NA FATMA
HAMAD, PEMBA
ABDALLA
Hussein Rashid, ni kijana mwenye ulemavu wa mchanganyiko, sasa yuko darasani,
akijumuika na wenzake kusaka haki yake ya elimu.
Hakuna aliyefikiria kwamba, kijana huyo engefikia darasa la
kumi (FII) skuli ya sekondari Kinyasini, maana changamoto ya mwendo, ukosefu wa
mkalimani yote ameyavaa.
Abdalla miaka 18, alizaliwa akiwa na mguu mmoja, huku akiandamwa
na uziwi na ulemavu wa matamshi, ambapo mama yake mzazi hakuwa na tamaa ya
kupata elimu kwa mtoto wake.
SAFARI YA
MAISHA YA ABDALLA
Baada ya kuzaliwa miaka 18 iliyopita kijijini kwao Kwale Gongo
Wete Pemba, mama mzazi alianza safari ya kila hospitali, ili kuhakikisha tatizo
la mguu linapona.
“Nilifika na mwanangu hospitali ya Unguja, baada ya kuzimaliza
za Pemba, ingawa kisha, akiwa ni miaka mitatau alianza kutumia mguu wa bandia,’’anaeleza
mama yake.
Mama yake Abdalla, bibi Time Kombo Juma ambae huyo ni mtoto
wake wa wanne , anasema safari ya mtoto wake, ilikuwa ni ya kukata tamaa zaidi
kuliko mafanikio.
Mguu wake wa bandia, aliyopewa baada ya miaka mitano,
alilazimika kuuwacha kutokana na kuendelea kumuumiza sehemu ya kifundo cha
mguu.
Ambapo, kutokana na kukosa shilingi 500,000 za kununua mguu
mwengine kwa wakati huo, sasa kijana wake alianza kutumia magongo maalum.
“Magongo yalikuwa yanamsaidia kwenda safari zake za hapa na
pale, na hadi pale alipoanza madrassa mwaka 2012 na kisha mwaka 2014 alipoanza safari
ya elimu ya msingi,’’anasema.
ABDALLA
NA SAFARI YA ELIMU
Mwaka 2015, wakati
akiwa na usaidizi wa magongo, alilazimika kutembea kilomita 5 kila siku za
kwenda na kurudi skuli, masafa yaliopo nyumbani kwao hadi skuli ya Kinyasini.
“Ilinibidi kila siku
nitoke mapema mno kwenda skuli, kwa sababu magongo kama visaidizi hupati kwenda
haraka haraka, lakini sikuwa kuchelewa skuli hata siku moja,’’anasema.
Nikiwa karibu na mama yake mzazi, akinisaidia ukalimani kwa
Abdalla ambae kwa sasa ni mwanafunzi wa darasa la 10 (FII) skuli hiyo ya
Kinyasani, anasema hamu yake ni kuwa fundi.
Nipotaka kujua ufundi wa aina gani, anasema ule unaokusanya
masuala ya umeme iwe redio ama simu, kazi ambayo kwa sasa anendelea kuonesha
utundu wake.
Mara anaporejea kutoka masomoni, hukusanya redio, Baskeli na
simu mbovu kuanza kuzirekebisha na zipo anazofanikiwa, na kujiingiza fedha japo
ndogo.
Changomoto anasema anyoivaa akiwa masomoni kuanzia darasa la
kwanza hadi leo hii akiwa darasa la kumi, ni kukosa mkalimani wakati mwalimu akisomesha.
“Wenzangu wananiacha nyuma mno, na kila mwaka mimi huwa
mwanafunzi wa mwisho, maana inabidi nimuangalie mwalimu mdomo mwanzo
mwisho,’’anasema.
Tunu yake kwanza ni kuona anasonga mbele na kufikia hadi chuo
kikuu, ili aisaidie familia yake, ambayo anasema imefanya juhudi kubwa hadi leo
kufikia elimu ya darasa la 10.
Abdalla ni kijana wa aina ya pekee kutokana na kutopenda
kukata tamaa, na kuwataka wenzake hasa wenye ulemavu ,atambue wajibu wao.
“Kama skuli yangu ya Kinyasini yengenipatia mkalimani kuanza
darasa la kwanza hadi leo hii, mbona mimi ningewabeba wote wanafunzi darasani,’’anafafanua.
MWANAFUNZI
MWENZAKE
Amour Hamad Issa anasema ,ubongo wa Abdalla uko vyemo mno,
ingawa changamoto iliyopo ni ya wizara ya elimu kwa kukosekana kwa wataalamu.
Pamoja na kwanza pia Abdalla ni kiziwi, lakini yapo baadhi ya
masomo mimi kama darasani sikwenda ananifahamisha yeye.
RAFIKI
WAKE WA MTAANI
Omar Hassan Ali, anasema mara Abdalla anaporudi skuli,
anautamaduni hadi leo kukimbilia madrasa, na amekuwa na juhudi kuliko mtu
mwengine mtaani kwetu.
Kazi kubwa ambayo huwenda ikamganda hapo baadae ni ufundi,
mara anatengeneza tv, simu, redio na hata suala la kuchonga chonga haliko mbali
nae.
“Kama serikali inawajali kwa vitendo watu kama Abdalla, suala
la mitihani ya darasani kwao isiwe kigezo cha kufaulu na kufeli, bali
waangaliwe wanachofanya,’’anashuri.
MAMA
MZAZI
Anasema kwa alipofikia mtoto wake hadi darasa la kumi na
mwishoni mwa mwaka kufanya mitihani, ni hatua moja kubwa.
“Kwakweli kama asipofaulu hatujajua tufanye nini, maana
kutokana na hali yetu ya kimaisha, tunahitaji msaada wa hali na mali ili afikie
ndoto zake,’’anasema.
Akili yake inatuma na kushika vizuri mno, lakini sasa
miundombinu ya elimu kwa ajili ya watu kama Abdalla, haipo skuli ya Kinyasini.
MWALIMU
WAKE
Asha Mbaruok Rashid ndio mwalimu wake skulini hapo, anapochukulia
elimu kijana Abdalla mwenye ulemavu mchanganyiko, anasema changmoto ni
kutokuwepo mwalimu mwenye mbinu.
“Ijapokuwa skuli yangu ina walimu 12, lakini hakuna hata mmoja
aliyewahi kupata mafunzo ya utaalamu wa kuwasomesha wanafunzi wenye ulemavu
kama Abdalla,’’anasema.
Bidii, nidhamu, heshima na hamu ya mwanfunzi Abdalla, imekuwa
ikikatishwa tamaa na wizara, kwa kule kutokuwepo kwa waalimu wenye sifa.
“Darasa analosoma Abdalla linawanafunzi 42, lakini kila mwaka
tukipima matokeo yeye anakuwa anashika mkia, inasikitisha,’’anasema.
MWALIMU WA MADRSAA
Mwalimu wa Madrasa anayosoma Abdalla, ustaadh Omar Hussein
Rashid anasema, licha ya vikwazo vinavyomkabili, lakini anabidii na anaonesha
anahamu ya kusoma.
“Pamoja na ulemavu mchanganyiko, lakini kwa sasa mas-hafu
ameshakaribia kuumaliza, na ameshasoma juzuu 18, na anaendelea na
hajakatisha,’’anasema.
WANAFUNZI
WENZAKE
Nao wanafunzi wanaosoma na Abdalla, walisema hana shida wamekuwa
wakishirikiana nae, licha ya kwamba kuna baadhi ya wakati hawamuelewi vizuri,
lakini wamekuwa wakimpa ushirikiano makubwa.
JIRANI WA
ABDALLA
Said Asaa, anasema kuwa kwanza wanawashukuru wazazi wa Abdalla
kuwa hawajambaguwa mtoto wao huyo, na wanampatia kila haki yake ikiwemo ya elimu.
Licha ya ulemavu
alionao Abdalla, lakini ukimuangalia unaona ni mtu mwenye uwezo mkubwa na bidii
ya jambo analohitaji kulipata, na ni muelewa kuliko vijana wengine.
Hata hivyo mzee huyo aliwashauri wazazi wenye watoto kama hao,
kutowabaguwa kwani Mwenyeezi Mungu ameshawajaalia waupokee mtihani huo.
BARAZA LA
TAIFA LA WATU WENYE ULEMAVU
Mratibu wa baraza la
taifa la watu wenye ulemavu
kisiwani Pemba Mashavu Juma Mabrouk, anasema
suala la uhaba wa walimu mjumuishi bado ni tatizo.
Hivyo ameishauri wizara
ya elimu kuwapa kipaumbele walimu ambao wamesomea fani ya ukalimani, wakati
zitakapotokea ajira ili kuona changamoto hiyo imeondoka.
‘’Niishauri wizara ya elimu wakati itakapotoa nafasi za ajira
kuwajiri walimu wengi waliosomea elimu mjumuishi, ili kuona wanafunzi wenye
ulemavu kama wa Abdalla nawao wamefaidika na elimu,’’ anaeleza.
WIZARA YA
ELIMU
Kaimu Mratibu Elimu Mjumuisho na Stadi za Maisha ‘EMSM’ Pemba Halima Mohamed Khamis, anasema
ujio wa dhana hiyo, ndio iliyokomboa watoto wenye ulemavu na wale wenye
mahitaji maalum, sasa kupata haki yao ya elimu.
Awali watoto wenye ulemavu wa aina mbali mbali, waliachwa bila
ya kupatiwa elimu, kuanzia ngazi ya jamii na serikali kuu.
Lakini ilipofika mwaka 1991, serikali kupitia wizara ya Elimu,
ilianzisha madarasa maalum, kwa ajili ya wanafunzi wenye ulemavu wa akili,
ambapo kwa Pemba ni skuli za Michakaini na Pandani msingi.
Kisha mwaka 2006, sasa kukazaliwa dhana ya elimu mjumuisho,
ambayo ni ule mpango wa kuwaweka darasa moja, kati ya wanafunzi wenye mahitaji maalum
na wale wengine.
Mpango huo ulianza kwa kusua sua, maana ulikuwa mpya kwa
wanafunzi wenye mahitaji na wale wengine, ambapo hadi sasa, wapo waalimu watano
wenye ‘Master’ 10 wenye shahda ‘Degree’
wakati wenye diploma 20 na 68 ngazi ya cheti wote wana fani ya Elimu ya
Mahitaji Maalum ‘SNE’
‘’Licha ya takwimu hiyo, lakini bado tunashida ya walimu
mjumuisho, hivyo tunaiomba wizara husika kuliweka somo la lazima katika vyuo,
ili kila mwalimu akitoka chuoni aweze kusomesha wanafunzi wenye
ulemavu,’’anasema.
Wanafunzi wenye uoni hafifu 803, wenye usikivu hafifu 690, wenye ulemavu wa matamshi 405, wenye vichwa vikubwa na vidogo 22 wakiendelea na masomo katika skuli mbali mbali kisiwani Pemba.
Kundi jengine ni wenye umbilikimo 13, mgongo wazi saba ,
ulemavu wa akili 111, ulemavu mchanganyiko 113 na ulemavu wa viungo wanafunzi
91.
SHERIA YA WATU WENYE ULEMAVU
Haki ya elimu, imetajwa kwenye kuanzia kifungu cha 9 hadi cha
10 sheria ya watu wenye ulamvu Zanzibar nambari 9 ya mwaka 2006.
“Chuo kitachotoa mafunzo lazima kizingatie mahitaji maalum kwa
watu wenye ulemavu, ikiwemo mtaala, alama, mitahani, vifaa husika,’’ndivyo
sheria inavyoeleza.
Ingawa sheria iko
kimnya juu ya hatua zinazofaa kuchukuliwa na mtu mwenye ulemavu, iwapo amekwenda
chuoni au skuli na hakuna miundombinu rafiki.
Abdalla alizaliwa miaka 18, kijijini kwao Kwale Gongo wilaya
ya Wete mkoa wa kaskazini Pemba, akiwa ni mtoto wa 4 kutoka kwa familia ya bwana Hussein Rashid.
MWISHO.
Comments
Post a Comment