NA ALI SULEIMAN, PEMBA
TAREHE 6 Disemaba mwaka jana, ilikuwa
siku pekee ya kihistoria kwa wazanzibari kuzaliwa upya kisiasa.
Hii ilikuwa
ni kufuatia kitendo cha rais wa Zanzibar Dk. Hussein Mwinyi, kumteua Maalim
Seif Sharif Hamad kuwa Makamu wa Kwanza wa rais.
Kitendo
hicho cha kikatiba, kilihusisha uungwana, ubobevu wa kisiasa, ukweli, nia ya
kimaendeleo, utayari wa kuwaunganisha wazanzibari, kwa viongozi wetu hawa
wawili.
Maana
walishasema wazee wa zamani kuwa, muungwana ni vitendo, na chanda chema
huvishwa pete, haya yanashabihiana mno na hapa kwetu Zanzibar kwa tendo hilo.
Maana
viongozi wetu wakuu, marehemu Maalim Seif Sharif Hamad na Dk. Hussein Mwinyi
ambao kwa upande mmoja ni viongozi wa vyama vya siasa, kwa kule kuungana kuunda
serikali ya pamoja.
Ingawa
uundaji wao wa serikali hii ya Umoja wa Kitaifa, umeelezwa ndani ya Katiba ya
Zanzibar ya mwaka 1984, kufuatia marekebisho ya 10, pia yaliofanywa mwaka 2010.
Awali,
Zanzibar ilishaanza mingurumo ngurumo ya kutaka kuchafuka kwa amani yetu, na
hasa baada ya kumalizika kwa uchaguzi mkuu wa vyama vingi, mwaka jana 2020.
Na
inawezekana wapo mabeberu, wakoloni wa kileo, wafitinishaji na wasiotakia mema
Zanzibra, walitamani kuona tunarudi kule, ambako tumeshakupita.
Maana,
wazanzibari walishavuuka kwenye kugomeana, kutengana, kupigana, kubaguana,
kuwekeana chuki, na sasa kuanzia baada ya uchaguzi mkuu na kuendelea, hayo
yameshazikwa.
Na ndio
maana, sasa serikali yetu ya Mapinduzi ya Zanzibar, imeshatimia, kwa kule kuwa
na serikali hiyo, ingawa yenye mfumo wa Umoja wa Kitaifa umaarufu ‘SUK’.
Ni mfumo,
ambao upo kikatiba, ambapo Makamu wa Kwanza inaelezwa kwenye Katiba hiyo kuwa,
atatoka ndani ya chama kilichoshika nafasi ya pili, huku Makamu wa Pili akitoka
kwenye chama anachotoka rais.
VYAMA VINASEMA JE JUU YA MARIDHIANO
HAYO
Hapa Makamu
wa Kwanza, ambae kisiasa anatoka chama ACT-Wazalendo, marehemu Maalim Seif
Sharif Hamad, alisema haikuwa kazi rahisi mpaka yeye kukubali kuingia kwenye
mfumo huo wa serikali.
Mara zote,
anapokutana na makundi ya wazazibari, husema bila kigugumizi kuwa, alikubali
hilo baada ya yeye kupokea ushauri kutoka kwa wazanzibari kadhaa, wakiwemo
wanachama wake.
Alikuwa
akielezwa faida ya kushirikiana kwenye serikali ya Umoja wa Kitaifa na hasara
ambayo wazanzibari wengeipata kwa miaka mitano ijayo.
“Mimi
nimeingia kwenye maridhiano haya kwa ajili ya kuiweka Zanzibar yetu, katika
mawanda mapana ya kutokomeza chuki, hasama, kubaguana, kutoaminiana na hasa kwa
vile, sote ni wa wamoja,’’aliwahi kusema wakati wa uhai wake.
Hata hivi
karibuni, alipokutana na wananchi wa wilaya ya Mkoani, marehemu Maalim Seif
alisema alichoangalia yeye kwanza ni kurudisha umoja wa wazanzibari, ambao walikwisha
uzoea kuishi kwenye amani na utulivu.
Anafafanua
kuwa, ikiwa maradhiano yameshafikiwa na viongozi wakuu, sasa asibakie mwengine
kupalilia chuki, hasama, utengano na ubaguzi, kwani hivyo sio asili ya
wazanzibari.
Hata
alipokuwa wilaya ya Micheweni Pemba, Makamu huyo wa Kwanza alirejea kauli yake,
ya kuwataka wananchi wa Zanzibar kuunga mkono maridhiano hayo.
Anasema kila
mmoja ni mshindi, na kila mmoja ana haki na fursa sawa kama mwenzake, hivyo
hakuna sababu kwa wenye mamlaka kuwabagua wengine.
“Sasa
tunaishi kwenye maruidhiano, yanayoambatana na amani na utulivu, kama kuna
sheha, mkuu wa wilaya, mkuu wa mkoa na wengine watende haki kama anavyosimamia
Rais Mwinyi,’’anafafanua.
Hata Rais wa
Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi,
akizungumza mara baada ya kumuapisha Makamu huyo wa Kwanza, alitaka maridhiano
hayo yaungwe mkono.
“Leo
tumeshamuapisha Maalim Seif Sharif Hamad, na Zanzibar sasa imeshazaliwa upya,
ni wajibu wetu wananchi kuunga mkono hili, maana ndio hatua ya kwanza ya kuelekea
kwenye Zanzibar mpya,’’anasema.
Lakini Dk.
Mwinyi, hata alipokuwa akizungumza kwenye siku ya maadili, alirudia kauli yake
ya kuwataka wazanzibari kuhakikisha kuwa, wanayalinda kwa gharama yoyote
maridhiano hayo.
Alikwenda
mbali zaidi, akisema kila mmoja kwa alipo awe mwandishi wa habari, kiongozi wa
dini, kiongozi wa chama cha siasa na vyama vya wafanayakazi, lazima hili
walikumbuke.
Akawatanabahisha
wazanzibari, kuwa azma yake na viongozi wenzake ndani ya serikali yenye mfumo
wa umoja wa kitaifa ,wanayo dhamira ya kweli ya kuwatumikia.
Anasema,
mipango, mikakati na mbinu za kuhakikisha wanageuza maisha yao, ipo vyema
wanachotakiwa kwao ni kuwajibika, kama anavyowakumbusha wasaidizi wake.
“Kila mmoja
afanye kazi kwa bidii, hamasa, ukweli, uwazi, uwajibikaji, ili haya maridhiano
tuliofikia sasa yawe fursa ya kufikia uchumi wa bluu,’’anasisitiza.
Katika
upande mwengine Kaimu Katibu Mkuu wa chama cha wananchi CUF Zanzibar, Mbarouk
Seif Salim, alisema suala la maridhiano ni jambo jema, hasa kwa makundi
yaliokosana katika jambo fulani.
Ingawa
alisema, suala la maridhiano ya Zanzibar, wengetamani mno kushirikishwa kwa
vyama vyote vya siasa , ingawa kwa upande wa kushiriki kwenye serikali ya Umoja
wa Kitaifa ni jambo la vyama vya CCM na ACT-Wazalendo.
“Mimi naona
maridhiano ni jambo jema, lakini yengependeza zaidi, hata vyama kama CUF,
CHADEMA, AAFP, ADC, Demokrasia Makini, navyo vyengeitwa na
kushirikishwa,’’anasema.
Aliyekuwa
mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya chama cha ‘ADC’ Hamad Rashid Mohamed,
amesema kwanza anaunga mkono maridhiano hayo, kwa vile ADC haipendi kuona hata
damu ya kunguni, ikimwangika.
Anasema,
maridhiano yaliofikiwa Zanzibar ndio mbolea ya kweli ya kuchapuza maendeleo, na
itapelekea maendeleo yatakayopatikana siku zijazo, kila mmoja kuwa mlinzi, kwa vile
atakuwa ameshiriki kwa njia moja ama nyingine.
Anasema amefurahishwa
mno na uwepo wa maridhiano na hasa kwa vile Rais wa Zanzibar Dk. Hussein Ali
Mwinyi ni mkweli, mjasiri, mpenda maendeleo na mwenye nia thabiti ya kuipata
Zanzibar mpya kiuchumi.
“Mimi
niwatake wakuu wa vyama, ambavyo hadi sasa vinashindwa kuridhia makubaliano
yaliofikiwa na viongozi wetu, waweke kando tofauti zao za kisiasa na tuungane
kuwajengea watoto wetu Zanzibar mpya.
Kama hayo,
pia yanaungwa mkono kupitia ADA-Tadea kwa aliyekuwa mgombea wa urais wa
Zanzibar kwa chama hicho, Juma Ali Khatib, akisema kasi ya maendeleo ya
Zanzibar, itatiwa mbolea na maridhiano hayo.
Khatib ambae
pia kwa sasa ni Mjumbe wa kuchaguliwa na rais wa baraza la Wawakilishi, anasema
suala la maridhiano, yaliofikiwa Zanzibar ni ukomavu wa kisiasa kwa
wazanzibari.
Anasema zipo
nchi kadhaa wananchi wake wamekuwa wakizihama baada ya kumalizika kwa uchaguzi
mkuu, kutokana na mchafuko na mapigano ya wenyewe kwa wenyewe ‘civil war’
ingawa Zanzibar hali ni shuwari.
“Sisi
ADA-Tadea kwanza tunaunga mkono maridhiano hayo, tukiamini kuwa, maendeleo ya
kweli, uchumi wa bluu na Zanzibar ya viwanda, haiwezi kujengwa kwenye
machafuko, chuki na kubaguana,’’anafafanua.
Mwenyekiti
wa Chama cha UMMA Mkoa wa kusini Pemba Mrayam Saleh Juma, anasema suala la
kuwepo kwa maridhiano hayo ni jambo jema, kwani wakosanao ndio wapatana nao.
Anasema, kwa
upande wao watahakikisha wanawaelimisha wananchi, ili kuona maridhiano
yaliofikiwa Zanzibar, yanakuwa endelevu, kwa maslahi mapana ya wazanzibari
wenyewe.
Anasema,
ingawa zipo kasoro zilizojitokeza, lakini sasa ni vyema kwa wananchi wa
Zanzibar, kuungana pamoja ili kuhakikisha wanaijenga nchi yao, kwa maslahi
mapana ya taifa.
“Sisi kama
Chama cha UMMA, tunayaunga mkono maridhiano hayo, maana bila shaka waliofikiria
kukutana ni kwa ajili ya maslahi ya watu wote,’’anafafanua.
Ingawa nae
alipendekeza, ni vyema maridhiano hayo yasitafsiriwe kama vile ni ya vyama
viwili ya ACT na CCM, bali ni vyama vyote na wazanzibari wote.
Hata
Mwenyekiti wa chama cha wakulima ‘AAFP’ Said Soud Said, amekuwa akinukuliwa na
vyombo vya habari, akiwataka wazanzibari kuunga mkono maridhiano hayo.
MAKUNDI MENGINE YA KIJAMII YANASEMAJE
Mufti wa
Zanzibar sheikh Saleh Omar Kaabi, amewasisitiza viongozi wa dini ya kiislamu na
wale wa kikiristo, kuendelea kuzitumia nyumba za ibada, kuhubiri umoja,
mshikamano, maridhiano na amani, kwani huo ndio utamaduni wa waumini.
Akizungumza
hivi karibuni, kwenye kongamano la amani, lililofanyika Chake chake na
kuandaliwa na Kamati ya pamoja ya viongizi wa dini Zanzibar, suala la kuishi
kwa upendo, umoja, mshikamano, maridhiano na kusameheana ndio nguzo kuu kwa
waumini.
“Sisi
viongozi wa dini, ambao kila siku tunakutana na waumini wetu kwenye nyumba za ibada,
tuendelee kuwanasihi kuishi kwa upendo, amani, maridhiano na
mashikamano,’’alieleza.
Mapema
Father Damas Mfoi, kutoka Kanisa Katoliki Unguja, anasema, umoja na mshikamano
unahusisha dini zote, hivyo hakuna haja ya kubaguana.
Alisema,
kila dini inahimiza umoja, mshikamano na kuishi kwa kusaidiana, hivyo ni vyema
wakashirikiana, ili jamii ya Zanzibar isigawanyike, kwa sababu ya kuamini dini
waipendayo.
“Sisi
wajumbe wa Kamati ya pamoja ya viongozi wa dini Zanzibar, tunashirikiana bila
ya kujali imani zetu, lazima na wananchi wote, tuwahubirie amani, maridhiano na
upendo,’’alieleza.
Kwa upande
wake Father Zeno Marandu kutoka Kanisa la Roman Katoliki ‘RC’ Chake chake, anasema
ushirikiano ndio msingi mkuu wa maisha ya mwanadamu.
“Lazima
tuishi pamoja, tuishi kama kiwili wili kimoja, na imani zetu za dini
zisitugawe, kwani hakuna dini inayohimiza chuki wala mfarakano,’’alieleza Zeno.
Akaenda
mbali zaidi, akashauri kuwa maridhiano yaliofikiwa kwa viongozi wakuu wa vyama
vya siasa kufanya kazi pamoja, ni silaha ya kumshinda adui.
Sheikh
Nassor Hafidh Mohamed wa Mkoani, alisema maridhiano yaliofikiwa, kila mmoja
yanamgusa kwani amani na utulivu ni tunda la watu wote.
Hivi karibu
Klabu ya Waandishi wa Habari Pemba ‘PPC’ kwa kushirikiana na shirika la
Intenews, liliwawezesha waandishi wa habari, kuandika habari za maridhiano na
amani.
Ambapo
kwenye mkutano huo wa siku moja, mwandishi mwandamizi Khatib Juma Mjaja,
aliwakumbusha waandishi hao kuwa wabunifu wa uteuzi wa maneno.
Anasema,
hata kalamu ya mwandishi wa habari, inaweza kuviza maridhiano na amani iliyopo
Zanzibar, ikiwa hawatokuwa waangalifu.
“PPC kwa
kushirikiana na Internews wameona ni bora kuwajengea uwezo nyinyi waandishi wa
habari hapa kisiwani Pemba, katika kipindi nchi ikiwa kwenye maridhaino musiwe
chanzo cha kuharibu yale yaliofikiwa na viongozi wetu wakuu,’’alisema.
Waandishi wa
habari Kheir Juma Basha na Juma Mussa Juma, walisema, jambo lililofanywa na PPC
na Internews ni jema.
Mwisho
Comments
Post a Comment