwani elimu waliopewa”, anaeleza.

Historia inatuambia kabla ya Zanzibar, kupata uhuru wake hakukua na usawa katika upatikanaji wa elimu.

Hivyo elimu ilitolewa kwa kuangalia rangi, tofauti za kitabaka na kwa gharama kubwa, jambo lililowanyima wazawa fursa za elimu.

Maana Ofisa Mambo ya Kale Pemba, Haji Seif anasema skuli ya mwanzo Pemba waalimu wake walikua ni miongoni mwa wahindi, ambao ndio watawala na wajenzi wa skuli hiyo.

Kwani hawakuwapa fursa wazawa wa Jambangome kujifunza wala kusomesha wingine, hivyo walikosa sifa ya kua waalimu.

Kwani wanafunzi walikua ni watoto wa watawala wa eneo hilo, ambao walipewa kipaumbele zaidi, kutokana na aina ya elimu inayotolewa.


Kwani ililenga kuwaandaa kibiashara na kiutawala watoto wao na gharama za elimu iliyotolewa, hawakuimudu wazawa.

Mwishoni mwa mwaka 1911, (wazungu, wamishini–Missionaries) walifika Jambangome, kwa matembezi lakini baadae walifanya makaazi yao katika mji huo.

Hatimae walivamia na kudhibiti mianya yote ya mapato ikiwemo biashara, hali iliosababisha wahindi wa jamii ya mabohora kusambaratika.

Ambapo walienea katika miji mbali mbali ya Pemba ikiwa ni miji ya Chake chake, Kengeja  na Mkoani ambayo kwa sasa, ndio miji yenye mvuto kwa kisiwa cha Pemba.

Baada ya muda kupita, ndipo skuli hiyo ilipo hamia katika mji wa Mkoani, na sasa inajuilikana kama skuli ya Uweleni.

Ilikua mwaka 1932, ambapo kwanza ilijuilikana kwa jina la Mkoani Government School, chini ya uongozi wa Abdallah Sadalla, akiwa ni mwalimu mkuu wa mwanzo.

skuli ya Uweleni Mkoani Pemba

Mwaka 1959 skuli hio, ilifanywa kuwa ni ya wanaume  pekee na hivyo kubadilishwa jina na kuitwa ‘Mkoani Boys School’.

Mwaka 1969, ilifanywa tena kuwa skuli ya mchanganyiko wa wanafunzi wanaume na wanawake na kubadilishwa jina na kuitwa skuli Uweleni.

Mwaka huo huo wa 1969, skuli hiyo ilipandishwa daraja na hivyo kufunguliwa sekondari ya  mwanzo.

Baadae mwaka1988, ilipandishwa daraja na kuwa skuli ya sekondari tu, baada ya kufunguliwa darasa la 12 kubadilishwa jina na kuitwa skuli  ya sekondari Uweleni.

Mwaka 2005, skuli hii ilipandishwa tena daraja na hadi sasa inatoa elimu ya juu ya kidato cha tano na sita.

Ambapo ikiwa ni skuli pekee ya kiwango hicho kwa wilaya ya Mkoani, hadi mwaka 2018 ilipofunguliwa rasmi skuli ya MOHAMMED JUMA PINDUA.

HALI ILIVYO KWA SASA

Katika eneo hilo la kihistoria la Jambangome, kwasasa kumebakiwa na magofu na vijumba vidogo vidogo vya wazawa.

Ambapo mabaki ya skuli hiyo ya mwanzo kujengwa Pemba, yamezomgwa na majani na miti mikubwa ya Mlandege.

Waswahili wanasema, chakale ni dhahabu, wakimaanisha chochote cha zamani kina thamani zaidi.

Hivyo ni jukumu la kila mmoja kuhakikisha analinda anapigania na kutunza historia ya Zanzibar kwa manufaa ya kizazi chote cha kizanzibari.

Kwani mabaki hayo ya skuli na mji wa Jambangome  yatakapoachwa bila matunzo, tutawaachia nini watoto wetu na vijukuu vyetu juu ya mji huo wa mwanzoni mwa karne ya 18.

                            MWISHO

Comments